CHAVITA YALIA NA KUSAHAULIWA NA SERIKALI. Na. Barakaelly Mosi
Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) kimesikitishwa na kitendo cha Serikali kuwasahau katika mipango yake na kuwafanya walemavu kuwa omba-omba kutokana na kusahauliwa huko. Hayo yalielezwa na washiriki wa mjadala wa kuangalia changamoto za walemavu wasiosikia (Viziwi) lililoandaliwa na CHAVITA kwa ufadhili wa Jumuia ya Kiraia ya The Foundation for Civil Society.
Washiriki wa mjadala huo walisikitishwa na kitendo cha serikali kushindwa kuajiri wataalam wa lugha ya alama katika taasisi zake muhimu kama Polisi, Mahakamani, Bungeni, Hosipitali, ofisi za Halmashauri na Televisheni ya Taifa ili kurahisisha uwasilishaji wa taarifa kwa walemavu hao bila sababu zozote za msingi.
Washiriki hao walisema kuwa serikali haina nia ya dhati ya kuwapatia wenye ulemavu wa kusikia haki yao ya msingi ya kuwapatia taarifa kutokana na kuwa wataalam wa lugha ya alama wapo; taasisi zake zinazo fedha za kuweza kuwaajiri lakini hawafanyi hivyo, tatizo ni nini? walihoji.
Aidha walieleza kuwa chama chao kiko tayari kutoa mafunzo kwa watu mbalimbali wenye nia ya kujifunza lugha ya alama ili waweze kurahisisha mawasiliano baina yao miongoni mwa jamii. walitoa rai kwa mashirika, taasisi na vyama mbalimbali vya kiraia kuwa na utaratibu wa kujifunza luhga ya alama ambayo walidai ni rahisi kujifunza na kueleweka kwa urahisi.
******************************************
MARAFIKI WA ELIMU WAJADILI MSWADA WA SHERIA YA UZAZI SALAMA
Na. Davis. Makundi
Wanaharakati wa Elimu kupitia asasi ya Marafiki wa Elimu Dodoma wamepata fursa ya kuijadili rasimu ya Mswada wa sheria ya uzazi salama 2012; na kutoa maoni yao juu ya namna ya kuuboresha mswada huo ambao baadaye utakuwa sheria kamili baada ya kupitishwa na Bunge na kusainiwa na Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wawakilishi wa Club za marafiki wa Elimu kutoka katika shule za Sekondari za Kikuyu ambayo ni ya serikali na shule binafsi ya Jamhuri zote kutoka Manispaa ya Dodoma; walionesha ushiriki wa hali ya juu katika kuchangia mawazo juu ya mswada huo uliofanyika katika ukumbi wa CCT mjini Dodoma.
Mjadala huo ulioandaliwa kwa ushirikiano baina ya mashirika ya CARE International, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) na Shirika la Utepe Mweupe ambapo Mkoani Dodoma mwenyeji wa mashirika hayo ilikuwa asasi ya Marafiki wa Elimu Dodoma (MED).
Washiriki hao walipendekeza kuwa katika mtaala wa elimu liwepo somo la Afya ya Uzazi kwa wanafunzi wa kuanzia angalau darasa la tano na kuendelea hadi katika vyuo ili kuifanya jamii ipate uelewa wa kutosha kuhusiana na suala la uzazi wa mpango na manufaa yake katika jamii na taifa.
Ili kuepuka suala la ndoa za utotoni ambalo licha ya kuwa sasa linapigwa vita na watu mbalimbali huku sheria ikitoa mwanya wa uwepo wa ndoa hizo; washiriki hao walipendekeza muda wa kufunga ndoa uwe angalau miaka 21 muda mambao kwa mtoto wa kike atakuwa angalau amehitimu elimu ya sekondari.
Majadiliano hayo pia yaliambatana na maswali na majibu kutoka pande zote zilizoshiriki (Wawezeshaji na wanafunzi) ambapo kila upande ulionesha umahiri mkubwa katika kuuliza na kujibu maswali hayo. Katika mjadala huo maswali kuhusiana na sheria ya makosa ya kujamiiana 1999 na maswali yahusianayo na Afya ya uzazi yaliulizwa kwa wingi hali iliyoufanya mjadala huo kutoa nafasi kwa idadi kubwa ya washiriki kuchangia.
