Hakuna Maisha Bora Bali Bora Maisha.
Familia moja katika Kata ya Kikuyu Kusini Manispaa ya Dodoma itaubaliana na kauli yangu kwa Bora Maisha kwa Kila Mtanzania na ukweli si Maisha Bora kwa kila Mtanzania kama ambavyo kauli hiyo imekuwa ikiimbwa kila kukicha na viongozi wetu wa Serikali na hata wa hama Tawala CCM.
Kwa zaidi ya mwezi mmoja na nusu sasa moja kati ya nyumba zilizoathiriwa na mvua zilizonyesha mjini Dodoma tangu mwishoni mwa mwezi Januari haijafanyiwa ukarabati licha yafamilia hiyo kuendelea kuitumia nyumba hiyo huku kila siku wakizidisha sala na kujikabidhi mikononi mwa muumba kwa lolote linaloweza kutokea.
Unadhani familia hii itachagua lipi kati ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania na Bora Maisha kwa Kila Mtanzania? Ni wazi kwamba jibu la familia hii unalo. Tuachane na nyumba ya mpiga kura huyu na kuangalia suala la usafi wa mazingira na hasa suala la choo; KARIBU!
Hiki ndicho choo kinacho tumiwa na familia hii; hiki ni kipindi cha mvua ambacho kwa kawaida kipindupindu nacho hushika hatamu. Bado najiuliza juu ya Familia hii; inaihesabu na kuikubali SERIKALI NA KAULI ZAKE? Majibu na ushauri wako ni muimu sana!
Wanaharakati Wajadili Mchakato wa Katiba Mpya.
Mchakato wa kuandika katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unazidi kushika kasi zaidi nchini baada ya wanaharakati wa mikoa saba kukutana Dodoma kujadili na kujifunza juu ya katiba ya sasa na mapungufu yake na jinsi ya kuelimisha wananchi umuhimu wa kuwa na katiba mpya.
Warsha hiyo ya sikun tatu inafanyika katika Hoteli ya Dodoma inahudhuriwa na wawakilishi wa Mitandao ya Asasi za Kiraia kutoka katika Mikoa ya Morogoro, Lindi, Rukwa, Ruvuma, Iringa, Mbeya Dodoma na Tabora.
Washiriki wa warsha hiyo wameeleza nia yao ya kuhakikisha kuwa watadumu katika kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanziba na kuahidi kuwa watajitahidi kuhakikisha katika mchakato huo watajitahidi kuziondoa kasoro zinazoonekana kuwa zinayumbisha Mungano huo.
Wakichangia mada katika warsha hiyo inayoonekana kuwavuta wanaharakati ha ambao ni waumini wa Asasi za kiraia nchini wamesema kuwa kazi ya kuelimisha jamii juu ya uwepo wa Katiba Mpya ni ya muhimu inayohitaji kujituma na kuwa na moyo wa kujitolea kuisaidia jamii ili ielimke na kuwa na maamuzi yaliyo sahihi na yenye manufaa kwa Taifa.
Naye Mkufunzi wa warsha hiyo Bw. Deus Kibamba (picha ndogo)kutoka Jukwaa la Katiba amesema watanzania watashiriki kwa mara ya kwanza kutunga katiba yao kwani katiba iliyopo kwa sasa hakutungwa na watanzania bali watanzania waliletewa katiba hiyo iliyotungwa na waingereza.
Washiriki wa warsha hiyo wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kukata kiu ya watanzania katika kudai katiba mpya.
Wadau hao walisema kuwa kauli ya Rais aliyoitoa kwenye maadhimisho ya sherehe za kutimiza miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM mkoani Dodoma tarehe 5 Februari, 2011 ilimaliza utata uliokuwepo kutokana na kauli tata za baadhi ya watendaji wake kama Mwanacsheria Muu wa Serikali na Waziri wa Sheria na Katiba.
Warsha hiyo inayoendeshwa kwa mtindo shirikishi kwalengo la kuwafanya washiriki wote wajisikie kuwa sehemu ya mchakato huo; imekuwa ya mafanikio makubwa hasa kutokana na wengi wa washiriki kuonekana kuwa makini na wasikivu katika kila hatua.
Tanzania, Tanzania; nakupenda kwa moyo wote.... Wanaharakati waliimba wimbo huo kuonyesha mshikamano wao kwa Tanzania na nia yao njema ya kudumisha Muungano huo ambao wamesema ni wa kipekee duniani hivyo hauna budi kuendelea kuwepo ili kuiweka Tanzania katika historia hiyo.
Kwani Viongozi wetu Hawaoni?
Wananchi wa Kata ya Hazina iliko shule ya Msingi wanajiuliza swali mkwamba "Kwani viongozi wetu hawaoni?" wakazi hawa wamefikia hatua hiyo mara baada ya kutosikia hatua zozote zilizochukuliwa na ama viongozi wa Mkoa, Wilaya, au Tarafa kuhusiana na vyumba viwili vya madarasa vilivyojengwa katika shule hiyo kuharibika vibaya kutokana na kujengwa chini ya kiwango.
