Mmoja wa washiriki wa mafunzo ya uanzishaji wa Mabaraza ya Shule kwa njia ya kidemokrasia yaliyotolewa katika kijiji cha Mvumi Misheni. Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Haki zangu Sauti yangu unaotekelezwa na mashirika yasiyo ya kiserikali ya Marafiki wa Elimu Dodoma (MED) na Women Wake Up (WOWAP) yote ya Dodoma kwa ufadhili wa Oxfam GB. Katika maoni ya washiriki hao waliomba suala la vifaa vya elimu hususan kwa wenye ulemavu lipewe kipaumbele.
WATAKA WABUNGE WAJITOKEZE KWENYE MIDAHALO.
Wananchi wa majimbo ya uchaguzi ya Mtera na Chilonwa katika Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma wamewataka Wabunge wao kujitokeza katika mijadala inayowakutanisha ili wapate fursa ya kujadili juu ya matatizo yao. Wapiga kura hao waliyasema hayo katika mahojiano ya ufanisi wa mijadala ya Mahusiano baina ya Wabunge na wananchi inaypfadhiliwa na shirika la The Foundation for Civil Society na kuratibiwa na Asasi ya CHANGONET ya Wilaya ya Chamwino.
Wananchi hao wameeleza kuwa wanakabiliwa na kero mbalimbali ambazo Wabunge wao walipaswa kuzijadili pamoja na kuzipaia ufumbuzi lakini hawajitokezi kuwasikiliza na kuwasababishia usumbufu mkubwa. "hapa kijijini tunakabiliwa na matumizi mabaya ya ardhi na wakati mwingine wanakuja watu wanajifanya wawekezaji na kutudhulumu ardhi yetu, watetezi wetu hao wabunge hawaonekani" alisema Bibi. Kurwa Mkazi wa kijiji cha Manchali.
Wananchi hao walihoji sababu za baadhi ya viongozi wa kisiasa kushindwa kujitokeza katika mikusanyiko ya wananchi wakati wao ndio wahamasishaji wa maendeleo katika maeneo yao na kuwasimamia watendaji wa serikali.
Walimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Bi. Fatma Said Ally kutokana na juhudi anazozionesha kila wakati katika Wialya hiyo na kushauri viongozi wa kisiasa kuiga mfano wa kiongozi huyo. "Mkuu wa Wilaya ameteuliwa na Rais lakini anaonyesha kutujali na kushiriki kwenye mijadala; hao tuliowapigia kura wanajifanya wana kazi nyingi kila tukiwahitaji, kama hizo nafasi zina kazi nyingi waziache wapewe wengine"
Mijadala ya kuimarisha mahusiano na Wabunge katika Wilaya ya Chamwino imekuwa ikifanyika na kukosa ushirikiano wa karibu kutoka kwa Wabunge licha ya uongozi wa Wilaya na Halmashauri kutoa ushirikiano katika kufanikisha Mijadala hiyo.
Tangu mijadala hiyo ianze mwaka 2012 imekuwa ikihudhuriwa na viongozi wa ofisi za Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri ila Wabunge na Madiwani wamekuwa hawatoi ushirikiano wa kutosha.
MED YAANZISHA MFUKO WA ELIMU YA SEKONDARI CHIDACHI
Na. Barakaely Christopher
Shirika la Marafiki wa Elimu Dodoma (MED) kwa kushirikina na wananchi wa kata za Kikuyu Kusini na Mkonze Manispaa ya Dodoma wameanzisha mfuko wa kuwalipia ada na michango mingine wanafunzi wote watakaofaulu mtihani wa darasa la saba na kujiunga na elimu ya sekondari kutoka shule ya msingi Chidachi.
Lengo la mfuko huo ni kuwahamasisha wanafunzi wa shule ya msingi chidachi kuongeza juhudi kwenye masomo yao na kuwa na uhakika wa kuendelea na elimu ya sekondari.
Muasisi wa mfuko huo Bw. Davis Makundi ambaye pia ni Mlezi wa shule ya Msingi Chidachi na Mratibu wa Shirika la Marafiki wa Elimu Dodoma (MED) alianza kampeni ya kuanzisha mfuko huo Septemba mwaka jana katika mahafali ya nne ya darasala la saba ambapo mgeni rasmi alikuwa Meneja wa Benk ya Posta Tanzania Bw. Emmanueli Gyumi aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Posta Tanzania.
