Log in
SAIDIA WAZEE TANZANIA

SAIDIA WAZEE TANZANIA

Tanzania

  1. MRADI – LIMA ALIZETI UEPUKE UMASIKINI

1.1  Utangulizi

Shirika la Saidia Wazee Tanzania, (SAWATA MARA) kwa kushirikiana na shirika la kimataifa “HELPAGE INTERNATIONAL – TANZANIA”, limekuwa linashughulikia utetezi na ushawishi kuhusu masuala ya wazee. Mambo muhimu kwa sasa ni:-

  • Matibabu bora bila malipo kwa wazee
  • Msaada kwa wazee wanaouguza wanaoishi na VVU na wanaolea watoto yatima
  • Sera ya Taifa ya Wazee itungiwe sheria
  • Wazee washirikishwe kwenye vyombo vya kutoa maamuzi kuanzia ngazi ya Kijiji, Kata, Wilaya na Taifa
  • Kupewa pensheni jamii kwa wazee wote
  • Kukomesha mauaji kwa wazee wenye umri mkubwa
  • Wazee kupewa pembejeo za kilimo

 

1.2  Juhudi za Serikali

 Kutambua umhimu wa matatizo ya wazee, serikali iliandaa sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003.

Sera inataja sababu ambazo zinatokana na hali ya mazingira ya wazee kama ifuatavyo:-

“Kuwatambua wazee kama rasilimali muhimu katika maendeleo ya Taifa letu.

-          Kutenga rasilimali za kutosha kwa lengo la kuboresha huduma kwa wazee.

-          Kuwashirikisha wazee katika maamuzi muhimu yanayohusu wao na Taifa kwa ujumla

-          Kutoa ulinzi wa kisheria kwa wazee kama kundi maalum”

Haya unaweza kuyapata kwenye aya ya 1.3 ya Sera ya Taifa ya Wazee

 

  Sera ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2003

Sera hii inazungumzia mifuko mbalimbali kwa wazee walio kwenye sekta rasmi.

 Sheria ya mfuko wa bima ya afya ya jamii

Sheria No. 1 ya mfuko wa bima ya afya ya jamii ya mwaka 2001, imelenga kuboresha maisha ya jamii isiyo katika sekta rasmi, kwa kuchangia kiasi kidogo kwa mwaka. Vile vile sheria ya mfuko huu, ibara ya 10 (1) inaruhusu Kamati ya Afya ya Kata, kuidhinisha wazee kusamehewa uchangiaji kwenye mfuko huu, na kupewa kadi ya utambulisho wa matibabu bora bila malipo.

 

 Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Taifa

Katiba  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na marekebisho yake,   ibara ya 12 (2) na ibara ya 14, zinazungumzia wazee kupewa hashima na kupata hifadhi kutoka serikalini na kutoka kwa jamii.

 2 HALI HALISI

Pamoja na kwamba serikali inaonyesha kuwajali wazee, bado maisha ya wazee ni duni

 2.1  Umasikini

Taarifa ya utekelezaji wa MKUKUTA 2009/10, iliyotolewa na Wizara ya Fedha na Uchumi, Novemba 2010, inaeleza kuwa:-

“mapato na matumizi ya kaya ya 2006/07 yalionyesha kuwa uwiano wa watu wanaoishi chini ya mstaari wa umasikini wa mahitaji muhimu ya Tzs 13,998 kwa mwezi mwaka 2007 ulikuwa asilimia 37.6 kwa vijijini, angalia jedwali la 2.13,ukurasa 26.”

Hii ni dhahiri kwamba wazee wengi ni masikini, kutokana na kuishiwa nguvu za kufanya kazi. Kwa hiyo wanahitaji msaada kutoka serikalini, wadau mbalimbali na jamii inayowazunguka.

 

2.2  Wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea

Wazee wengi wa miaka 60+ hawamo katika sekta rasmi, na maisha yao mijini na vijijini yako mashakani. Wengi wako vijijini, wakiwa wameelemewa na umasikini wa kipato. Wengi wamepungukiwa na nguvu za kufanya kazi, hasa wale wanaoanzia miaka 70 na kuendelea. Hawa wanahitaji msaada mkubwa kutoka serikalini na kwa jamii inayowazunguka.