Jengo hili lililojengwa kwa fedha za MMEM II; halifaimkwa shughuli zozote kutokana na kuwa a nyufa zinazotihia kila aina ya kiumbe hai kinachothamini uhai wake.
Hapa ndipo tunapojiuliza kama kweli rasilimali za umma zinatumika ipasavyo au la; jamii nayo inapaswa kuwajibika katika kusimamia vyema rasilimali za umma badala ya kuiachia serikali ambayo kazi hizi mbovu zinapofanyika viongozi wanakuwa hawahusiki.
Kero ya Maji Kikuyu Hadi lini?
Wakazi wa kata ya Kikuyu Kusini Manispaa ya Dodoma hawajui hatima yao dhidi ya kero ya maji wanayo endelea kuipata kwa miongo kadhaa hadi sasa. wakazi hao wamekuwa wakitumia maji ya visma vifupi yasiyo safi wala salama kwa kipindi kirefu imeelezwa.
Kama picha inavyoonesha hapo juu; wakazi hawa wamedai kuwa wameishi katika kata ya Kikuyu kwa zaidi ya miaka ishirini na matumaini pekee waliyo nayo kuhusiana na maji ni visima vifupi wanavyo vitumia katika eneo hilo lenye wakazi wa kipato cha kati.
Licha ya kukubali kupigwa picha na kukataa kutaja majinayao; wakazi hao wameeleza kuwa wamedumu kwenye eneo hilo tangu enzi za diwani mkongwe wa eneo hilo Al-maarufu Mkungugu Marehemu Mloge aliyedumu kwenye udiwani wa eneo hilo kwa awamu nne; Meya mstaafu wa Manispaa ya Dodoma na Diwani wa eneo hilo Mh Francis Mazanda na baadaye Kata hiyo ilimpata Diwani ambaye walimtaja kwa jina la Baba Jofu ambaye alichaguliwa katika uchaguzi wa 2010 lakini alifariki dunia kabla ya kuapishwa.
Wakazi hao wamedai kuwa eneo hilo limesahaulika kwa kipindi kirefu kwa huduma hiyo muhimu licha ya ahadi kede-kede zinazotolewa na viongozi mbalimbali wa kisiasa na serikali kila wakati kuwa watatatua kero hiyo.
Wakazi hao wameeleza kuwa maji hayo yanayo patikana kwenye visima vifupi vilivyopo kando ya barbara ya Iringa hatua chache kutoka stendi ya daladala za Kikuyu si safi wala salama kwa matumizi ya binadamu.
Eneo la Kikuyu ni miongoni mwa maeneo yenye uhaba mkubwa wa huduma ya maji safi na salama jambo ambalo linasababisha usumbufu mkubwa kwa wakazi wa eneo hilo kwa kulazimika kutumia muda mrefu kutafuta maji.
Wazazi waaswa na Tuisheni za wanavyuo.
Wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika shule ya Sekondari ya Kikuyu Manispaa ya Dodoma wameaswa kujihadhari na Tuisheni zinazoendeshwa na wanavyo kwani zina madhara makubwa kuliko faida.
Rai hiyo ilitolewa kwenye mkutano wa wazazi wa wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne wanaosoma katoka shule hiyo kufuatia malalamiko kuwa wengi wa wanafunzi wa shule hiyo wanajihusisha na masuala ya ngono na wanachuo wa St. Johns.
Wazazi na walimu wa shule ya sekondari ya Kikuyu walieleza masikitiko yao mbele ya Mwenyekiti wa Kamati ya maendeleo ya Kata ya Kikuyu Kaskazini Mh. Meja Risasi kuwa, baadhi ya wanafunzi wa kike katika shule hiyo wamekuwa wakisingizia kufundishwa na wanachuo hao lakini matokeo yake wanaishia kufanya nao ngono badala ya masomo.
Wazazi hao wameombwa kuhakikisha kuwa wanawalinda watoto wao dhidi ya mtego wa wanachuo kwa kuhakikisha kuwa wanawazuia kwenda kwenye tuisheni hizo bandia.
Ili kupunguza tatizo hilo; Mkuu wa shule ya Kikuyu Sekondari Bi. Mkoyi aliwaeleza wazai kuwa shule hiyo imeazimia kuwa wanafunzi wa kidato cha pili na tatu watafanya marudio ya masomo kila siku za masomo bila malipo hivyo wazazi wahakikishe kuwa wanawawezesha watoto wao angalau kwa fedha ya kujinunulia soda mchana ili wasirudi nyumbani mara baada ya masomo ya kawaida.
Wazazi waliupongeza walimu na uongozi wa shule hiyo ambayo katika matokeo ya kidato cha nne 2010 zaidi ya wanafuzi 40 walifaulu katika daraja la kwanza hadi la tatu.
MED Yaomba Wastaafu Kufundisha kwa Mikataba.
