Log in
Baraza la Watoto wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Baraza la Watoto wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Dar es Salaam, Tanzania

Baraza la Watoto wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lina historia inayoanzia katika Mkutano wa watoto kutoka sehemu mbalimbali nchini Tanzania bara na visiwani waliokutana katika mkutano wa maandalizi ya Mkutano Maalum wa Baraza la Umoja wa Mataifakuhusu watoto uliofanyika tarehe 8-10 Mei 2002. Mkutano huo wa Umoja wa Mataifa hukutanisha Maraisi kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. Katika kikao cha maandalizi kilichoitishwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kilichofanyika mwezi mei Mwaka 2000 cha maandalizi ya kundi la watoto waliokuwa wawakilishe watoto wa Tanzania katika Mkutano huo wa Umoja wa Mataifa, waliweza kutafakari ushiriki wa watoto katika masuala yanayowahusu pamoja na mambo mengine ya ushiriki wa watoto katika uandaaji nja utungaji wa Sera na sheria mbalimbali zinazogusa haki na Ustawi wao.

Changamoto zilizojitokeza katika vikao vilivyoainishwa hapo juu ndio msingi uliosababisha kuamua kuunda chombno kitakacho hakikisha ushiriki wa watoto katika ngazi mbalimbali kutoka ngazi ya familia hadi ngazi ya Taifa. Chombo hiki kilitarajiwa kuwa cha uwakilishi na utetezi katika masuala yanayogusa ustawi wa watoto yawe ya Kitaifa au kimataifa. Chombo kilichoundwa kilipewa jina la Baraza la Watoto wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

 

Baraza hili liliundwa rasmi mwezi Disemba, 2002 ambapo uundwaji wake umepitia mchakato mrefu uliohusisha vikao kadhaa ambavyo hatimaye kuwezesha kuundwa kwa mfumo wa uongozi, utendaji na uteuzi wa wawakilishi katika ngazi mbalimbali za Baraza. Taratibu hizo zilizokubaliwa katika vikao hivyo rasmi zilisadia kupatikana kwa Katiba ambayo ndiyo inayoongoza utendaji wa Baraza hili.

Ili kuwezesha uendeshaji rahisi na kuweka viwango vya kiutendaji vya Baraza, katika kikao cha pili cha Kamati Kuu ya Baraza la Watoto wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilichofanyika tarehe 23 mpaka 25 Aprili, 2003, kilipendekeza kuwepo kwa mwongozo na utumike kwa ajili ya kuwezesha kuundwa  kwa mabaraza ya mikoa na Wilaya. Katika Mkutano Mkuu wa pili wa Baraza la Watoto wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliofanyika tarehe 20 – 22 Decemba 2003, Bagamoyo mkoa wa Pwani, wajumbe walipitisha mwongozo huo wa kwanza ili uweze kutumiwa na watoto mikoani ili kusaidia kuanzisha mabaraza katika ngazi ya mkoa na wilaya.

Kuundwa kwa Mabaraza haya kunaenda sambamba na nia ya Tanzania kukidhi haja ya mikataba ya Kimataifa na kikanda ikiwemo ya Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto na ule wa Umoja Wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto. Uundaji wa mabaraza haya katika mikoa, wilaya, kata na vijiji utasaidia kukuza uwezo wa watoto kiufahamu kuhusu masuala yanayowahusu katika maeneo husika, kujenga utamaduni wa demokrasia na kuboresha dhana ya utawala bora katika kizazi hiki kinachotarajiwa kushika hatamu. Halikadhalika, mabaraza ya Watoto yatasaidia kuhakikisha Watoto wanapata fursa ya uhakika ya kujumuika, kushiriki, kushirikishwa, kutoa maoni yao, kusikilizwa na kufanyiwa kazi kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto kifungu cha 12, na 13 na kwa mujibu wa Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto kifungu cha 7, 8 na 9. Tanzania ni nchi mwanachama na imesaini na kuridhia mikataba hii.

Aidha, Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya Mwaka 2008 imeanisha tamko la Sera kuhusu uanzishwaji mabaraza haya katika ngazi mbalimbali. Ni muhimu kuzingatia kuwa mabaraza haya ni sehemu ya utekelezaji wa sheria ya Mtoto namba 21 ya Mwaka  2009. Katika sheria hii, pamoja na mambo mengine, ibara ya II kifungu cha 11 cha sheria hii kinasisitiza umuhimu haki ya mtoto katika kujenga hoja, na haki ya kutoa maoni, kusikilizwa na kushiriki kikamilifu katika mambo yanayohusu ustawi wake bila kikwazo chochote. Ibara ya VIII ya Sheria hii, inaainisha wajibu na majukumu ya Serikali za Mitaa katika kulinda, kukuza na kuendeleza ustawi wa Mtoto kwenye maeneo wanayoishi. Kifungu cha 94 cha ibara hii kinaweka msisitizo wa wajibu wa Serikali za Mitaa katika kusimamia na kuhakikisha ustawi na maendeleo ya mtoto. Uundwaji na usimamizi wa uendeshaji wa Mabaraza ya Watoto katika ngazi mbalimbali za serikali  ni sehemu ya utekelezaji wa wajibu huu unaotolewa kisheria.