Katika mkutano huo wazazi wa wanafunzi wa shule ya msingi Chidachi uliofanyika shuleni hapo wameomba mfuko huo uanze haraka na kuazimia kuwa wazazi wote wenye watoto katika shule hiyo wahusike kuchangia uendelevu wake ili kupunguza mzigo wa kusomesha watoto pasi na uhakika kutokana na kipato duni walichonacho. Akaunt ya Mfuko huo itafunguliwa katika Benki ya Posta Tanzania Tawi la Dodoma.
Katika mkutano huo wazazi walipokea jumla ya madawati 15 na seti moja ya bendi ya shule vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya sh. 1,200,000 fedha ambazo zimetokana na michango ya wadau wa elimu, wazazi na wanafunzi kupitia kazi za mikono kwenye somo la Elimu ya Kujitegemea (EK).
Mwalimu Mkuu wa Shule ya hiyo Bi. Ashura Mhoji alieleza kuwa shule yake imekuwa ikifanya vizuri kwa kufaulisha wanafunzi kwa kati ya 80% hadi 100% kutokana na mwamko na ushirikiano uliopo baina ya walimu, wazazi, wanafunzi na wadau mbalimbali wa Elimu. Aidha alilishukuru shirika la MED kwa mchango wake mkubwa ambao limekuwa likitoa mara kwa mara katika shule hiyo. MED katika mkutano huo imechangia kiasi cha sh. 150,000 kwa ajili ya madawati na mfuko wa Elimu.
Meneja wa Mradi wa MRMV Bi Rehema Mwakajila akiwa na maafisa wa Asasi ya Marafiki wa Elimu Dodoma (MED) alipofanya ziara Mkoani Dodoma kwa ajili ya ufuatiliaji wa Mradi.
Wanafunzi wa shule ya msingi Nghaheleze iliyoko Wilayani Chamwino wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kupokea msaada wa Vitabu vya kiada. Vitabu hivyo vilikabidhiwa kwao na shirika la Marafiki wa Elimu Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma Bi. Fatma Said Ally akiongea na wadau wa Elimu wakati wa uzinduzi wa mradi wa My Rights My Voice unaotekelezwa na Asasi ya Marafiki wa Elimu Dodoma (MED) na Women Wake UP (WOWAP) kwa uhisani wa Shirika la Oxfam GB. Pichani mwenye shati la Blue ni Mratibu wa MED Bw. Davis Makundi na mwenye shati la Black ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino BBaltazary Ngowi.
HAKIELIMU YAPONGEZWA Na. Davis Makundi
Shirika la HakiElimu limepongezwa kwa kazi nzuri wanayoifanya nchini hasa katika kuboresha Elimu na Demokrasia nchini. Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Asasi ya Marafiki wa Elimu Dodoma (MED) Dk. Sinda Hussein Sinda ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma UDOM wakati akifungua mkutano wa wajumbe wa Bodi hiyo ambayo ni ya kwanza tangu MED kupata usajili rasmi.
Dk. Sinda pichani alisema mara nyingi mashirika yanayofanya kazi na wadau wake hupenda kuwatumia wadau hao kama chambo cha kuwapatia umaarufu kwa ajili ya kujikuza wao lakini kwa HakiElimu imekuwa tofauti kwani hadi hatua za mwisho wa usajili waliendelea kutoa ushirikiano kwa MED hadi usajili ukapatikana. "Ndugu wajumbe, tuna kila sababu ya kuwashukuru HakiElimu kwa jambo hili ambalo sote tunaamini bila wao leo hii MED isingekuwepo" alisema Dk. Sinda.
Naye Mratibu wa MED Bw. Davis Makundi aliwaeleza wajumbe kuwa ushirikiano huo umezidi kuimarika kwani HakiElimu licha ya kukubali jina la "Harakati za Marafiki wa Elimu" litoholewe na MED na kutumika; mwishoni mwa mwezi Aprili, 2012 walituma mkataba wa sh. 1,370,000/= kwake kwa ajili ya kuendesha vipindi 10 vya radio Mkoani Dodoma vitakavyohusiana na Elimu, Demokrasia na masuala ya utawala Bora.
Bodi ya MED inaandaa utaratibu wa kufanya mawasiliano na HakiElimu kwa ajili ya kuwaomba wakubali kuwa wanachama wa heshma katika shirika la MED kwa mujibu wa katiba.