Washiriki waliomba serikali, taasisi mbalimbali na asasi zisizo za kiserikali kuwezesha kufanyika kwa mijadala ya aina hiyo mara kwa mara ili kukuza uelewa wa wanafunzi na Club za marafiki wa Elimu ili elimu hiyo iyafikie makundi mbalimbali ya jamii kwa haraka.
Akifunga mjadala huo Meneja wa Miradi kutoka sherika la CARE International Bw. David Lyimo aliwataka washiriki kuimarisha Club zao na kuongea bidii katika masomo ili kuwa mfano katika jamii ndani na nje ya shule kwa kufanya vyema kila wakati katika masomo yao pamoja na tabia zao kwa ujumla.
MCHAKATO WA KUPATA WAJUMBE WA BODI YA MED WAANZA. Na. Bentez Fares.
Asasi ya Marafiki wa Elimu Dodoma (MED) imeanza mchakato wa kutafuta Wajumbe wa Bodi yake kwa ajli ya kusimamia shughuli za Asasi hiyo. Mchakato huu umeanza siku chache baada ya MED kuwasilisha Katiba na vielelezo muhimu kwenye Ofisi ya Msajili wa Asasi za Kiraia katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na kuahidikwa kupata hati ya usajili ifikapo Ijumaa ya tarehe 10 Februari; 2012.
Katiba ya MED inaelekeza kuwa kutakuwa na Bodi ya Ushauri ya MED ambayo itasimamia Sekretarieti ya MED katika utekelezaji wa wa majukumu na kuwasilisha taarifa yake kwenye Mkutano Mkuu wa Wanachama.
Bodi ya MED itakutana mara nne kwa mwaka katika vikao vyake vya kawaida na pia inaweza kuitisha mkutano wa Bodi wa dharura wakati wowote itakapoonekana inafaa kufanya hivyo.
Ili kuwepo na uwiano wa kijinsia katika Bodi hiyo; Katiba ya MED inaelekeza kuwa wajumbe watakuwa tisa na kati yao lazimama watatu kati yao wawe wanawake. Kwa mujibu wa katiba hiyo; wanawake wanaweza kuchaguliwa kwa idadi yoyote kuingia kwenye Bodi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya MED wajumbe wa Bodi wanapaswa kuomba kupata nafasi hizo. Asasi ya MED ni miongoni mwa asasi chache za Mkoa wa Dodoma zinazo juihusisha na Elimu, Demokrasia, Utawala Bora na utetezi wa Haki za Wanafunzi.
MED Yaanza Mchakato wa kupata Usajili wa Kudumu. (Na Prince Kimaro)
Asasi ya Marafiki wa Elimu Dodoma (MED) imeingia katika mchakato wa kupata usajili wa NGO ili kuongeza ufanisi katika kazi zake baada ya kufanya kazi kama CBO kwa kipindi cha miaka mitatu.
Mratibu wa MED na mwanaharakati wa Elimu na Maendeleo Mkoani Dodoma Bw. Davis Makundi amesema ana uhakika kwa kazi zilizofanywa na MED katika hatua ya CBO; zinatosheleza sasa kujikita katika hatua ya juu zaidi ya kuwa NGO ili kufanya kazi katika eneo kubwa zaidi Mkoani Dodoma.
Bw. Makundi pichani alieleza kuwa anajua kuwa eneo alilochagua ni gumu na lina changamoto nyingi ambazo zitahitaji umakini katika kuzikabili na kufikia malengo ya uwepo wa asasi hii. "Sekta ya Elimu; suala la Demokrasia; changamoto ya Utawala bora na haki za makundi mbalimbali wakiwemo vijana hasa wanafunzi, wanawake, wenye changamoto za ulemavu nk tutazifanyia kazi kwa umakini mkubwa ili kurejesha faraja kwa makundi hayo.
