Log in
Marafiki wa Elimu Dodoma (MED)

Marafiki wa Elimu Dodoma (MED)

Dodoma, Tanzania

Parts of this page are in Swahili. Edit translations

Kwa Usafiri huu kweli!

Hii ni hali halisi katika Wilaya ya Kondoa ambako matumizi ya matrekta madogo (Power tiller) sasa yanatumika kubeba abiria na mizigo badala ya kufanya kazi za kilimo. Haishangazi wala kusikitisha kwani kulingana na hali halisi ya maisha; huu ni ubunifu.

 

Watoto wa Sikuhizi!! 

Kwa kuzingatia mabadiliko ya kiuchumi na taaluma; tunakipimaje kizazi hiki cha Sayansi na Teknolojia?

Miaka kadhaa iliyopita tuliwasikia watoto na vijana wengi wakishirki kwenye michezo kadhaa ikiwemo ile ya kombolela, sambi, kuruka kamba, kubembea na mingine mingi.

Hivi sasa ni nadra sana kwa watoto wa marika ya miaka 5-16 kuwasikia wakijihusisha na michezo hiyo kutokana na teknolojia.

Swali muhimu la kujiuliza hapa ni je! mabadiliko haya yanatupeleka kwenye tamaduni gani? Kama watoto wataisaha michezo hiyo iliyo tukuza na kujikuta kuwa na maadili mema kwa jamii ikitoweka; tutavuna nini kwenye tamaduni za kimagharibi?

Watafute watoto wa siku hizi na uwaulize swali dogo tu juu ya michezo wanayoipenda kwa sasa! Majibu utakayo kutana nayo ni pamoja na Kucheza gemu kwenye kompyuta, kuangalia TV nk.

Wito wangu ni kwamba; tunapofurahia mabadiliko ya taknolojia; tukumbuke tulikotoka ili tusije kuwa watumwa wa teknolojia.

 

Dodoma Kavu; Inalimika, Inafugika.

Pamoja na Mkoa wa Dodoma kusifika kwa ukame; Mkoa huu ulio katikati ya Nchi ya Tanzania wakazi walio wengi wanaishi kw kutegemea kilimo na ufugaji.

Ni dhahiri kwamba Mkoa huu ni wa wafugaji na wakulima. Ila ninachokizungumzia hapa ni maisha ya wakazi wake waishio mjini hasa katikati ya mji ndani ya Manispaa ya Dodoma.

Ukiwa katika Manispaa ya Dodoma si jambo la ajabu kukutana na watumishi wa nyumbani hsa wanaume wakiwa na matoroli yakiwa na majani ya mifugo hasa ng'ombe licha ya kuwa mbuzi, kondoo, nguruwe na kuku wanafugwa kwa wingi.


Mkazi wa Mtaa wa Chidachi aliyefahamika kwa jina moja la Daniel akisukuma toroli lenye majani ya ng'ombe kama alivyokutwa na mpiga picha wetu.

Kilimo:    

Shuhuli za Kilimo katika Mkoa huu zinaendeshwa katika Wilaya zake zote hasa ikizingatiwa kuwa ardhi ya Dodoma inasifika kwa kuwa na mbolea inayojitosheleza kwa mazao ya aina mbalimbali ya nafaka ikiwemo mahindi, ufuta, alizeti, mtama, uwele, mbaazi, karanga nk.

Kama ilivyo kwa ufugaji, ndani ya Manispaa ya Dodoma wakazi wake wamekuwa wakijihusisha na kilimo cha mazao mbalimbali katika maeneo ya viwanja vilivyo wazi ambavyo wamiliki wake bado hawajaanza kuvijenga nk.

        

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

                           Kilimo cha Mahindi katika Kata ya Mkonze Manspaa ya Dodoma  Mkonze.

Lucas Mkasanga Miaka 14; Darasa la Tatu!

Kijana Lucas Mkasanga (14) ni mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Mwenge iliyoko katika Kata ya Mbabala Manispaa ya Dodoma.

Lukas anasikitishwa na kuchelewa kwake kujiunga na elimu ya msingi kutokana na kile alichodai ni kutengana kwa wazazi wake hali iliyo mfanya akaishi na bibi yake mzaa baba Wilayani Kondoa kwa kipindi kirefu.

Kwa mujibu wa maelezo ya Lucas; baba yake ni mpishi wa shule ya Sekondari Bihawana iliyoko katika kata hiyo ya Mbabala.