Wakati huo huo wananchi wa kijiji cha Chidachi kilichoko Kata ya Mkonze Manispaa ya Dodoma wamesema wanatamani sana HakiELimu ikubali kuwa Mlezi wa Shule ya Msingi Chidachi ambayo licha ya kuwa ni shule changa, imekuwa na mafankio makubwa kitaaluma siku hadi siku.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Bi. Zuhura Muhoji pichani kulia; alitoa ombi hilo kwa asasi ya MED na kuiomba iwasiliane na HakiElimu katika kufuatilia suala hilo. Wazazi na wanajamii wa Mkonze walieleza kuwa HakiElimu limekuwa ni shirika lisilo la kiserikali lenye mfano wa kuigwa kutokana na shughuli zake kuigusa jamii moja kwa moja tofauti na mashirika mengine ambayo yamekuwa yakifanya kazi kwa hisia za mahitaji ya jamii badala ya kuangalia hali halisi ya matatizo ya jamii husika. Shule ya Chidachi ilianzishwa katika Mpango wa MMEM na kuanza kupokea wanafunzi mwaka 2004. Mahafali ya kwanza ya shule hityo yalifanyika 2006 ambapo ufaulu ulikuwa 100%. Mahafali zilizofuata matokeo yake ni kama yanavyoonekana kwenye mabano; 2007 (91%) 2008 (88.8%) 2009 (86.9%) 2010 (87.5%) na 2011 (100%). Pamoja na mafanikio hayo kwa shule ya Chidachi, shule ina upungufu mkubwa wa madawati, nyumba za Walimu, vitabu vya kiada na ziada pamoja na changamoto ya Maktaba.
CLUB ZAOMBA MAKTABA, TUISHENI KUNUSURU UFAULU KIDATO CHA IV, 2012
Na. Davis Makundi
Wanachama wa Club za Marafiki wa Elimu Dodoma kutoka katika shule mbalimbali Mkoani Dodoma wameomba msaada wa kupata walimu na Maktaba za jamii ili kuwanusuru na matokeo mabaya katika mtihani wa kidato cha nne na kidato cha pili mwaka huu.
Wanachama hao ambao ni wanafunzi wa shule za sekondari kutoka katika shule mbalimbali ndani ya Manispaa ya Dodoma wamesema ili kuhakikisha kuwa wanachama wa Club hizo wanakuwa mfano wa kuigwa katika matokeo yao ni vyema uwepo mkakati wa aina yake wa kuongeza ufaulu kwa kuwapatia wanachama hao masomo ya ziada na fursa ya huduma za Maktaba ili kuongeza ufaulu wao.
Maombi hayo ya wana Club yamekuja kufuatia uchambuzi uliofanywa na wanachama hao kwa ushirikiano na MED kuhusu kero ambazo zinawafanya wasifanye vizuri kwenye mitihani yao ya kidato cha pili na ile ya kidato cha nne.
Wakiongea katika mjadala huo wanafunzi hao wamekiri kuwa juhudi za ziada za kila mwanafunzi zinachangia kwa zaidi ya asilimia 70% kiwango cha 30% kilichosalia kinapaswa kutoka kwa walimu, jamii, wazazi na wadau wengine. "tunajitahidi lakini wadau wengine nao watusaidie kupata vitabu na walimu kwa masomo ya ziada ili tufaulu" alisema Charles Chunga pichani mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya Kikuyu Sekondari.
Wakiunga mkono wazo hilo wanafunzi hao walitoa ombi kwa wadau kuchangia uanzishwaji wa Maktaba za jamii na kutafuta namna ya kuwezesha walimu wa masomo ya ziada ili wanafunzi wasio na uwezo wa kujiunga na Maktaba ya Mkoa na malipo makubwa ya tuisheni wapate huduma hiyo kwa gharama nafuu au bure kabisa pale inapo wezekana. ___________________________________________________________________________
MVUA YAEZUA PAA, MABATI YAANIKWA KWENYE NYAYA ZA UMEME Na. Baraka Mosi
Mvua iliyoambatana na upepo iliyonyesha juma lililopita imeezua paa la nyumba moja katika Mtaa wa Chidachi Kijiji cha Mkonze Manispaa ya Dodoma na kuiacha familia hiyo ikiwa haina mahali pa kuishi.
Sehemu kubwa ya paa la nyumba hiyo lililoezuliwa lilisukumwa na upepo na kutua kwenye nyaya za umeme hali iliyo ufanya mtaa huo kukosa umeme kwa muda wa siku mbili mfululizo.