Bwana Makundi amesema MED itasajiliwa kama NGO itakayo fanya kazi zake katika Mkoa wa Dodoma na kujihusisha na uhamasishaji katika kuboresha Elimu, Demokrasia, Utawala Bora, haki za wanafunzi, kuimarisha mawasiliano baina ya jamii na serikali pamoja na kupambana na umaskini miongoni mwa jamii. "Kufanya kazi kwenye NGO ni kutumikia umma; ni lazima tujitoe na kuweka rehani maisha yetu kwa ajili ya Taifa" Alisema.
Akizungumzia suala la mchakato wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Makundi amesema suala la Katiba ni la watanzania wote bila kujali kiwango chao cha Elimu, taaluma, umri, hali ya kifedha na hata kiafya; hivyo mjadala wa katiba uwe huru na kila mtu apate nafasi ya kutoa maoni yake bila kuwepo kwa kipingamizi.
Asasi ya MED imekuwa ikiendesha mijadala, mikutano ya majadiliano, kuanzisha Club za Marafiki wa Elimu katika shule za Msingi na sekondari ambazo zimekuwa zikijadili masuala mbalimbali yanayo wakabili wanafunzi katika shule zao.
Shughuli za Marafiki wa Elimu Dodoma zimeongeza chachu ya harakati katika maeneo mengi ya mji wa Dodoma hasa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambao hivi sasa wanaendesha club zao kutetea haki za wanafunzi, maendeleo ya shule, masuala ya demokrasia, utawala bora na maendeleo ya jamii katika maeneo yao.
Kazi ya kufuatiliaa taarifa za Changamoto za Elimu kwa Wanafunzi wa shle ya Kata ya Mbabala Sekondari Manispaa ya Dodoma.
Katika Bunge hili la Tano; Mswada wa kujadili kuanzishwa kwa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utajadiliwa. Usikose kuwasilisha mawazo yako; KATIBU SANA.
BIASHARA UTOTONI NA ELIMU
Mtoto Samson Hezron (11) mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya Msingi Ngh'ongh'onha katika Manispaa ya Dodoma ni miongoni mwa wanafunzi wa shule za msingi wanao juihusisha na biashara wakiwa na lengo la kusaidia kuinua kipato cha familia zao.
Samson akionge na MED alisema kuwa anafanya biashara ya miwa ili kuongeza kipato kwenye familia na kuweza kupata fedha za kukidhi mahitaji yake muhimu yakiwemo ya sare na madaftari ya shule.
"Baba na mama yangu hawana kazi japo baba amesoma hadi darasa la saba; nikipata fedha nampa mama kwa ajili ya chakula na nyingine naweka kwa ajili ya mahitaji ya shule"
Samson anadai kuwa hufanya biashara kwa kufuata ratiba ya nyumbani kuwa ni lazima awe nyumbani kabla ya saa kumi na moja jioni wakati hufanya biashara kwa siku za jumamosi, jumapili, siku za mapumziko na likizo.
Kijana huyu anaongeza kuwa pamoja na kufanya biashara katika umri mdogo ratiba yake ya masomo anaiheshimu na kujikuta akipata si chini ya alama 70 kwa somo la Hisabati, 80 kwa sayansi na 30 kwa somo la kiingereza. "Kiingereza ni kigumu sana kwangu; hata hivyo mwalimu wa kiingereza na sayansi Mwl. Luganissa nampenda sana kwani anaelekeza vizuri bila viboko"
Kijana Samson akiwa na miwa yake tayari kuelekea mitaani kutafuta waeja wa miwa.
Mtoto Samson nadai kuwa mtaji wake wa miwa ni kiasi cha sh 2000 ambazo humpatia faida ya kati ya sh 2000 hadi 2500 kwa siku. Kuhusu kupata muda wa kujisomea "Sam" anasema hasomi tuition kwani kaka yake anayesoma darasa la saba ana mfundisha kila siku kuanzia saa 12 jioni nyumbani kwao.