 

2.3  Mifuko ya Jamii ya sekta rasmi

Kuna mifuko mitano inayosaidia kupunguza umasikini kwa wazee walioko kwenye sekta rasmi.

 

  • National Social Security Fund (NSSF)

Hutoa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa watu binafsi, watumishi wa mashirika ya umma ambao hawalipwi pensheni na baadhi ya watumishi wa serikali.

  • Public service Pension Fund (PSPF)

Hutoa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa serikali kuu ambao wanapata pensheni.

 Parastatal Pension Fund (PPF)

Hutoa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa mashirika binafsi na ya umma

 

  • Local Authorities Provident Fund (LAPF)

    Hutoa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa serikali za mitaa.

  • National Health Insurance Fund (NHIF)

    Hutoa bima ya afya kwa watumishi wa serikali kuu walio kwenye malipo ya pensheni

 

Kutokana na mifuko  iliyotajwa hapo juu, hakuna hata mfuko mmoja unaohudumia wazee wasio katika sekta rasmi. Nia ya mifuko hii ni kuzuia na hatimaye kupunguza au kuondoa umasikini.

 

2.4  Mfuko wa bima aya afya ya jamii sekta isiyo rasmi

Kwa vile mifuko iliyotajwa hapo juu haiwatambui wazee wasio katiak sekta rasmi, sheria ya mfuko wa bima ya afya ya jamii “The Commuty Health Fund (CHF) Act, 2001” itumike kuwapunguzia bughudha ya kulipia matibabu. Jamii kulingana na CHF ichangie mfuko huu, ili kuweza kuzipa uwezo zahanati na vituo vya afya vinavyowatibu wazee, kuwa na fedha za kutosha kununua madawa ambayo yatasaidia jamii wakiwemo na wazee.

3 MATEGEMEO YA WAZEE

3.1  Kuongeza kipato

Pamoja na kwamba, wazee wanahitaji msaada, sera ya taifa ya wazee, inawataka washiriki katika miradi ya uzalishaji mali. Shughuli hizi zinaweza kufanyika kwa vikundi. Hasa kwa wazee ambao bado wananguvu kidogo. Lakini wazee wengi hawana elimu ya kutosha, ya jinsi ya kuendesha miradi na kuisimamia.

3.2  Shughuli za kufanya

SAWATA MARA inatarajia kufanya mradi kwa wazee wenye miaka kuanzia 60 na kuendelea. Shughuli zitakazofanywa ni:-

 Kutoa elimu kwa wazee

Katika kuunga mkono mikakati iliyomo katia MKUKUTA II ya kukuza uchumi na hatimaye kupunguza umasikini wa kipato, kuwa na afya njema, SAWATA MARA, inatarajia kuangalia yafuatayo:-

Lengo kuu 1:kuhamasisha watu kujiongezea kipato na hatimaye kupunguza umasikini, kwa njia ya kilimo cha ALIZETI.


Matokeo ya jumla yaliyoweza kupatikana baada ya ushirika mzuri ni haya:-

1. ukuaji wa kipato na ulio endelevu

2. Uwezekano wa kupata ajira binafsi kwa wanawake na vijana

Tumaini kubwa katika lengo hili ni kukuza uchumi wa kipato cha wastani kwa kila mwananchi. Hivyo kuongeza ukuaji wa kipato kitaifa. Na hii inaweza kusaidia ukuaji wa uchumi kutoka asilimia 6 mwaka 2009 hadi asilimia 8 hadi 10 kwa mwaka, ifikapo mwaka 2025, kama inavyoonyesha kwenye MKUKUTA II. Uhamasishaji katika lengo kuu hii, unalenga zaidi katika malengo mahususi yafuatayo:-

1.Usimamizi mzuri wa kilimo bora

2 Kuwa na ukuzaji wa uchumi kwa kuwa na kilimo endelevu kitakachopunguza umaskini              wa   kipato.

3.Kilimo kiweze kutoa ajira kwa rika zote, wazee wa kuime na kike, na vijana, bila kuwasahau walemavu.

4.Upatikanaji wa mafuta ya alizeti kwa wingi, kwa ajili ya kutumia katika kuandaa chakula, na hivyo kuleta lishe nzuri na afya nzuri inayotokana na lishe bora.

