Log in
Wanaharakati wa Elimu Mazingira na Afya (WEMA)

Wanaharakati wa Elimu Mazingira na Afya (WEMA)

Mkalapa, Ndanda-Masasi, Tanzania

Parts of this page are in Swahili. Edit translations

HABARI ZINAZOHUSU WANAKIKUNDI WA WEMA - MKALAPA, WILAYA YA MASASI

1. WANAHARAKATI WA ELIMU, MAZINGIRA NA AFYA - WEMA, WAENDESHA MJADALA WA WAZI KATIKA MJI MDOGO WA NDANDA, MASASI

Tarehe 03 Mei 2010, Wanaharakati wa Elimu, Mazingira na Afya-WEMA, waliendesha mjadala wa wazi uliofanyika katika mji mdogo wa Ndanda uliopo katika wilaya ya Masasi. Katika mjadala huo watu mbalimbali wakiwamo; wadau wa elimu, wazazi, wanafunzi pamoja na wanaharakati wa Elimu, Mazingira na Afya, walishiriki katika mjadala huo.

Mada katika mjadala huo ilikuwa; "Namna disco toto na kumbi za starehe zinavyoathiri watoto na wanafunzi kujifunza." Mjada huo uliongozwa na Mchungaji Joseph Mwanga ambaye pia ni Mtunza Fedha wa kikundi cha WEMA, pamoja na Mr. Allyi K. Kamtande, Katibu wa kikundi cha WEMA.

Washiriki wote waliohudhuria walikubaliana na mada ambayo iliwasilishwa kwa ustadi mkubwa na waongoza mjadala. Waongozaji wa mjadala walitoa mifano mingi ya jinsi "disco toto" zinavyowapawisha watoto kiasi kwamba hawasikilizi makatazo ya wazazi wao. Kwa upande wa pili waongozaji wa mjadala walielekeza lawama kwa baadhi ya wazazi ambao hutoa fedha na kuwapatia watoto wao ili waende kwenye "disco toto" ama kuangalia picha kwenye kumbi za video, wakidhani kuwa kufanya hivyo wanaonesha mapenzi kwa watoto wao.

Katika kuunga mkono hoja hiyo, wapo waliosema kuwa kukithiri kwa kumbi za video vijijini ndiyo kichocheo kikubwa cha matendo ya ngono, na hatimaye kuongezeka kwa mimba za wanafunzi. Aidha, wengine walisema kitendo cha mtoto kwenda kwenye kumbi za starehe kunawakutanisha watoto wenye tabia nzuri, na watoto wenye tabia mbaya kama ile ya uvutaji bangi. Matokeo yake, watoto wazuri hujikuta wakijiingiza katika matendo ya uvutaji bangi pamoja na unywaji wa pombe.

Wachangiaji wengine walienda mbali zaidi kwa kuhusisha swala la kuendekeza starehe na taaluma. Walielezea kuwa, hali ya morali ya usomaji (kujisomea) kwa wanafuzi siku hizi haipo kabisa. Walibainisha kuwa hakuna mwanafunzi anayerudi shuleni akachukua daftari ama kitabu na kujisomea. Matokeo yake ni kushuka kwa taaluma. Washiriki walibainisha wazi kuwa hali ni mbaya zaidi vijijini ambako walimu ni wachache na pia kuna upungufu mkubwa wa vitabu. Washiriki walipendekeza kuwa mijada ya aina hii ni muhimu na kwamba inafaa ifanyike mara kwa mara na katika maeneo tofauti kwani inasaidia kuleta changamoto kwa wananchi. Mjadala huo ulifadhiliwa na shirika la hiari la HakiElimu.

Wanaoonekana kaktika picha ni watoto (wanafunzi) wakisasambua kiduku (aina mojawapo ya uchezaji) kama walivyokutwa na mpiga picha katika moja ya kumbi zilizopo katika mji mdogo wa Ndanda. (Taarifa hizo za mjadala wa wazi zimechapishwa katika magazeti mbalimbali likiwemo gazeti la Mwananchi Na. 03629 la tarehe 25 Mei 2010 uk.10 na Mwananchi Na. 2 linalozungumzia 'Maarifa' uk.2, mada maalumu inayohusu ELIMU.)

