Fungua

/ndanda/post/4362: Kiswahili: WI000CF2AB6BE00000004362:content

« Iliyotangulia   ·   Ifuatayo »
Asili (Kiswahili) Kiswahili

HABARI ZINAZOHUSU WANAKIKUNDI WA WEMA - MKALAPA, WILAYA YA MASASI

1. WANAHARAKATI WA ELIMU, MAZINGIRA NA AFYA - WEMA, WAENDESHA MJADALA WA WAZI KATIKA MJI MDOGO WA NDANDA, MASASI

Tarehe 03 Mei 2010, Wanaharakati wa Elimu, Mazingira na Afya-WEMA, waliendesha mjadala wa wazi uliofanyika katika mji mdogo wa Ndanda uliopo katika wilaya ya Masasi. Katika mjadala huo watu mbalimbali wakiwamo; wadau wa elimu, wazazi, wanafunzi pamoja na wanaharakati wa Elimu, Mazingira na Afya, walishiriki katika mjadala huo.

Mada katika mjadala huo ilikuwa; "Namna disco toto na kumbi za starehe zinavyoathiri watoto na wanafunzi kujifunza." Mjada huo uliongozwa na Mchungaji Joseph Mwanga ambaye pia ni Mtunza Fedha wa kikundi cha WEMA, pamoja na Mr. Allyi K. Kamtande, Katibu wa kikundi cha WEMA.

Washiriki wote waliohudhuria walikubaliana na mada ambayo iliwasilishwa kwa ustadi mkubwa na waongoza mjadala. Waongozaji wa mjadala walitoa mifano mingi ya jinsi "disco toto" zinavyowapawisha watoto kiasi kwamba hawasikilizi makatazo ya wazazi wao. Kwa upande wa pili waongozaji wa mjadala walielekeza lawama kwa baadhi ya wazazi ambao hutoa fedha na kuwapatia watoto wao ili waende kwenye "disco toto" ama kuangalia picha kwenye kumbi za video, wakidhani kuwa kufanya hivyo wanaonesha mapenzi kwa watoto wao.

Katika kuunga mkono hoja hiyo, wapo waliosema kuwa kukithiri kwa kumbi za video vijijini ndiyo kichocheo kikubwa cha matendo ya ngono, na hatimaye kuongezeka kwa mimba za wanafunzi. Aidha, wengine walisema kitendo cha mtoto kwenda kwenye kumbi za starehe kunawakutanisha watoto wenye tabia nzuri, na watoto wenye tabia mbaya kama ile ya uvutaji bangi. Matokeo yake, watoto wazuri hujikuta wakijiingiza katika matendo ya uvutaji bangi pamoja na unywaji wa pombe.

Wachangiaji wengine walienda mbali zaidi kwa kuhusisha swala la kuendekeza starehe na taaluma. Walielezea kuwa, hali ya morali ya usomaji (kujisomea) kwa wanafuzi siku hizi haipo kabisa. Walibainisha kuwa hakuna mwanafunzi anayerudi shuleni akachukua daftari ama kitabu na kujisomea. Matokeo yake ni kushuka kwa taaluma. Washiriki walibainisha wazi kuwa hali ni mbaya zaidi vijijini ambako walimu ni wachache na pia kuna upungufu mkubwa wa vitabu. Washiriki walipendekeza kuwa mijada ya aina hii ni muhimu na kwamba inafaa ifanyike mara kwa mara na katika maeneo tofauti kwani inasaidia kuleta changamoto kwa wananchi. Mjadala huo ulifadhiliwa na shirika la hiari la HakiElimu.

Wanaoonekana kaktika picha ni watoto (wanafunzi) wakisasambua kiduku (aina mojawapo ya uchezaji) kama walivyokutwa na mpiga picha katika moja ya kumbi zilizopo katika mji mdogo wa Ndanda. (Taarifa hizo za mjadala wa wazi zimechapishwa katika magazeti mbalimbali likiwemo gazeti la Mwananchi Na. 03629 la tarehe 25 Mei 2010 uk.10 na Mwananchi Na. 2 linalozungumzia 'Maarifa' uk.2, mada maalumu inayohusu ELIMU.)

 

(Bila tafsiri)

Ili kuhariri tafsiri, lazima ufungue. Fungua · Jiandikishe