Chama cha Skauti Ulimwenguni kilianzishwa na Muengereza aitwae Sir Baden Powell (BP) tangu mwaka 1907 huko Uingereza katika kisiwa cha Brown Sea,
Uskauti uliingia Zanzibar mwaka 1912 miaka 5 tu baada ya kuanzishwa na Sir Baden Powell.
Chama cha Skauti Zanzibar kilianzishwa Mwaka 1912 kabla ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, baada ya Mapinduzi ya Zanzibar 1964 Mheshimiwa Rais wa kwanza hayati Abeid Amani Karume akaisitisha kuendelea kufanya kazi na kuona kwamba ni sehemu ya ukoloni kwani uskauti huo umeletwa na Waingereza.
Hata hivyo mwaka 1992 Mheshimiwa Rais wa Awamu ya tano Dr Salmin Amour Juma alipokwenda Magila Mkoani Tanga katika jamboree na kuwaona vijana wa Skauti, Mheshimiwa Rais alikuwa na shauku ikiambatana na furaha baada ya kuwaona vijana wa skauti katika mkoa huo, Ndipo akaamua Uskauti huo uwepo na visiwani Zanzibar ili vijana nao waweze kujifunza ubunifu, uzalendo na ukakamavu.
Kutokana na kauli hio ndio kwa mara ya pili uskauti ukafufuliwa na kuundwa kamati maalum ya kufufua Uskauti Zanzibar, chini ya wizara ya vijana katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa wakati huo,
Sura ya kwanza ya uskauti ndipo ilipoanza kuonekena baada ya kuanzishwa kundi la majaribio katika skuli ya Msingi Mwembeladu, hadi kufikia mwaka 2000 Zanzibar kulikua na makundi 15 na Wanachama 150, hadi sasa mwaka 2017 kuna makundi 36 na Wanachama 300 Unguja na Pemba.
Vijana wengi hapa Zanzibar wameshindwa kuwa wazalendo wa taifa lao na kukosa kujiamini pindi wanapoamua kufanya maamuzi sahihi yanayohusu maisha yao, nakujikuta wanaingia katika vikundi viovu,
Kwakua jamii kubwa ya Wazanzibar haina ufahamu na elimu ya kutosha kuhusu SKAUTI , hivyo tumeona ipo haja ya Kuunganisha Makundi yote ya Skauti na kuueneza uskauti katika maeneo mengine ya Zanzibar na kua na usimamizi mzuri wa skauti ili kuweza kuisaidia jamii iliyotuzunguka.
Kupitia kuanzishwa kwa Uskauti imefanya vijana kuwa wakakamavu, weledi na wazalendo katika taifa lao katika kubuni mbinu mbali mbali za kuondoa changamoto miongoni mwao na wananchi kwa ujumla,
Chama cha Skauti Zanzibar ni chama hiari, na wala hakifungamani na vyama vya siasa nchini wala hakina chembe ya ubaguzi wa rangi dini wala jinsia, pia huchangia elimu na Malezi kwa vijana kwa kupitia njia ya ‘Uskauti’ ambapo humjenga kijana kimwili, kiakili, kimtazamo, kijamii, kiimani ili waweze kujitegemea na kuwajibika na kumfanya kijana kujifunza mengi kwa vitendo kama Kusaidia jamii katika Majanga, kutoa huduma za jamii katika siku kuu za kitaifa, Uokozi, na kusaidia jamii katika ujenzi wa Taifa letu