MED Yaanza Mchakato wa kupata Usajili wa Kudumu. (Na Prince Kimaro)
Asasi ya Marafiki wa Elimu Dodoma (MED) imeingia katika mchakato wa kupata usajili wa NGO ili kuongeza ufanisi katika kazi zake baada ya kufanya kazi kama CBO kwa kipindi cha miaka mitatu.
Mratibu wa MED na mwanaharakati wa Elimu na Maendeleo Mkoani Dodoma Bw. Davis Makundi amesema ana uhakika kwa kazi zilizofanywa na MED katika hatua ya CBO; zinatosheleza sasa kujikita katika hatua ya juu zaidi ya kuwa NGO ili kufanya kazi katika eneo kubwa zaidi Mkoani Dodoma.
Bw. Makundi pichani alieleza kuwa anajua kuwa eneo alilochagua ni gumu na lina changamoto nyingi ambazo zitahitaji umakini katika kuzikabili na kufikia malengo ya uwepo wa asasi hii. "Sekta ya Elimu; suala la Demokrasia; changamoto ya Utawala bora na haki za makundi mbalimbali wakiwemo vijana hasa wanafunzi, wanawake, wenye changamoto za ulemavu nk tutazifanyia kazi kwa umakini mkubwa ili kurejesha faraja kwa makundi hayo.
Bwana Makundi amesema MED itasajiliwa kama NGO itakayo fanya kazi zake katika Mkoa wa Dodoma na kujihusisha na uhamasishaji katika kuboresha Elimu, Demokrasia, Utawala Bora, haki za wanafunzi, kuimarisha mawasiliano baina ya jamii na serikali pamoja na kupambana na umaskini miongoni mwa jamii. "Kufanya kazi kwenye NGO ni kutumikia umma; ni lazima tujitoe na kuweka rehani maisha yetu kwa ajili ya Taifa" Alisema.
Akizungumzia suala la mchakato wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Makundi amesema suala la Katiba ni la watanzania wote bila kujali kiwango chao cha Elimu, taaluma, umri, hali ya kifedha na hata kiafya; hivyo mjadala wa katiba uwe huru na kila mtu apate nafasi ya kutoa maoni yake bila kuwepo kwa kipingamizi.
Asasi ya MED imekuwa ikiendesha mijadala, mikutano ya majadiliano, kuanzisha Club za Marafiki wa Elimu katika shule za Msingi na sekondari ambazo zimekuwa zikijadili masuala mbalimbali yanayo wakabili wanafunzi katika shule zao.
Shughuli za Marafiki wa Elimu Dodoma zimeongeza chachu ya harakati katika maeneo mengi ya mji wa Dodoma hasa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambao hivi sasa wanaendesha club zao kutetea haki za wanafunzi, maendeleo ya shule, masuala ya demokrasia, utawala bora na maendeleo ya jamii katika maeneo yao.
Ibitekerezo (6)
good job
NILIKUWA NAOMBA NA WATU WENYE ULEMAVU WAJARIBU KUANGALIWA KWA SABABU WENGINE HAWANA MSAADA WOWOTE KWA MFANO MIMI HAPA SINA MSAADA WOWOTE ULE NATOKA NYUMBANI KWA MIGUU NAKURUDI KWA MIGUU BASI JAMANI JARIBUNI KUANGALIA NA HILI KWA WATU KAMA SISI WENYE ULEMAVU. MCHANGO WANGU NDIYO HUO SINA MENGI YAKUONGEZEA.