5.Mapato yatakayopatikana kutokana na kuuza mazao ya alizeti, yatakuza uchumi wa mtu au familia zinazoishi vijijini.                                                                                                          

     Elimu inatakiwa kutolewa kwa wakulima ili waweze kushiriki katiak programu ya

     Maendeleo ya sekta ya kilimo (ASDP) na ile ya kilimo kwanza. Mwelekeo ukiwa ni kilimo cha     kisasa zaidi.                                                                                                                    Hihi itawezesha kuelewa umuhimu wa kushiriki katika uzalishaji mali. Jinsi ya

Kushirikiana wao kwa wao na serikali za mitaa kwa upande mwingine. Elimu hii itakuwa juu ya kilimo bora, hasa kilimo cha alizeti. Serikali inasisitiza utekelezaji wa sera ya kilimo kwanza Tanzania. Kilimo cha alizeti hakina ugumu katika uandaaji wa mashamba. Wazee watapata faida nyingi zikiwemo za:-

  •  Kupata mafuta ya kupikia, na hivyo kujenga afya zao
  • Kupata fedha baada ya kuuza sehemu ya mazao ya mafuta na kuwawezesha kupata fedha ya kununua mahitaji mengine ya msingi.

 Kutoa elimu ya ujasiriamali

Elimu hii itawawezesha kuandaa mazao ya alizeti ili yaweze kukubalika katika soko. Kuwafundisha utayarishaji na ufungaji wa mafuta ya alizeti kwa kutumia mashini ndogo ndogo. Mafunzo haya yatatolewa na shirika la viwanda vidgo vidogo (SIDO), pamoja na afisa maendeleo ya jamii. Vilevile kujua namna ya kupata soko kubwa la kununua wazao yao endapo yatakuwa mengi. Watakaopata elimu hii ni viongozi wa mabaraza ya wazee, ili wapate uelewa wa zao la alizeti. Wazee 1,050 kwa Kata 22, wanatarajiwa kufikiwa.

Uundaji wa mabaraza ya wazee

Ili kuweza kushrikiana na serikali, vijiji na Kata vitaunda mabaraza ya wazee, ili kushiriki katika vikao vya maamuzi na kuweza kutetea miradi yao na kupata ushauri wa maafisa ugani. Wazee wasio walengwa wa moja kwa moja, wanaotarajiwa kunufaika ni 10,282.

 Kutoa elimu kwa viongozi wa Kata

Lengo kuu 2: Utawala bora pamoja na uwajibikaji. Huduma zinazotolewa kwa wote na kwa kuzingatia zaidi maskini na makundi yaliyo katika hali hatarishi. Ili kufikia malengo, yafuatayo yafanyike:-

 

  1. Kuwa na mipango mizuri inayotoa kinga ya jamii na kutambua thamani ya kila mmoja na hivyo kuleta usalama kwa wote. Hali hii itapunguza hatari dhidi ya makundi yaliyo katika hali hatarishi. Na hii ni pamoja na wanawake, watoto, wastaafu na wazee wote kwa ujumla.

2. Serikali (Halmashauri) kushirikiana na taasisi ambazo zinafaya kazi katika jamii, kusaidia    kuondoa umaskini wa kipato.

 3. Kushawishi utungaji wa sheria inayohimiza utekelezaji wa sera ya Taifa ya wazee ya mwaka 2003.

 

Viongozi wengi wanahitaji elimu ili kuweza kujua umuhimu wa mipango inayoweza kuwaletea wazee kipato. Viongozi watakaopewa elimu hiyo ni:-

  • Madiwani wa Kata 22
  • Maafisa watendaji wa Kata 22
  • Wenyeviti wa vijiji 88
  • Maafis watendaji wa vijiji 88

 Elimu itakayotolewa kwao ni:

  • Utawala bora
  • Ujasiriamali
  • Kilimo cha alizeti.

 Hii ni kuwapa uwezo wa kusimamia vizuri miradi ya wazee.

Ufuatiliaji na tathmini

Kutakuwa na ufuatiliaji na tathmini ya matokeo ya utekelezaji wa mradi

4 WATU WANAOELEKEA UZEENI, MIAKA 50-59

4.1  Shughuli za kufanya

  • Kutoa elimu juu ya mfuko wa bima ya afya ya jamii “CHF”

Lengo kuu 3: Ubora wa maisha “afya, lishe, kpato” unaambatana na ustawi wa jimii, hasa kundi la wazee walio katika mazingira hatarishi.