Taarifa zaidi zinasema kuwa hakunamtu aliyejeruhiwa kufuatia tukio hilo lililotokea usimu wa kuamkia jumamosi ya juma lililopita.
___________________________________________________________________________
ULE USEMI WA "MVUMILIVU HULA MBIVU" UMETIMIA Na. Davis Makundi
Ni kama utani lakini ni kweli imetimia kwa binti Kurwa Martin Ng'ondi mwanafunzi wa kidato cha nne (iv) katika shule ya sekondari Changaa iliyoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma. Katika shule hiyo iliyokuwa na wanafunzi watatu (3) wa kidato cha nne wakiwemo wasichana wawili na mvulana mmoja; ni Kurwa pekee aliyehudhuria masomo shuleni hapo mnamo tarehe 4 Aprili, 2011 tulipofanya ziara shuleni hapo.
Akizungumza kwa kujiamini na kuwa na uhakika wa alichikuwa akikisema, Kurwa alituahidi kuwa havunjwi moyo na idadi ndogo ya wanafunzi wa darasa lake na uhaba wa walimu katika shule hiyo bali yeye anacho hitaji ni kuhitimu masmo yake ya kidato cha nne. "najua kuwa nakabiliwa na changa moto ya uhaba wa walimu, idadi ndogo ya wanafunzi na uhaba wa vifaa hapa shuleni; lakini kwangu hili nitakabiliana nalo hadi nimalize masomo ya kidato cha nne" alisema Kurwa."
Ahadi ya binti huyu ilitimia baada ya kuvumilia na kuvuna mbivu zake kwa kufanya mtihani wa kidato cha nne na kuambulia alama 35 ambazo si nzuri kwa wahitimu wetu. Kwa Kurwa yeye angeepuka vipi alama hizi kama darasani wako watatu (wasichana wawili na mvulana mmoja) na shule yake yenye wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne ina walimu watatu?
Kurwa Martin na Zainabu Idi wao walipata alama 35 wakati Yasini Ali yeye alipata alama 33 baada ya kupata daraja D katika masomo ya CIV na GEO. Uvumilivu wa vijana hawa na matokeo yao ni kichocheo kwa vijana wote walio katika shule zetu za kata kutambua kuwa licha ya changamoto ya walimu, vifaa, na mazingira magumu ya kujifunzia na kufundishia; wanapaswa kufanya juhudi za ziada ili kufikia malengo yao. ___________________________________________________________________________
SHULE YAFAULISHA 100%; YAJIKITA KUPELEKA WATOTO SHULE ZA VIPAJI!
Na. Makundi DJ
Shule ya Msingi Chidachi iliyoko katika Kata ya Mkonze Manispaa ya Dodoma; imefanikiwa kufaulisha wanafunzi wote waliohitimu darasa la saba 2011. Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2004 ilifanikiwa na imeendelea kuwa na mafanikio makubwa kitaaluma tangu mwaka 2006 ambapo wanafunzi wake wamekuwa wakifaulu kwa kati ya asilimia 86% hadi 100%.
Kwa mujibu wa taarifa ziliziopatikana katika shule hiyo; uongozi wa shule sasa unajikita kuongeza uwezo wa watoto kitaaluma ili wafaulu kwa kiwango cha jiuu na kuchaguliwa kwenda kwenye shule a watoto wenye vipaji maalum.
Licha ya mafanikio ya Chidachi inakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa vitabu, madawati, vyumba vya madarasa na vifaa vya micheo pamoja na viwanja vya michezo kwa wanafunzi hao.
Uongozi wa shule hiyo hivi sasa pamoja na mikakati hiyo unatafuta wafadhili na wadau mbalimbali kwa lengo la kuchangia maendeleo ya shule ya shule hiyo katika taaluma na michezo.
Shule ya Chidachi ni miongoni mwa shule mpya zilizojengwa katika program ya awali ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM).
___________________________________________________________________________
CHAVITA YALIA NA KUSAHAULIWA NA SERIKALI. Na. Barakaelly Mosi
Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) kimesikitishwa na kitendo cha Serikali kuwasahau katika mipango yake na kuwafanya walemavu kuwa omba-omba kutokana na kusahauliwa huko. Hayo yalielezwa na washiriki wa mjadala wa kuangalia changamoto za walemavu wasiosikia (Viziwi) lililoandaliwa na CHAVITA kwa ufadhili wa Jumuia ya Kiraia ya The Foundation for Civil Society.