 

2. MKUTANO MKUU WA MWAKA WA MARAFIKI WA ELIMU TANZANIA

Siku ya tarehe 01 Septemba 2010 hadi 03 Septemba 2010, kwenye ukumbi wa VETA Dodoma, kulifanyika mkutano mkuu wa Marafiki wa Elimu Tanzania. Mkutano huo uliitishwa na shirika la hiari la HakiElimu. Kwa mujibu wa taarifa ya waandaaji wa mkutano huo, walielezea kuwa mkutano huo ulihudhuriwa na Wanaharakati wa Marafiki wa Elimu wengi zaidi kuliko mikutano mingine iliyotangulia.

Jumla ya washiriki zaidi ya mia moja walihudhuria mkutano huo. Miongoni mwa wanaharakati waliohudhuria mkutano huo, alikuwemo Mratibu na Mshauri wa kikundi cha Wanaharakati wa Elimu, Mazingira na Afya - WEMA, Mr. Mussa P.M. Kamtande.

Kwenye picha anaonekana Mratibu na Mshauri wa kikundi cha WEMA, Mr. Mussa P.M. Kamtande akisisitiza jambo, wakati alipopata nafasi ya kuelezea na kutoa uzoefu wake wa namna kikundi chake cha WEMA kilivyoweza kufanikiwa katika shughuli zake.

Mambo ambayo yameweza kufanywa na kikundi cha WEMA katika kipindi cha miaka mitatu toka kuanzishwa kwake mwezi Januari 2008, ni pamoja na ; Kuanzisha Maktaba ya Jamii Mkalapa, baadhi ya vitabu na machapisho yalitolewa na HakiElimu. Ujenzi wa ubao wa matangazo karibu na ofisi ya kijiji cha Mkalapa, mradi pia uliofadhiliwa na HakiElimu. Kuendesha mijadala ya wazi ambayo nayo ilifadhiliwa na HakiElimu, na Kuendesha vipindi vya redio kupitia redio Pride fm 87.8 ya mjini Mtwara, ambapo marafiki wa elimu kutoka mikoa ya Mtwara na Lindi walishirikishwa. Kati ya mwaka 2009 na mwaka 2010 jumla ya vipindi 23 vilirushwa hewani kupitia kipindi chake maarufu cha "Joto la Wiki" kinachorushwa na redio Pride fm 87.8, kila siku ya Jumapili kuanzia saa 10.15 hadi saa 12.00 jioni.

Kikundi cha WEMA kimefanikiwa pia kuunda vitengo ambavyo lengo lake ni kuwawezesha watu mbalimbali kushiriki katika mafunzo ya ujasiliamali. Kitengo kimojawapo kinajulikana kama; WEMA ART AND CARPENTRY SKILLS PROMOTION ama kwa kifupi; "WACS-Promotion." Kitengo hiki kinajishughulisha na kutoa mafunzo ya aina mbalimbali yakiwemo mafunzo ya useremala, uchoraji na uchangaji vinyago, pamoja na ujasiliamali. Kitengo hiki licha ya kwamba kinasimamiwa na WEMA, kitafanya shughuli zake chini ya Mchungaji Joseph Mwanga, mtaalamu wa seremala kutoka chuo cha ufundi VETA Ndanda.

Kitengo kingine kilichoundwa na WEMA kinajulikana kama; WEMA WOMEN EMPOWERMENT GENERATION, ama kwa kifupi,"WEMA Women-EG". Kitengo hiki kimelenga kuwahamasisha akina mama ambao ndio mhimili mkuu wa familia,ili waweze kushiriki katika harakati mbalimbali za kiuchumi. Katika hatua za awali,WEMA Women-EG wameanza kujifunza utengenezaji wa vyungu vya kupandia maua.