Lengo hili litafanikiwa tu baada ya kuimarisha mfumo wa afya, lishe na kipato. Utashi mkubwa wa kuongeza watumishi wengi wa afya katika zahanati, vituo vya afya na hospitali na vilevile maafisa ugani katika kata.

Shabaha za kuutekelezaji

Kuhakikisha kuwa wazee wanapatiwa vitambulisho vya kupatiwa tiba bora bila malipo kwa wazee wote. Ili kufikia shabaha hii, mikakati ifuatayo inatakiwa kutekelezwa.

1. Kuorodheshwa majina yote ya wazee walio na miaka sitini  (60+) na kuendelea, kwa kila Kata

2. Kufuatilia upatikanaji wa vitambulisho kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya Musoma Vijijini.

3. Kutoa elimu kwa jamii ili iweze kuwatambua wazee na kuwapa hifadhi.

Kwa watu wenye umri wa miaka 50-59 au chini ya miaka 50, CHF itawasaidia kuwa na uzoefu wa kujiwekea akiba ya matibabau kwenye mfuko huu, na hivyo kulinda afya zao.

Wakiwa katika hali ya afya bora, wataweza kufanya kazi vizuri. Hii itasaidia vile vile zahanati kuwa na dawa za kutosha, kupitia kwenye mfuko wa zahanati, utakaochangiwa na wanakijiji watakaokuwa wanachama wa mfuko huu. Elimu hii, itatolewa kwenye mikutano ya hadhara, kwenye makao makuu ya Kata. Jumla ya watu 15,853 wanatarajiwa kunufaika na elimu hii katika Kata 22 za Halmasahuri ya Wilaya ya Musoma vijijini.

Kutoa elimu ya ujasiriamali

Elimu hii italenga zaidi kuwaelimisha ili waweze kujiandaa kukabiliana na hali ya uzee baadaye. Uundaji wa vikundi mbalimbali vya uasiriamali, ambavyo wanaweza kuviendeleza hata watakapofikia uzeeni, Vikundi hivi vitawezesha kushirikiana na serikali za mitaa katika kukuza mapato yao. Elimu ya kuanzisha mifuko ya akiba ya kuweka na kukopa, “Savings and credit Co- operative Society” (SACCOS).

5. MAMBO YA KUANGALIA

5.1  Hatarishi

Katika kutekeleza mradi huu, inawezekana vikatokea vihatarishi vinavyoweza kukwamisha utekelezaji wa mradi.

  •  Wadudu

Yawezekana kukawa na wadudu ambao wanaweza kushambulia mimea ya alizeti, na hivyo kukwamisha uzalishaji. Afisa ugani wa kila Kata ataweza kubaini hali hii, na kuwasaidia wakulima.

  • Fedha

Mradi huu, unategemea ufadhili. Kupatikana kwa ufadhili kutawezesha utekelezaji mapema.

  •  Utaalam

Upungufu wa maafisa ugani kwenye Kata unaweza kusababisha upungufu wa mazao. Uelewa mdogo wa wakulima unaweza kusababisha uzalishaji mdogo.

  • Utamaduni

Mazoea ya watu kulima mazao mengine tofauti na alizeti  yanaweza kuwa kikwazo. Hapa, elimu itaendelea kutolewa.

6 UTEKELEZAJI WA MRADI

Mradi huu, LIMA ALIZETI UEPUKE UMASIKINI, utatekelezwa na SAWATA MARA kwa ushirikiano na halamashauri ya wilaya Musoma vijijini. Mkurugenzi Mtendaji Musoma Vijijini (DED) atatoa wataalama katika sekta ya:-

  • Kilimo
  • Maendeleo na ustawi wa jamii
  • Afya
  • Mipango
  • Mafisa Watendji wa Kata
  • Maafisa watendji wa vijiji

Vilevile DED atatoa gari katika utekelezaji wa mradi

 7 MIRADI MINGINE

SAWATA MARA itafurahi pia kama itapata ufadhili katika miradi mbalimbali katika maeneo yafuatayo:-

  • Lambo kwa ajili ya ufugaji samaki
  • Utunzaji mazingira- upandaji miti
  • Umeme wa jua