Kijana Samsoni ni mmoja kati ya watoto wanaofanya biashara mbalimbali mkoani Dodoma kwa lengo la kukabiliana na hali ngumu ya maisha katika gfamilia zao. Wengi wa vijana wenye umri sawa na wa Samson hujihusisha na kuomba-omba mitaani, biashara ya vyuma chakavu na kuokota chupa za plastiki na kuziuza kwa wafanya biashara wa chupa hizo.
KIKUYU YAUNDA KAMATI YA KURATIBU SHUGHULI ZA CLUB ZA MARAFIKI
Marafiki wa Elimu katika shule ya Sekondatri Kikuyu wameamua kuunda kamati ya shule kwa ajili ya kuratibu shughuli za Marafiki ili kuongeza ufanisi na uendelevu wa harakati za Marafiki katika shule hiyo. |
Uamuzi wa wanaharakati hao kuwa na Kamati hii ni kuhakikisha kuwa Marafiki wa shule hiyo wanafanya kazi yao kwa umakini zaidi na kuongeza tija katika mijadala na uhuru wa kutoa maoni na kuchangia mada mbalimbali za Club za Marafiki katika shule hiyo.
Shule ya Kikuyu ina jumla ya Club 9 za Marafiki ambazo zinahusisha mikondo 9 ya kidato cha kwanza hadi cha tatu. “Kuundwa kwa Kamati hii kutasaidia kuimarisha uhuru wa mijadala na kuzifanya Club zidumu kwani zitasimamiwa na wanafunzi wenyewe”. Club za Marafiki wa Elimu Kikuyu zinajiendeshwa kwa kusimamiwa na Kamati ya Marafiki wa Elimu Dodoma kwa kushirikiana na Mwalimu Mlezi wa Club hizo.
Timu ya Marafiki wa Elimu katika shule ya Sekondari Kikuyu Mkoani Dodoma imeonesha mabadiliko makubwa katika kutetea walimu kwa kutoa wito kwa wadau mbalimbali kuwatetea walimu ili kupata stahiki zao na kuboresha ari ya walimu kufanya kazi zao pasipo kinyongo.
Wanaharakati hao wameeleza kuwa kuendelea kushuka kwa kiwango cha ufaulu katika shule za sekondari hasa za kata ni matokeo ya kupuuzwa kwa ushauri wa walimu au walimu kusahaulika. Vijana hao wamewataka wadau hasa taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali kusaidia kupaza sauti juu ya kilio cha walimu ili kuwaongezea ari katika kutekeleza majukumu yao.
MARAFIKI WAJADILI NAMNA YA KUBORESHA MMES II- MOROGORO
Wawakilishi wa harakati za Marafiki wa Elimu kutoka kanda tatu za Mashariki, Kusini na Nyanda za juu Kusini; walikutana mjini Morogoro kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu mustakabali wa Elimu na namna nzuri ya kuboresha ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Elimu.
Aidha washiriki hao waliipongeza Serikali kwa juhudi zake za kuboresha kiwango cha Elimu kupitia mipango yake ya maendeleo ya Elimu kama MMEM I&II, MMES I&II na Mafunzo ya Ualimu Kazini (TDMS).
Wanaharakati hao walitambua mafanikio ya mipango hiyo kuwa ni pamoja na kufanikiwa kujenga shule nyingi za msingi na sekondari, ongezeko kubwa la uandikishaji wa watoto katika shule zetu, ongezeko la juhudi za kupeleka pesa shuleni kwa lengo la kuboresha hali ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika shule nyingi hapa nchini. Moja ya Maktaba katika Shule ya Sekondari zilizoko Mkoani Dodoma.
Ushauri ulitolewa na wanaharakati hao kwa serikali kwamba; katika kutekeleza MMES II uliozinduliwa Januari 2011; ambao unalenga kuboresha kiwango cha elimu ya sekondari, uandikishaji wa wanafunzi, mfumo wa uongozi na mfumo wa ukaguzi; ni budi serikali iyafanyie kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mipango iliyopita.