Asasi ya Marafiki wa Elimu Dodoma MED imemwomba Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ushari ya Wilaya (DCC) Bw. John Tuppa; kuishauri kamati yake ili iwatumie walimu wastaafu kufundisha shule za sekondari za kata.
Barua ya MED yenye maombi hayo iliwasilishwa kwa Mkuu wa Wilaya kwa lengo la kusaidia kupunguza tatizo la uhaba wa walimu katika shule za kata katika Wilaya ya Dodoma.
Kwa mujibu wa barua hiyo; MED imemuomba Bw. Tuppa kuwatumia walimu wastaafu kufundisha katika shule za kata ambazo wastaafu hao wanaishi badala ya kuendelea kuwasubiri vijana wadogo wanaohitimu masomo na kwenda kufundisha kwenye shule hizo bila kuzaa matunda tarajiwa.
Barua hiyo ilieleza kuwa; licha ya nia ya serikali kuwatumia wahitimu wa kidato cha sita kuziba pengom la walimu; wahitimu hao wamekuwa wakituhumiwa kuwa sehemu ya chanzo cha ongezeko la mimba kwa wanafunzi wa shuleni wanazo fundisha.
Baadhi ya wadau wameipongeza MED kwa hatua hiyo ya uthubutu waliyo ichukua kwa Mkuu wa Wilaya na kuongeza kuwa; wastaafu wengi wenye taaluma ya ualimu wana maadili ya kazi hiyo hivyo wanaweza kusaidia sana kupunguza tatizo la uhaba wa walimu kwenye shule za kata kama wastaafu hao watatumika ipasavyo na kupewa stahili zao.
Mratibu wa MED Bw. Davis Makundi amekiri kumwandikia Mkuu wa Wilaya barua hiyo na kusema; hiyo ni haki ya msingi kwa mtu binafsi, taasisi au kikundi chochote cha kijamii kwani barua hiyo ni ya kumshauri na si ya amri kwa kiongozi huyo wa Wilaya.
Wenye Ulemavu Waomba Msaada wa Vifaa.
Watu wenye changamoto za ulemavu wamewaomba wanasiasa kuwasaidia kupata nyenzo mbalimbali kwa ajili ya shughuli zao za kila siku.
Wakiongea kwa nyakati tofauti na MED wanachama wa Chama Cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) tawi la Dodoma wamesema; wanasiasa wana nafasi nzuri ya kutetea haki za walemavu kama kweli wakidhamiria kufanya hivyo.
Mwenyekiti wa CHAVITA tawi la Kondoa Bw. Mustafa Shabani amesema watu wenye ulemavu wana changamoto ningi za kimaendeleo zinazo sababishwa na ulemavu wao. Alisema kwamba wao kama watu wengne wanahitaji kupata taarifalakini hawazipati kwa usahihi kutokana na wao kukosa vifaa maalum vya kuongeza usikivu au wakalimani.
Naye Bw. Ally Jumanne ambaye ni katibu wa chama hicho alisema ni vema wanasiasa wakasaida kuishawishi serikali ijali haki na mahitaji ya wenye changamoto za ulemavu ili nao wanufaike na rasilimali za taifa kama wananchi wengine wasio na ulemavu.
Wadau hao wamesema kuwa vifaa vya kusaidia wenye ulemavu kama vile vifaa vya kusaidia kuongeza usikivu, kuona, fimbo maalum za wasioona na baiskeli za miguu mitatu pamoja na vifaa vingini ni ghali kiasi kwamba mtu mwenye ulemavu si rahisi kuvipata.
Walishauri serikali iwasaidie kupata wakalimani kwa ajili ya kutafsiri habari na matukio mbalimbali kupitia Televisheni na kuwasaidia wasioona kupata CD na tepu za sauti ambazo zitawasaidia kuwafikishia habari na taarifa mbalimbali kwa wakati.
MED Hewani Kuanzia Mach 2011.
Asasi ya Marafiki wa Elimu Dodoma (MED) inatarjia kuanza kuendesha vipindi vyake vya Radio kuhusu Elimu kuanzia mwezi Machi, 2011. Wanachama wa MED na wadau wote wa Elimu wanakaribishwa kushiriki kwenye vipindi hivyo.
Hayo yameelezwa na Mratibu wa MED Bw. Davis Makundi alipkuwa akiongea na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake. Bw. Makundi amesema vipindi hivyo vitaendeshwa kwa udhamini wa mashirikaya HakiElimu na Uwezo.net yote ya jijini Dar Es salaam
"Vipindi hivi vitakuwa vya moja kwa moja kutoka studio (Live) na vitaruhusu wasikilizaji walio nje ya studio kupifa simu au kutuma SMS kwa lengo la kuchangia mada au kuuliza maswali alisema" Bw. Makundi.
Vipindi hivyo vitakavyosikika kwa muda wa nusu saa (dk. 30); vitakuwa vikisika kwenye Radio Kifimbo 89.8 inayorusha matangazo yake kwenye masafa ya FM Mkoani Dodoma. Bw. Davis Makundi