 8 UTAWALA

SAWATA MARA inavyo vitendea kazi vichache vinavyosaidia kuendesha Ofisi. Tatizo kubwa ni ukosefu wa gari la kuwezesha kuwafikia walengwa kwa urahisi. SAWATA MARA itafurahi kupata ufadhili wa gari “Double Cabin Pick up.. TOYOTA HILUX ”

 

9 UMUHIMU WA  UFADHILI

Tunajua umuhimu wa serikali kujua idadi ya watu wake, ni kwa ajili ya kupanga mipango yake kwa ajili ya maendeleo. Au kwa ajili ya kutoa huduma kwa jamii. Idadi ya watu hutolewa kwa kuwekwa katika makundi mbalimbali. Yaani, kwa mfano; Watoto, Vijana na watu wazima. Katika kundi la watu wazima; kuna wanaozeeka tuseme wenye miaka 45 hadi 59), wazee (tuseme wenye miaka 60-75) na waliozeeka (tuseme wenye miaka 75 na kuendelea).

Hapa tunazungumzia zaidi watu wenye umri wa miaka 60 na kuendelea, hasa wale wanoishi vijijini. Watu hawa wameanza kupungukiwa uwezo wa kufanya kazi, kwa vile nguvu zao zimepungua. Kwa maana nyingine wanahitaji usaidizi. Usaidizi huu unaweza kusaidia katika haya yafuatayo:-

  1. Utawawezesha kujua namna mpya za kupambana na maisha katika hali yao ya uzee, baada ya kupata mafunzo ya kuendesha miradi midogo midogo, kabla hawajafikia hali ya kushindwa hata kujipatia maarifa yatakayosaidia kujiongezea kipato.

2.Wazee wenye umri kuanzia miaka 60 hadi 75, wakipewa uwezo wa kuendesha miradi midogo midogo, ambayo inaweza pia kutoa fundisho kwa vijana kuweza kujiandaa na maisha ya uzeeni, itawafaa wazee kujipatia kipato kuendeleza maisha.

3.Miradi ya wazee ikifanikiwa, itakuwa kichocheo kwa vijana ambao wanawategemea wazee. Vile vile kwa watu wanaoelekea uzeeni, wataweza kuiga mifano hiyo.

10. UTABIRI WA MAISHA YA WAZEE

Usitawi wa wazee

Kwa vile wazee wa miaka 60 hadi 75 wanoishi vijijini, wanategemewa kuwa bado wanazo nguvu za kusimamia shughuli za kuwaongezea kipato, kwa usaidizi wa jamii inayowazunguka kwa mambo ambayo yatahitaji nguvu zaidi, maisha yao yanaweza kuboreka.

  •  Msaada kutoka serikalini

Wazee wengi wakiweza kuunda vikundi mbalimbali na kubuni miradi inayowafaa kwenye maeneo wanayoishi, serikali inaweza kuwasaidia kuwapa fedha za kuanzisha miradi hiyo huko vijijini. Vile vile serikali inaweza kuwapa wataalam wa miradi husika kwa mfano, kilimo, uvuvi, mifugo, nyuki n.k.

  •  Msaada kutoka mashirika

Mashirika mbalimbali yenye huruma kwa wazee, yanaweza vile vile kutoa msada unaofaa kwa wazee. Tuelewe kwamba wazee wanakabiliwa na matatizo mengi sana. Ukiacha masuala ya Afya, wazee wanakabiliwa na ulezi wa watoto ambao hawana wazazi (yatima), ama watoto waliotelekezwa. Wanauguza watu wenye VVU/UKIMWI

  • Mabadiliko ya teknolojia

Wazee wanakumbwa na hali ya mabadiliko ya teknolojia, wanahitaji usaidizi wa kupatiwa vitendea kazi kwa mfano, pembejeo za kilimo.

11. MAFUNZO KWA MAENDELEO

Ni vizuri wazee ambao bado wanao uwezo wa kupokea mafunzo na kuyafanyia kazi kwa manufaa ya wazee wengine, wapewe mafunzo ya namna ya kuendesha miradi katika maeneo yao huku vijijini. Mafunzo haya, yanaweza kutolewa kwa njia ya semina fupi. Haya mafunzo yatelenga faida zifuatazo:-

  1. Kuongeza uzalishaji

Mafunzo ya kutosha yanasaidia kuongeza uzalishaji na ubora wa mazoa kutokana na ufanisi wa utendaji.

