Log in
Tanzania Educational Motivation Alliance-TEMOA

Tanzania Educational Motivation Alliance-TEMOA

Kyela, Tanzania

Parts of this page are in Swahili. Edit translations

MAONI YA TEMOA KUHUSU ADHABU YA MWANAFUNZI MBEYA DAY SEKONDARI

Kwa masikitiko makubwa tunapenda kutoa pole kwa wale wote walioathirika kwa namna moja ama nyingine kutokana na kitendo, maamuzi, ama hatua zilizochukuliwa na upande wowote juu ya suala hili.

Kwa ujumla wake, sisi tuna maoni ambayo yaweza kuwa tofauti na ya wengine ama kufanana kwani suala hili limechangiwa kwa pamoja na vitu viwili. kwanza hisia kali zilitawala suala hili kuanzia kutokea hadi hatua zilizochukuliwa. pili ni kukosekana kwa uelewa wa taratibu za kiutendaji kwa wote waliohusika wakiwemo mawaziri waliotoa matamko mbali mbali. kwa misingi hiyo kuna haja ya kuja na ushauri wa kitaalamu ili kuondoa sintofahamu inayojaribu kutengenezwa na tukio hilo. 

KUHUSU ADHABU YENYEWE:

Hakuna sheria wala kanuni inayounga mkono adhabu ya namna ile katika utumishi aidha wa waalimu ama wa idara yoyote ile hapa nchini. kwa maana hiyo adhabu ile ilikuwa kinyume cha sheria na ilitolewa huenda kwa kukosa ufahamu wa kanuni kwani waliohusika ni wanafunzi ni sio waalimu kamili. Lakini pia inawezekana kuwa adhabu ile ilichangiwa na tabia iliyooneshwa na mwanafunzi katika mazingira husika. kwa mfano: iwapo mwalimu aliamua kumuadhibu mtoto kwa adhabu ya viboko kama alivyoadhibu wengine na mwanafunzi huyo kugoma bila sababu ya msingi (genuine reason why not) na akatoa maneno ya kummudhi mwalimu, kitendo kama kile kinatarajiwa japo sio cha kiungwana lakini kwa hurka ya binadamu huenda kikatokea. 

mwisho wa yote tuseme kuwa kulikuwa na haja ya kutumia muda wetu mwingi kujua sababu ya kutoa adhabu kali kiasi kile ambayo kwa watoto watukutu ni ya kawaida na ina lengo la kukomesha tabia fulani. Temoa tunaamini kuwa mwalimu au mtu yeyote sio kichaa kumwadhibu mtoto mmoja tu kiasi kile bila kuwepo sababu ya kufikia hatua ile iliyotawaliwa na hisia kali. Tunaendelea kuwaamini walimu kuwa ni walezi na wana nia njema na wanafunzi na ndio maana huchukua hatua kali pale wanapoona mtoto anakwenda kinyume na maadili ili afanikishe adhma yake ya maisha. 

Mwalimu anakumbana na mazingira magumu kuliko huenda mtumishi mwingine yeyote hapa nchini kwani ukilinganisha na watumishi wengine wote, mwalimu ndiye pekee anayekutana na watoto kutoka familia zaidi ya miatano kila siku na nio jukumu lake kuhakikisha watoto wenye tabia tofauti wanakuwa na tabia moja njema katika jamii; tabia ya kuwa mwadilifu aliyetayari kujifunza na mzalendo. hii siyo kazi rahisi.

Maoni hayo hayana nia ya kutengua ukweli wa kisheria kuwa mwalimu anapaswa kuzingatia kanuni na miiko ya kazi yake awapo kazini na nyumbani kama ilivyo kwa watumishi wengine. ni muhimu kueleweka kuwa mwalimu ni mtumisha kama walivyo watumishi wengine na anazo haki na wajibu wa kufuata. haiatasaidia chochote kumfanya mnyonge ama kumbeza.

Msimamo wetu huo unatokana na hatua zilizochukuliwa bila kuzingatia nafasi ya mwalimu pamoja na haki ya kusikilizwa kama binadamu (Natural justice), hii haikuwa haki kwa walimu waliohusika na ilikuwa na madhara makubwa kwa wanafunzi wote nchini kwani ilionekana waalimu waliamua kumuonea mwanafunzi na hakukuwa na kosa upande wa mwanafunzi. Tumeipotosha jamii na kurudisha nyuma ari ya walimu kushughulika na maadili ya watoto wenu. (wahusika wafuatuilie mijadala katika baadhi ya majukwaa ya walimu katika mitandao ya kijamii)

KUHUSU MAAMUZI YA SERIKALI

Kwanza niipongeze serikali kwa ukaribu iliouonesha katika kushughulikia suala hili na kuonesha ni jinsi gani serikali iko makini kuona kwamba kanuni na sheria zinafuatwa na walimu wawapo kazini.

Inawezekana kuwa kulikuwa na umuhimu wa kuingilia kati hili suala lakini pia inawezekana kulikuwa hakuna sababu ya msingi kuliingilia kati hili suala na kulitolea maamuzi bila uchunguzi. Ni muhimu kuweka pembeni hisia zetu pale tunaposhughulikia msuala ya kisheria hasa yanayohusu pande mbili, hii itasaidia kutofanya maamuzi yanayopendelea upande mmoja. 

Kwa kawaida uamuzi wa kuwafukuza vyuoni hufanywa na vyuo vinavyodahili wanafunzi husika kwa maana vyuo vyote nchini ni autonomous na vinavyo vyombo vya kinidhamu vinahusika na kufukuza wanafunzi vyuoni. Kuagizwa kunaweza kufananishwa na kumuagiza hakimu kumhukumu kifo mtuhumiwa kabla ya kesi kusikilzwa. Hii haikufanyika vizuri. 

HITIMISHO

Kama chombo kinacho shughulikia maendeleo ya elimu, tunapenda kutoa rai kwa pande zote mbili kuepuka kujiingiza ama kuingiza matendo yanayoweza kuleta mpasuko na mgawanyiko katika jamii kuhusu elimu ya mtoto. Si vizuri kutumia hisia kuamua ama kutoa adhabu mtu yeyote bila kuifanya utafiti. Suala la elimu ni suala la umoja na mshikamano kati ya mzazi, serikali na walimu. Kuwagawa waalimu na jamii ni kuandaa kitu ambacho hakuna atakayeweza kukikabili hapo baadae. maamuzi yote lazima yazingatie haki sheria na kanuni husika. kitendo kile kilisababisha mmomonyoko mkubwa sana wa maadili miongoni mwa wanafunzi na chuki kubwa sana kutoka kwa wazazi dhidi ya waalimu. Si busara kutengeneza hali hii kwa jamii. 

Waalimu wathaminiwe na wapewe nafasi ya kutekeleza majukumu yao. Si busara kuingilia bila kufuata busara na sheria. Wanao uwezo wa kushughulika na Watoto wetu na wakatusaidia kulea kizazi hiki kikaidi. Tunawaomba walimu kusamehe kejeri na matamko yote hasi yaliyotolewa na watu ama jamii na kuendelea kufanya kazi yao kwa weledi bila hofu kwani Tanzania ni yetu site. Tushirikiane kuijenga.

Imetolewa na TEMOA Makao makuu

BEnedict Mwasokwa

Mwenyekiti Mtendaji

October 16, 2016
« Previous Next »

Add a comment

Your name:
Your location:
Your email:
(optional)
Your email address will not be published.