Mpango wa utoaji wa elimu ya watu wazima vijijini uungwe mkono
Na ASIA KILAMBWANDA
Taaluma ni nyenzo kubwa ya kufikia maendeleo , pia huharakisha mipango ya kufika katika Nyanja mbalimbali za kiuchumi, kijamii na hata kisiasa bila kujali taaluma hiyo ni nadharia ama vitendo inategemea jinsi ya matumizi ya taaluma hiyo.
Katika kulifahamu hili Halmashauri ya wilaya ya Mtwara Vijijini kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la kuwahudumia watoto (Unicef), imeandaa mpango wa utoaji wa elimu kwa watoto waliopita muda wa kuandikishwa kujiunga na elimu ya shule ya msingi, elimu ya watu wazima ujulikanao kama MENKWA .
Mpango huo umetoa mafunzo ya walimu watakaoshiriki kakika ufundishaji wa wanafunzi watakaosoma elimu ya watu wazima(MENKWA),katika mkakati wa kuondoa ujinga na umasikini na kuongeza idadi ya watu wanaojua kusoma na kuandika .
Mafunzo haya yaliwashirikisha 60 na wadau wa elimu katika ngazi ya kata ili kukidhi mahitaji ya wananchi na watoto katika utoaji wa elimu husika bila kuathiri kundi au nafasi na haki ya kupata elimu.
Baadhi ya kata zilizoshiriki ni Naumbu, madimba, Tangazo, nanyamba, likomnde, Dihimba, Msimbati, Nitekela, Mgau na Malanje. Na nyingine ni mayembe chini, mchanja, msanga mkuu, chawi, libobe, Bandari, kilambo na Nachenjele.
Matarajio ya elimu au taaluma yeyote katika jamii ni kuona kwamba inaleta tija na mabadiliko katika nchi, kwa mtu binafsi na taifa kwa ujumla.
Kwa hali hii mpango wa kutokomeza ujinga hasa katika maeneo yaliyosahaulika(Vijijini) utaondoa ufinyu wa kufikiri unaowafanya vijana wengi washindwe kujituma kutokana na ukosefu wa elimu jambo ambalo ni hatari kwa maisha ya vijana.