Tanzania kuwa mwenyeji wa Kongamano la Kimataifa kuhusu uhifadhi wa mbuga za wanyamapori
Wizara ya Maliasili na Utalii inatoa taarifa kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa Kongamano la Kwanza la Africa kuhusu Uendeshaji, Changamoto na Fursa za Uhifadhi wa Mbuga za Wanyamapori na Meneo yaliyohifadhiwa. Ifuatayo ni taarifa kamili kwa umma.
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
TAARIFA KWA UMMA
TANZANIA KUWA MWENYEJI WA KONGAMANO LA KIMATAIFA KUHUSU UHIFADHI WA MBUGA ZA WANYAMAPORI
Wizara ya Maliasili na Utalii inatoa taarifa kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa Kongamano la Kwanza la Africa kuhusu Uendeshaji, Changamoto na Fursa za Uhifadhi wa Mbuga za Wanyamapori na Meneo yaliyohifadhiwa (The 1st Pan-African Conference on Sustainable Tourism Management In National Parks and Protected Areas: Challenges and Opportunities). Kongamano hilo limepangwa kufanyika katika kituo ya cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) tarehe 15 hadi 19 Oktoba 2012. Washiriki wapatao 300 kutoka nchi mbalimbali wanatarajia kuhudhuria mkutano huo.
Tanzania imeteuliwa kuwa mwenyeji wa Kongamano hilo na Shirika la Umoja wa Mataifa Utalii Duniani (UNWTO) kufuatia mkutano wake (UNWTO General Assembly) ambao ulifanyika nchini Korea tarehe 14 hadi 18 Oktoba 2011. Katika Mkutano huo Tanzania ilichaguliwa kuwa mjumbe katika Baraza la Utendaji (Executive Council) la Shirika hilo hadi mwaka 2015. UNWTO ni shirika la Umoja wa Mataifa linaloongoza masuala ya Sera, Mafunzo, Uendelezaji na Utangazaji katika sekta ya utalii duniani.
Kongamano hilo la Oktoba 2012 ambalo ni la kwanza la aina yake litawakuwakutanisha wahifadhi na wadau wa sekta ya Utalii ili wajadili namna ya kufanikisha uhifadhi na utalii. Tanzania imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa Kongamano hilo kutokanana na sifa nzuri na uzoefu tulio nao katika kuanzisha na kuendesha hifadhi za Taifa.
Tanzania itanufaika kwani washiriki wa Kongamano hilo watapata fursa ya kutembelea vivutio vyetu vya utalii, watatumia fedha kwa malazi, chakula, burudani na huduma nyingine watakazotumia wakiwa hapa nchini na hivyo kuacha fedha katika mzunguko wa kiuchumi hapa nchini. Aidha, tutatumia Kongamano hilo kutangaza vivutio vyetu vya utalii. Faida nyingine kubwa ni kuwa, washiriki wa Tanzania watapata fursa kushiriki kwenye Kongamano hilo kwa gharama nafuu na watapata nafasi ya kubadilishana ujuzi na ueledi kutoka kwa wenzao wa nchi za nje.
Wito unatolewa kwa wanachi, wafanyabiashara na wadau wote kujiandaa ipasavyo ili kunufaika na ujio huo wa kimataifa. Taarifa mbalimbali zitaendelea kutolewa kuhusu maendeleo ya matayarisho ya mkutano huo
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
16 Februari 2012