Aliongeza kuwa sasa anaishi na mama yake wa kambo ambaye anamshukuru kwa kumpeleka shule ili afikie malengo yake ya kuja kuwa Mwalimu hapo baadae.

 

Lucas anaeleza changamoto zilizopo shuleni kwake kuwa ni pamoja na uhaba wa vitabu ambapo hivi sasa kitabu kimoja kinatumiwa na wanafunzi wanne hadi sita.

Kuhusu adhabu shuleni anasema kwamba hilo ni jambo la kawaida kwa wanaofanya makosa shuleni japo amewatetea walimu wake kuwa si wachapaji sana.

Lucas alihitimisha mahojiano yake kwa kuiomba Serikali iangalie namna ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia hasa kwa kuongeza vifaa muhimu mashuleni kama vile vitabu, vifaa vya michezo na kusikiliza matatizo ya walimu ili wawe na moyo wa kuwafundisha kwa bidii.

Kijana huyu anaelezea mafanikio yake kitaaluma kuwa ni mazuri darasani ambapo anashika nafasi ya kwanza kati ya wanafunzi 94 wa darasa lake.

Wakati huo huo kamera yetu ilimnasa kijana mmoja ambaye jina lake halikufahamika mara moja akiwa na lundo la madaftari ya wanafunzi wenzake akiyapeleka nyumbani kwa mwalimu kwa ajili ya kusahihisha kazi za wanafunzi.

Kwa mujibu wa maelezo ya baadhi ya wanajamii walieleza kuwa kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi na uhaba wa walimu katika shule hiyo; walimu wana lazimika kufundisha vipindi mfululizo na baadaye kwenda kusahihisha kazi hizo wakiwa nyumbani.

Jambo la kujiuliza hapa ni je! kwa hali hii ya mwalimu kujikuta wakifanya kazi za shule muda wote yani nyumbani na shuleni; jamii. serikali na wadau wengine tunafanya nini ili kuwawezesha walimu kumudu maisha yao ya kila siku?

 Maria (11) na Video za Usiku.

Maria Yohana (11) ni mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya Msingi Mwenge iliyoko katika Kijiji cha Mbabala A Manispaa ya Dodoma.

Maria ni miongoni mwa watoto ambao hawanabudi kuokolewa kutoka katika hatari ya kukumbwa na balaa la mmomonyoko wa maadili kutokana na yeye mwenyewe kukiri kujihusisha na utazamaji wa video hasa nyakati za usiku.

Ilikuwa majira ya saa kumi na mbili na nusu (12:30) za jioni nilipo kutana na mtoto huyu kwenye eneo la vilabu maarufu kama Makondeko; maria alikuwa akisubiri picha iliyoanza saa 8 mchana iishe ili aingie picha ya pili inayoanza saa moja hadi saa mbili na nusu usiku.

Kwa maelezo ya Maria; kiingilio katika nyumba hiyo ya video ni sh. 100 kwa watoto. Hata hivyo yeye anamudu kulipa kiingilio kwa kuomba kwa wazazi wake au vijana (majirani zake) anao wafahamu.

Kwa Maria ambaye ni mtoto bado; hajatambua fika hatari iliyo mbele yake; lakini  kwa wazazi na jamii inayomtazama Maria akiingia na kutoka katika chumba hiki cha video katikati ya kilabu cha pombe kuna jambo nadhani wanaliona kwa Maria.

Kuhusu muda wa kurudi nyumbani Maria anaeleza kuwa kuna wakati anarudi na majirani zake na wakati mwingine hurudi peke yake au akiwa na mdogo wake kama wanavyo onekana pichani.

Baadhi ya wazazi walioongea na mwandishi wetu alieleza masikitiko yake juu ya serikali ya kijiji cha Mbabala kulifumbia macho suala la wengi wa watoto wa kijiji hicho kuangalia video katika nyumba hiyo iliyoko katika eneo la kilabu.

"Kuna wakati mwingine huyu mtu anaonyesha picha mbaya za X hadi usiku na watoto wa shule za Sekondari na hawa wadogo wote wanaangalia" alisema mmoja wa wakazi wa eneo hilo.

Eneo la Makondeko ni eneo pekee lenye mkusanyiko mkubwa wa watu na shughuli mbalimbali zikiwemo za kibiashara katika Kijiji cha Mbabala A.