WEMA Women-EG wameanzisha timu za mpira wa pete na wavu kwa ajili ya wasichana, chini ya ufadhili wa; "Sports Development Aid (SDA)" kupitia mradi wake wa; "Mother & Daughter Project". Mradi wa 'Mother & Daughter Project' umelenga kuhamasisha akina mama wapate nafasi ya kufanya mazoezi madogo madogo kwa ajili ya kujenga afya zao. Tafiti nyingi zilizofanyika, zimedhihirisha wazi kwamba akina mama wengi katika nchi zinazoendelea kama Tanzania, wakati wote huwa kazini, na kwamba hawapati muda wa kupumzika. Katika hatua za awali, shirika la hiari la SDA chini ya mradi wa "Mother & Daughter Project" wametoa mipira kwa timu hizo mbili kwa ajili ya mazoezi.

Pamoja na mambo hayo yote, kitengo kinakusudia kuwapatia akina mama mafunzo ya; utaalamu wa utengenezaji wa batiki, utaalamu wa ubanguaji wa korosho pamoja na ufugaji wa kuku wa kienyeji. Aidha, WEMA Women-EG wanakusudia kutembelea taasisi zilizopo katika Kata ya Mwena wilaya ya Masasi ili kuongea na wanafunzi wa kike juu ya umuhimu wa mtoto wa kike kuwa na elimu, pia kuwakumbusha athari za miba za utotoni kwa msichana. Aidha, lengo la baadaye wakiwa na uwezo ni kutembelea taasisi nyingi zaidi katika wilaya ya Masasi.

Kikundi cha WEMA kimesajiliwa rasmi chini ya CBO's na mpango wa baadaye ni kukisajili kuwa NGO. Kikundi kina Katiba pamoja na Mwongozo unaotoa mwelekeo wa mambo yanayoshughulikiwa na yale yanayotarajiwa kushughulikiwa. Wanaharakati wa Elimu, Mazingira na Afya - WEMA wanayashukuru mashirika yote ya hiari ambayo yamekiwezesha kikundi kupiga hatua katika kutekeleza malengo iliyojiwekea

3. WANAHARAKATI WA WEMA WASHIRIKI MAONYESHO YA SERIKALI ZA MITAA

Tarehe 01 Julai 2010 Wanaharakati wa Elimu, Mazingira na Afya-WEMA, walishiriki katika maonyesho ya Serikali za Mitaa yaliyofanyika kiwilaya katika mji mdogo wa Ndanda Masasi. Kikundi cha WEMA kilishiriki maonyesho hayo kwa kuonyesha baadhi ya shughuli wanazozifanya. Walionyesha baadhi ya vitabu vinavyopatikana katika maktaba yao, pia walionyesha baadhi ya miche ya miti waliyootesha katika kitalu chao, hali kadhalika, walionyesha vyungu vya kupandia maua ambavyo ni miongoni mwa kazi wazojifunza kikundi cha akina mama wa WEMA, kinachojulikana kama; "WEMA WOMEN EMPOWERMENT GENERATION" ama kwa kifupi "WEMA Women - EG."

Katika picha wanaonekana watoto waliotembelea banda la WEMA wakati wa
maonyesho hayo ya Serikali za Mitaa, wakisoma vitabu. Aidha, wengine wanaonekana katika picha hiyo, ni baadhi ya wanakikundi cha WEMA ambao walishiriki wakati wa maonesho hayo. Aliyeinama na kugusa mtungi wa maua, ni Mchungaji Joseph Mwanga ambaye ni Mtunza Fedha wa WEMA.

4. UZINDUZI WA MAKTABA YA JAMII YA WEMA - MKALAPA

Tarehe 11 Julai 2009 iliambatana na tukio muhimu na la kihistoria katika kijiji cha Mkalapa. Kijiji cha Mkalapa kipo katika wilaya ya Masasi mkoani Mtwara. Kikundi cha Wanaharakati wa Elimu, Mazingira na Afya-WEMA walizindua rasmi Maktaba yao ya Jamii ya WEMA ambayo ina vitabu na machapisho zaidi ya 750.