Walitaja mapungufu yaliyojitokeza katika mipango iliyopita kuwa ni pamoja na udahili wa wanafunzi shuleni ambapo wanafunzi wenye hata chini ya alama 150 walichaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari, watendaji wa mipango hiyo hasa wakuu wa shule, bodi na kamati za shule kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusiana na mipango na kwa kiasi kikubwa wananchi ambao ndio wadau wakuu hawakuelimishwa wala kushirikishwa kama mpango unavyoeleza.Wanafunzi wa darasa la Saba wanaojiandaa kuingia kidato cha kwanza 2012.
Marafki wa Elimu kwa kauli moja waliazimia kuishauri serikali kutekeleza mambo 6 ambayo wanaamini kuwa kama yatafanyiwa kazi ipasavyo; mafanikio chanya yatapatikana katika maendeleo ya elimu haa nchini. Maazimio hayo ni pamoja na:-
- Serikali ihakikishe kuwa inapeleka fedha za ruzuku mashuleni kwa kiwango cha mpango kwa wakati.
- Serikali ihakikishe kuwa wadau wote muhimu katika kutekeleza mpangio wanakuwa na uelewa wa kutosha kwa kuelimishwa kuhusu wajibu wao, haki zao na kushirikishwa kikamilifu katika kila hatua yautekelezaji.
- Serikali ihakikishe kuwa inaimarisha ukaguzi wa ndani na wa nje katika shule na pia ukaguzi huo ufanyike mara kwa mara ili kudhibiti na kubaini ubadhirifu wa rasilimali za shule.
- Serikali izingatie viwango vya ufaulu vilivyotamkwa kwenye serra ya Elimu katika kuchagua watoto wa kujiunga na elimu ya sekondari na kuhakikisha kuwa taarifa za maendeleo ya wanafunzi pamoja na matokeo halisi ya mwisho yanakuwa ndio kigezo cha kumchagua mwanafunzi kujiunga na sekondari.
- Serikali ihakikishe kuwa inaongeza idadi ya walimu mashuleni na kuwapatia walimu mafunzo kazini mara kwa mara na kuboresha mazingira ya walimu hasa wanaofanya kazi maeneo ya vijijini.
- Serikali ihakikishe kuwa uteuzi wa wasimamizi wa shule unazingatia vigezo vya uteuzi kama miongozo inavyoelekeza; wakuu wa shule wapewe semina za mara kwa mara kwa ajili ya kuboresha utekelezaji wa majukumu yao na kuhakikisha kuwa Bodi na Kamati za shule zinajengewa uwezo wa mara kwa mara ili kuboresha usimamizi wa majukumu yao.
Tamko hili la wanaharakati halina budi kuungwa mkono na wadau wote wapenda maendeleo ya Elimu nchini hasa kwa kuzingatia ushindani wa ubora wa Elimu tunaokabiliana nao hasa katika Muungano wetu wa Jumuia ya Shirikisho la Afrika Mashariki.
SHULE TUNAZO; VITENDEAKAZI JE?
Wakati serikali yetu ikijinadi kuwa imepata mafanikio makubwa katika kuwezesha watoto wengi kujiunga na elimu ya msingi hapa nchini; bado kuna umuhimu mkubwa wa serikali kutafakari kwa kina kile watoto hawa wanachokipata katika shuleni hizo.
Ni ukweli usiopingika kwamba shule zetu za msingi zimepata wanafunzi wengi ambao kwa hakika wamejiunga na shule za msingi kwa ajili ya kupata elimu hii muhimu kwa maisha yao ya kila siku. Kwa hili tunapaswa kuipongeza serikali kwani wapo vijana wengi ambao kwa juhudi za serikali hasa kuiptia mpango wa MMEM wangeikosa fursa hii.
Pamoja na pongezi hizi; yapo mambo ambayo tunapaswa kuyatazama kwa mapana zaidi hasa katika suala zima la upatikanaji wa vitendea kazi kama vitabu vya kiada na ziada, walimu wa kutosha kwa masomo yote, madawati, vyumba vya madarasa, matundiu ya vyoo, mazingira safi nya kujifunzia na kufundishia na viwanja vya michezo kwa watoto wetu.