Washiriki wa mjadala huo walisikitishwa na kitendo cha serikali kushindwa kuajiri wataalam wa lugha ya alama katika taasisi zake muhimu kama Polisi, Mahakamani, Bungeni, Hosipitali, ofisi za Halmashauri na Televisheni ya Taifa ili kurahisisha uwasilishaji wa taarifa kwa walemavu hao bila sababu zozote za msingi.
Washiriki hao walisema kuwa serikali haina nia ya dhati ya kuwapatia wenye ulemavu wa kusikia haki yao ya msingi ya kuwapatia taarifa kutokana na kuwa wataalam wa lugha ya alama wapo; taasisi zake zinazo fedha za kuweza kuwaajiri lakini hawafanyi hivyo, tatizo ni nini? walihoji.
Aidha walieleza kuwa chama chao kiko tayari kutoa mafunzo kwa watu mbalimbali wenye nia ya kujifunza lugha ya alama ili waweze kurahisisha mawasiliano baina yao miongoni mwa jamii. walitoa rai kwa mashirika, taasisi na vyama mbalimbali vya kiraia kuwa na utaratibu wa kujifunza luhga ya alama ambayo walidai ni rahisi kujifunza na kueleweka kwa urahisi.
******************************************
MARAFIKI WA ELIMU WAJADILI MSWADA WA SHERIA YA UZAZI SALAMA
Na. Davis. Makundi
Wanaharakati wa Elimu kupitia asasi ya Marafiki wa Elimu Dodoma wamepata fursa ya kuijadili rasimu ya Mswada wa sheria ya uzazi salama 2012; na kutoa maoni yao juu ya namna ya kuuboresha mswada huo ambao baadaye utakuwa sheria kamili baada ya kupitishwa na Bunge na kusainiwa na Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wawakilishi wa Club za marafiki wa Elimu kutoka katika shule za Sekondari za Kikuyu ambayo ni ya serikali na shule binafsi ya Jamhuri zote kutoka Manispaa ya Dodoma; walionesha ushiriki wa hali ya juu katika kuchangia mawazo juu ya mswada huo uliofanyika katika ukumbi wa CCT mjini Dodoma.
Mjadala huo ulioandaliwa kwa ushirikiano baina ya mashirika ya CARE International, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) na Shirika la Utepe Mweupe ambapo Mkoani Dodoma mwenyeji wa mashirika hayo ilikuwa asasi ya Marafiki wa Elimu Dodoma (MED).
Washiriki hao walipendekeza kuwa katika mtaala wa elimu liwepo somo la Afya ya Uzazi kwa wanafunzi wa kuanzia angalau darasa la tano na kuendelea hadi katika vyuo ili kuifanya jamii ipate uelewa wa kutosha kuhusiana na suala la uzazi wa mpango na manufaa yake katika jamii na taifa.
Ili kuepuka suala la ndoa za utotoni ambalo licha ya kuwa sasa linapigwa vita na watu mbalimbali huku sheria ikitoa mwanya wa uwepo wa ndoa hizo; washiriki hao walipendekeza muda wa kufunga ndoa uwe angalau miaka 21 muda mambao kwa mtoto wa kike atakuwa angalau amehitimu elimu ya sekondari.
Majadiliano hayo pia yaliambatana na maswali na majibu kutoka pande zote zilizoshiriki (Wawezeshaji na wanafunzi) ambapo kila upande ulionesha umahiri mkubwa katika kuuliza na kujibu maswali hayo. Katika mjadala huo maswali kuhusiana na sheria ya makosa ya kujamiiana 1999 na maswali yahusianayo na Afya ya uzazi yaliulizwa kwa wingi hali iliyoufanya mjadala huo kutoa nafasi kwa idadi kubwa ya washiriki kuchangia.
Washiriki waliomba serikali, taasisi mbalimbali na asasi zisizo za kiserikali kuwezesha kufanyika kwa mijadala ya aina hiyo mara kwa mara ili kukuza uelewa wa wanafunzi na Club za marafiki wa Elimu ili elimu hiyo iyafikie makundi mbalimbali ya jamii kwa haraka.
Akifunga mjadala huo Meneja wa Miradi kutoka sherika la CARE International Bw. David Lyimo aliwataka washiriki kuimarisha Club zao na kuongea bidii katika masomo ili kuwa mfano katika jamii ndani na nje ya shule kwa kufanya vyema kila wakati katika masomo yao pamoja na tabia zao kwa ujumla.