Vitabu vilivyomo kwenye maktaba ya WEMA vimechangiwa na wafuatao; HakiElimu (machapisho na vitabu zaidi ya 150), Mratibu na mshauri wa kikundi Mr. Mussa P.M. Kamtande (amechangia vitabu na machapisho zaidi ya 450), pamoja na taasisi kama; Chuo cha Ualimu Mtwara (K), na Chuo cha Ualimu Mtwara (U), ambao kwa pamoja wamechangia machapisho yapatayo 150.

Katika picha hapa chini anaonekana Mwenyekiti wa Kikundi cha WEMA Mr. Fidelis Milanzi akiwa na mgeni rasmi Mr. Richard Lucas wakiangalia vitabu kwenye maktaba hiyo. Mgeni rasmi katika shughuli hiyo ni mwakilishi wa shirika la HakiElimu kutoka makao makuu Dar es Salaam. Anayeonekana kwa nyuma ni Mr. Boniventura Godfrey ambaye pia ni miongoni mwa wageni waliowakilisha shirika la HakiElimu siku hiyo ya uzinduzi wa maktaba. Maktaba ya WEMA ina vitabu vinavyokidhi viwango vyote vya kitaaluma kuanzia; elimu ya Awali, Msingi, Sekondari hadi chuo kikuu.Hivi sasa maktaba hiyo inatumia jengo la kuazima, lakini jukumu lililopo mbele yao ni ujenzi wa jengo la kudumu la WEMA kwa ajili ya maktaba. (Taarifa za uzinduzi wa maktaba ya jamii ya WEMA zilichapicha na magazeti mbalimbali yakiwemo gazeti la "The Citizen" la tarehe 17 Julai 2009 na Mwananchi la tarehe 15 Julai 2009)

5. NAMNA WANA-WEMA WALIVYOWAKUMBUKA WANAFUNZI YATIMA SIKU YA MJADALA WA WAZI - NDANDA

Tarehe 03 Mei 2010 kikundi cha Wanaharakati wa Elimu, Mazingira na Afya-WEMA waliendesha mjadala wa wazi katika mji mdogo wa Ndanda. Wana-WEMA waliitumia siku hiyo kukabidhi misaada kwa wanafunzi watatu ambao ni yatima kutoka katika shule tatu za msingi. Wanafunzi hao ni Genofever Kavili mwanafunziwa darasa la IV kutoka shule ya msingi Mtunungu, Fatuma Hassani wa darasa la VI kutoka shule ya msingi Mkalapa, na Moshi Raphael pia wa darasa la III kutoka shule ya msingi Liputu.

Moja ya majukumu ya WEMA katika elimu ni kuwabaini na kuwasaidia wanafunzi yatima, waliofiwa na wazazi wao na ambao wanashindwa kuendelea na masomo kwa kukosa vitu muhimu kama ada na vifaa vingine kama daftari. Lengo la baadaye la WEMA ni kuwafikia na kuwasaidia wanafunzi yatima wengi zaidi wenye matatizo na ambao wanashindwa kupata msaada kutoka kwa ndugu zao.

Hata hivyo uwezo wa kikundi kuwahudumia watu wengi zaidi itategemea uwezo wa kifedha wa kikundi. Kwa sasa misaada hiyo hutokana na michango ya wanakikundi wenyewe.

 

 

 

 

 

Katika picha inayoonekana hapa juu, anaonekana Mratibu Elimu Kata wa Kata ya Mwena; mama Clara Maona akimkabidhi kifurushi mwanafunzi Genofever Kavili wa darasa la VI kutoka shule ya msingi Mtunungu. Ndani ya kifurushi hicho mna sare ya shule (shati na sketi). Wanafunzi wenzake pia walipewa msaada kama huo.