KUHUSU UBOMA.
Utawala Bora kwa Maendeleo (UBOMA) ni asasi isiyo ya kiserikali, isiyolenga kupata faida binafsi iliyoanzishwa mwaka 2009 na kusajiliwa Machi 26’ 2010 na Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na watoto kwa hati yenye namba OONGO 3798.
UBOMA ilianzishwa kwa lengo la kupigania upatikanaji wa maendeleo endelevu kwa jamii ili kuona kwamba siku moja jamii ya kitanzania inaishi ikiwa bora katika kila sekta. Katika kulitimiza hili, Uboma ilifanya utafiti mdogo kuhusu wavuvi na maisha yao katika kata za Kibirizi na Katonga na haya hapa chini.
HALI IKOJE KIBIRIZI NA KATONGA?
Wakazi wa Kibirizi na Katonga ni miongoni mwa wananchi wengi masikini wa mkoa wa Kigoma wanaoishi chini ya dola moja kwa siku. Licha ya kujishughulisha na uvuvi na kuzungukwa na Ziwa Tanganyika lenye Samaki, Dagaa na rasilimali anuai ambazo ni malighafi adhimu na inayohitajika kote Tanzania na nchi za nje; bado wengi wao wameendelea kuishi katika lindi la umasikini wakikabiliwa na ukosefu wa huduma bora za Afya, Elimu bora na miundombinu duni ya umeme maji na barabara.
Pamoja na hali hii, wananchi hawa wamekuwa wakichangia pato la taifa kupitia kodi na ushuru wa bidhaa kila wanapotoka ziwani kuvua samaki au dagaa. Wakati mwingine hulilipa hata jeshi la Ulinzi la Tanzania (JWTZ) kiasi cha Tsh 10,000 kila mwezi ili liwalinde na majambazi wanapokuwa katika uvuvi Ziwani nyakati za usiku! Hili ni jambo la ajabu kwa kuwa jeshi linaendeshwa kwa kodi za watanzania na Ulinzi ni jukumu lake la msingi.
Katika uchunguzi wake UBOMA imefanikiwa kuongea na wavuvi kadhaa wa Kibirizi na Katonga kuhusu jinsi wanavyoshirikishwa katika mipango mbalimbali ya maendeleo ya kijamii katika kata zao na ile ya kuboresha sekta ya Uvuvi, aidha kama wanafahamu haki yao ya kushiriki katika upangaji wa viwango vya ushuru kisha kupatiwa taarifa ya makusanyo na matumizi na mamlaka zinazohusika (Halmashauri). Jibu lilikuwa hapana.
Wavuvi wote waliohojiwa wameeleza kutofahamu na kwamba wanachojua serikali wanakusanya fedha zao kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kiserikali. Hali hii ndiyo iliyoisukuma UBOMA kuandaa Mafunzo ya Usimamizi wa Rasilimali za sekta ya uvuvi kwa wavuvi na wadau muhimu wa sekta hii ili kuhakikisha zinawanufaisha na hivyo kuinua uchumi wa jamii ya wavuvi ikiwa ni pamoja na kuboreshwa kwa huduma za kijamii.