Log in
Wanaharakati wa Elimu Mazingira na Afya (WEMA)

Wanaharakati wa Elimu Mazingira na Afya (WEMA)

Mkalapa, Ndanda-Masasi, Tanzania

Parts of this page are in Swahili. Edit translations

KAZI NA SHUGHULI ZINAZOSHUGHULIKIWA NA KIKUNDI CHA "WANAHARAKATI WA ELIMU, MAZINGIRA NA AFYA" (WEMA)

1. Kikundi cha WEMA kinaendesha Maktaba ya Jamii ambayo ipo katika kijiji cha Mkalapa kilichopo wilaya ya Masasi. Maktaba ya WEMA ina vitabu vinavyokidhi mahitaji ya watu wa viwango mbalimbali vya kitaaluma kuanzia elimu ya watu wazima, elimu ya Awali, elimu ya Msingi, Sekondari, hadi chuo kikuu. Sababu kubwa iliyokichochea kikundi cha WEMA hadi kufanya maamuzi ya kuanzisha maktaba ya jamii ni hali halisi ya uhaba wa vitabu katika shule nyingi za Awali, Msingi, na Sekondari katika wilaya ya Masasi.

Kikundi cha WEMA kinadhani kwa kuanzisha maktaba hiyo ya jamii katika kata ya Mwena, kutawasaidia wanafunzi wanaosoma katika shule mbalimbali zilizo jirani na maktaba hiyo kupata fursa ya kuitumia maktaba kwa lengo la kuinua kiwango chao cha taaluma.

2. Kikundi cha WEMA kimeanzisha pia shughuli za kiufundi na kiuchumi chini ya kitengo kinachojulikana kama; "WEMA ART AND CARPENTRY SKILLS PROMOTION" kwa kifupi kitajulikana kama WACS-Promotion.

Lengo la WACS-Promotion ni kuwapatia ujuzi na utaalamu vijana watakaopenda kujifunza fani za useremala, sanaa za uchoraji na uchongaji vinyago. Kwa upande mwingine kikundi kitakuwa ni chanzo kingine cha mapato. WACS-Promotion watakuwa chini ya usimamizi na uratibu wa WEMA kama ambavyo shughuli nyingine za WEMA hufanyika.

WACS-Promotion kama kikundi cha ujasilia mali na mafunzo,kwa ujumla wake watajishughulisha na mambo yafuatayo; i/ Kutoa mafunzo ya ufundi wa seremala kwa vijana chini ya usimamizi wa mtaalamu kutoka chuo cha VETA Ndanda, ambaye pia ni Mwana-WEMA. ii/ Kufanya kazi za kiufundi zikiwemo; utengenezaji wa samani pamoja na shughuli za ujenzi kwa watu wa kawaida wanaohitaji huduma hiyo zikiwamo shule, zahanati, n.k. kwa gharama nafuu. iii/ Kuanzisha shughuli za uchongaji wa vinyago, uchoraji n.k. kwa kuwashirikiisha wataalamu mabingwa wa kazi hiyo ili baadaye waweze kutoa ujuzi huo kwa vijana watakaopenda kujifunza fani hizo.

3. Wanaharakati wa Elimu, Mazingira na Afya - WEMA, wameanzisha pia kitengo kinachojishughulisha moja kwa moja na maswala yanayowahusu wanawake. Kitengo hicho kinajulikana kama; "WEMA WOMEN EMPOWERMENT GENERATION," kwa kifupi kitajulikana kama WEMA Women-EG.

WEMA Wommen-EG wanaamini kwamba mwanamke akijengewa uwezo na uelewa wa kutosha katika mambo ya elimu, mazingira, uchumi, michezo na afya atakuwa na uwezo wa kukabiliana na maisha, hatimaye kujijengea uwezo utakaomwezeshya kujikwamua kiuchumi, na kuwa tegemeo katika familia. Aidha, WEMA Women-EG wanaamini kuwa mwanamke mmoja akielimika katika familia, basi familia nzima imepata kukombozi unaoihakikishia familia hiyo maisha bora.

WEMA Women-EG katika kumletea mwanamke changamoto ya maendeleo watajishughulisha na mambo yote yaliyoainishwa ndani ya katiba ya WEMA, ambayo ni; Elimu, Mazingira, Afya, Uchumi pamoja na Michezo.

Katika elimu watawahamasisha wasichana ili watilie mkazo elimu kwa mtazamo kwamba kila msichana anayeandikishwa shule, asiishie njiani. Katika mazingira wamejipanga kuhakikisha wanaifikisha elimu sahihi kwa wanawake wote juu ya namna ya kutunza vyanzo vya maji, na kuwaelimisha ubaya wa kukata miti ovyo, bila kupanda mingine. Aidha watawahamasisha wanawake wenzao juu ya umuhimu wa kutumia majiko yasiyotumia kuni nyingi pamoja na utunzaji wa mazingira kwenye makazi wanayoishi. Kwa upande wa afya watashirikiana na asasi nyingine za kijamii na kiraia katika kampeni mbalimbali zinazohusu afya mfano; mapambano dhidi ya malaria, kunawa mikono, usafi wa mazingira, VVU na kinga dhidi ya UKIMWI.

Aidha, watajihusisha pia kuwapatia elimu wasichana wadogo waliopata mimba katika umri mdogo, ya namna ya kutunza mimba ili kuwawezesha kujifungua salama. Pia watatumia nafasi hiyo kukemea tabia ya kuendekeza vitendo vya ngono wangali bado wadogo. Kwa upannde wa uchumi watawatumia wataalamu wanaopatikana katika maeneo yao ili wapatiwe elimu ya usindikaji matunda na uhifadhi, utengenezaji wa vyungu vya kupandia maua, utengenezaji wa batiki, ususi, ubanguaji wa korosho, pamoja na elimu ya biashara. Kwa upande wa michezo WEMA Women-EG watawaunganisha wasichana wa rika tofauti tofauti kwa lengo la kuunda vikundi vya michezo ili kwa pamoja waweze kucheza michezo mbalimbali kama sehemu ya mazoezi. Kila baada ya mazoezi watapatiwa ujumbe unaohusu jambo lolote; mfano, Wachezaji msidanganyike, UKIMWI bado ni tishio.

4. Shughuli nyingine zitakazofanywa na WEMA ni pamoja na kukusanya kazi za sanaa za zamani kutoka kwa makabila manne ya mikoa ya Mtwara na Lindi ambayo ni; Wamakuwa, Wayao, Wamwera na Wamakonde kwa lengo la kuzihifadhi ili kizazi kilichopo na kijacho waweze kuona na kujifunza sanaa za wazee wao ambazo kwa sasa zimetoweka machoni pa watu wengi.