Fungua
Wanaharakati wa Elimu Mazingira na Afya (WEMA)

Wanaharakati wa Elimu Mazingira na Afya (WEMA)

Mkalapa, Ndanda-Masasi, Tanzania

CHIMBUKO LA KIKUNDI CHA WANAHARAKATI WA ELIMU, MAZINGINA NA AFYA (WEMA)

Asasi ya kiraia ya "Wanaharakati wa Elimu, Mazingira na Afya", kwa kifupi, WEMA ni asasi iliyoanza shughuli zake mwezi Januari 2008. Kikundi cha WEMA kimeanzishwa baada ya kusoma machapisho mbalimbali yanayotolewa na shirika la hiari la HakiElimu. Taarifa nyingi za HakiElimu zinazungumzia juu ya matatizo yanayojitokeza katika elimu. Ukweli wa taarifa za tafiti zao umegusa hali halisi ya matatizo yanayojitokeza katika vijiji vilivyopo Kata ya Mwena. Baada ya kubaini ukweli huo, Wana-WEMA kwa pamoja waliamua kuunda kikundi ili kuwa na nguvu ya pamoja kuwezesha kutoa msukumo kwa jamii kwa lengo la kuchochea mabadiliko katika nyanja ya elimu, afya, uchumi na utunzaji wa mazingira. Harakati za HakiElimu za kuleta mabadiliko katika elimu,ndizo zilizozaa mtandao wa Marafiki wa Elimu nchini. Kikundi cha WEMA ni miongoni mwa vikundi vilivyoundwa kupitia mtandao huo wa Marafiki wa Elimu.

Wanaharakati wa mtandao wa Marafiki wa Elimu ni mtu yeyote ambaye anadhani kuwa, akijiunga na Marafiki wa Elimu anaweza kusukuma mbele mabadili katika elimu hapa nchini. Kwa mtazamo huo kujiunga na mtandao huo ni jambo la hiari, unaweza kujiunga kama mtu binafsi au kama kikundi. Matatizo makubwa yaliyowasukuma wana-WEMA wakafanya maamuzi ya kuanzisha kikundi ni pamoja na kutoridhishwa na mazingira ya shule nyingi za msingi hasa kwa upande wa majengo, vitabu, na taaluma kwa jumla. Kadhalika, hali duni ya ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kidato cha nne, hali inayochangiwa na kushuka kwa ari ya wanafunzi kujisomea vitabu, pamoja na hali ya matumizi mabaya  ya fedha zinazotumwa vijijini kwa ajili ya miradi ya kijiji.

Kata ya Mwena ina shule za msingi zipatazo saba na sekondari nne ikiwemo shule moja ya binafsi inayomilikiwa na madhehebu ya dini, na shule moja ya A'level. Pamoja na kuwepo wanafunzi wengi wanaohitimu kidato cha nne, idadi ya wanafuzi wanaoendelea na masomo ya kidato cha tano ni ndogo sana. Ubora wa elimu umeshuka kwa kiwango kikubwa kutokana na sababu mbalimbali. Pamoja ya kwamba hali inaonekana wazi, lakini hakuna mwenye ujasiri wa kusema kinachotokea. Kikundi cha WEMA kimeazimia kuikumbusha jamii juu ya wajibu wake.

Katika hatua ya awali anaanza kushughulikia; mazingira, afya, uchumi, na kisha baada ya kazi kuwajumuike pamoja kucheza michezo. Kwa upande wa mazingira, wana-WEMA wameshuhudia jinsi mazingira yalivyoharibiwa katika maeneo mbalimbali, pia hata dalili za kutokea jangwa zinaonekana wazi. Wana-WEMA wanaamini kuwa ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira nguvu ya pamoja inahitajika.

Hali katika afya haina tofauti na hali ya mazingira. Wenye jukumu la kuelimisha jamii juu ya afya za wananchi, hawatekelezi jukumu lao. Wana-WEMA wanaamini kwa kutumia nguvu ya kikundi na kuwashirikisha wananchi, wanaweza kukabiliana na matatizo yanayohusiana na afya.

Ili jamii iweze kumudu kufanya mambo muhimu katika maisha inahitaji kuwa na uchumi mzuri. Lakini kwa sasa, hali ya maisha ya wananchi ni mbaya. Wananchi wanaonekana dhahiri kuwa wamelemewa na umaskini wa kipato. Hali hiyo ndiyo inawapa nguvu wana-WEMA kwa kuamini kwamba jamii ikitambua malengo, dira na dhamira ya WEMA, hakuna sababu ya kutokuwa na maisha bora kwa kila mwananchi. Kinachohitajika ni kufanya maamuzi ya dhati ya kupambana na vikwazo vya maendeleo.