 2.Kuongeza hamu ya utendaji.

Mafunzo huongeza kujiamini katika utendaji kwa wasimamizi wa miradi. Hii huongeza ujasiri na utashi wa kutekeleza miradi.

3. Mipango ya mahitaji.

Wazee wakiona mafanikio yao, watakuwa tayari kujiwekea mipango ya baadaye ya kuwa na viongozi imara, kuongoza miradai yao kwa ufanisi zaidi, na hivyo kuifanya kuwa endelevi.

4. Kuboresha Afya an usalama.

Kufanikiwa kwa miradi kutofanikisha wazee wawe na kipato kitakacho wasaidia kuboresha Afya zao, na hivyo kuwa na usalama katika maisha yao. Usitawi wa wazee kwa ujumla na hata kwa mmoja mmoja kwenye kikundi utaboreka.

12. JAMII NA SERIKALI YAO

 Wazee wakiwezeshwa, watapunguza utegemezi mkubwa kwa serikali yao. Hali hii itaongeza uhusiano mzuri kwa:-

  • Jamii yenyewe itaongeza ushirikiano
  • Wazee wataitegemea serikali yao kwa mambo ambayo hawana uwezo nayo

13. SABABU ZA KIJAMII NA KIUCHUMI

Tunaelewa kwamba, ni vigumu kuwa na jamii yenye utulivu katika hali ya umaskini, na maendeleo yaliyo nyuma. Na hii husababishwa na mgawanyo mdogo wa rasilimali za taifa. Hali hii husababisha vurugu za kisiasa. Vurugu hizi hujitokeza katika sura mbalimbali, zikiwemo za ukoo, makundi, mila, ubaguzi na hata udini.

14. HAMASISHA

Nini maana ya hamasisha?

Hamasisha ni kitendo cha kumjengea mtu hamasa ya kutaka kufanya kazi. Ni njia ambayo humjengea mtu hamu, msukumo, utashi wa utekelezaji. Humsisimua mtu aweze kufikia lengo lake. Kila binadamu ana kitu kinacho msukuma afanye kitu na siyo kukaa bure.

Ni juu ya jamii kuweza kujua mahaitaji ya wazee, uwezo wao na matarajio yao. Hivyo kuwasaidia, ili waweze kujiongezea kipato. Jamii ikifanya hivyo, itajua namna ya kuwahamasisha na kuwashirikisha ili kufanikisha malengo yao.

Mahitaji ya binadamu

Mara nyingi, mahitaji ya mwanadamu yamegawanyika kama ifuatavyo:-

1 Mahitaji ya kimwili

Wazee wanahitaji kuwa na uhakika wa maisha yao. Hii inajumuisha chakula, mavazi, nyumba nzuri, maji safi na salama, pamoja na mahitaji mengine muhimu.

2 Hifadhi

Baada ya kupata mahitaji ya kimwili, wazee huhitaji hifadhi, kuwa na kipato cha kujikimu, ulinzi na usalama wa maisha yao, na kupata bima ya kinga juu ya hatari, kwa mfano bima ya Afya.

3 Uhuru wa kujumuika

Kila mtu ana uhuru wa kuwa kwenye kundi analotaka. Wazee nao wanatakiwa kushiriki katika vikao vyenye maamuzi, ili waweze kusema yanayowahusu.

15. UFADHILI

Ili wazee waweze kujikimu kwa kuongezea kipato, unaombwa kutoa ufadhili kuendesha mradi wa LIMA ALIZETI UEPUKE UMASIKINI.  Maeneo ya kufadhili katika mradi huu ni:-

  1. Uhamasishaji wa wazee kuwa na mradi wa LIMA ALIZETI UEPUKE UMASIKINI.
  2. Mafunzo ya viongozi wa vikundi juu ya usimamizi wa miradi.
  3. Pembejeo za kilimo.
  4. Ufadhili wa gari TOYOTA HILUX-DOUBLE CABIN, kama kitendea kazi kwa shirika la SAIDIA WAZEE TANZANIA (SAWATA MARA), ili liwezeshe kuwafikia walengwa kwa urahisi.