Ukosefu wa mahitaji muhimu au vitendea kazi hivyo na kutokuwepo kwa juhudi za dhati za kutatua tatizo hilo ni sawa na kuididimiza elimu na kuwapotezea muda vijana hawa ambao kila kukicha wanaitafuta elimu na kujikuta ndoto zao zikiishia hewani.
Kwa kitabu kama hiki anachokisoma kijana huyu aliyefahamika kwa jina moja la Issa mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Pahi Wilayani Kondoa; ni ushahidi tosha kuwa bado kijana huyu na wengine wengi wana safari ndefu ya kutimiza ndoto zao za kupata Elimu bora na yenye manufaa kwa maisha ya baadaye.
Wadau wote wa Elimu nchini; hatuna budi kumpongeza kijana huyu kwani licha ya kitabu hiki kubaki kipande baada ya kuliwa na wadudu ambao haijafahamika kama ni jamii ya mchwa au panya; bado ameendelea kuhitaji japo masalio ya kile kilichoandikwa kwenye kitabu hiki. Hongera sana Issa!
WILAYA YA KONDOA NA VITUKO KATIKA ELIMU
Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa iliyoko umbali wa kilometa 160 kutoka Dodoma inakabiliwa na hali mbaya ya maendeleo ya Elimu kufuatia shule zake za Sekondari kudorora katika matokeo ya mitihani ya kitaifa ukiwemo wa kidato cha nne uliofanyika mwishoni mwa 2010. Kibao hiki kinaelekeza lugha rasmi ya kutumia kwenye shule ya Sekondari Changaa.
Kufuatia matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yaliyo tangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa mwanzoni mwa mwaka 2011; shule tano kati ya kumi zilizofanya vibaya kitaifa zilitoka katika Wilaya ya Kondoa ambazo ni Changaa, Kolo, Hurui, Kikore na Thawi.
Hii ni hali halisi ilivyo katika chumba cha darasa kinachotumika kama ofisi ya walimu.
Timu ya wanaharakati wa Elimu kutoka Asasi aya Marafiki wa Elimu Dodoma MED ilifanya ziara katika shule ya Changaa ambapo ilifanikiwa kufika kwa tabu kutokana na muiundombinu mibaya hasa ya barabara za kufika katika shule hiyo ambayo pia haina hata kibao cha kuelekeza jinsi ya kuifikia shule hiyo.
Ziara ya Marafiki wa Elimu Dodoma ilibaini vituko vya aina yake katika shule hiyo yenye wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne na kuwaacha hoi kwa mshangao baada ya kubaini kuwa shule ya Changaa ina wanafunzi watatu (3) tu wa kidato cha nne kwa mwaka 2011 ambapo kati yao wasichana ni wawili na mvulana mmoja tu. Kurwa Martin mwafunzi pekee wa kidato cha nne kati ya watatu aliye hudhuria masomo wakati wa zira ya Marafiki wa Elimu katika shule ya Sekondari Changaa.
Sababu za uwepo wa wanafunzi watatu wa kidato hicho ilielezwa ni kutokana na wengi wao kukata tamaa ya matokeo mabaya na pia umbali wa kutoka shuleni na makazi ya wenyeji.
Wanafunzi wa shule hii tangu wajiunge na Elimu ya Sekondari hawajawahi kujifunza masomo ya Sayansi na Hisabati kutokana na kukosekana kwa mwalimu wa masomo hayo japo Mkuu wa shule hiyo ni walimu wa masomo hayo. Hii ni picha ya Maabara ya shule ya Sekondari Changaa iliyoko Wilayani Kondoa.
Imeelezwa kuwa 2009 shule hiyo ilikuwa na mwalimu mmoja; 2010 walimu wawili na 2011 shule ina walimu watatu wa kuajiriwa na mmoja wa kujitolea na kulipwa posho na jamii.
Wanafunzi wa Changaa wanatembea kwa zaidi ya kilomita sita kwa siku kwenda na kurudi shuleni kutokana na shule hiyo kuwa mbali na makazi ya watu jambo ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa wengi wa wanafunzi hao kukosa hamu ya kuendelea na masomo.Wanafunzi wa Changaa Sekondari wakizitafuta Km3 za kurejea nyumbani.