WAZAZI WALEZI WAELIMISHWE JUU YA HAKI ZA WATOTO NA KUZITEKELEZA Matukio ya utumikishaji watoto hasa katika ngazi ya familia umeongezeka. Hali hii inachangiwa kwa kiasi kikubwa na umaskini, ukatili wa majumbani na matatizo ya wana ndoa, mambo ambayo husababisha ongezeko la watoto wa wanaoishi katika mazingira magumu na kwa sehemu kubwa ni kutokana na wazazi wengi kutozijua haki za watoto kama zilivyoainishwa kwenye Sera ya taifa ya watoto, Sheria ya watoto na ajenda 10 za watoto kitaifa. Pia chanzo kingine ni hali ya uyatima unaotumiwa na baadhi ya wanafamilia wanaotaka kunufaika na mali za mtoto yatima ambaye wazazi wake walifariki wakiwa na uwezo wa mali. Kimsingi unapokuwa yatima ni rahisi kudhulumiwa mali kutokana na kukosa uwezo au uelewa wa kuweza kujitetea na kudai haki au mali. Haki ya kulindwa hupotea na mtoto anakosa mapenzi kwa kwa walezi wenye uchu wa kurithi mali za yatima hao kinyume na sheria. Kwa kawaida vitendo hivi vya dhulma na uvunjaji wa haki za watoto vimekuwa vikifanywa na watu walio karibu na watoto haasa ndugu wanaojumuisha wazazi ama walezi kama riporti ya UNICEF Augost 2011 inavyoeleza. Ripoti hiyo inabaini kwamba 60% ya watoto walioweza kutoa taarifa ya kufanyiwa vitendo vya uvunjifu wa haki, ukatili wa kimwili, walifanyiwa na ndugu wakiwemo baba na mama.
Itakumbukwa akizungumza bungeni Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Lucy Nkya Julai mwaka huu, alisema jumla ya watoto 802,100 nchini wanaishi katika mazingira hatarishi. Hii ni idadi kubwa na inadhihirisha uwepo wa vitendo vya uvunjaji wa haki za watoto na vimeshamiri kwa kiwango cha kutisha katika nchi yetu. Kwa kutambua hili CHIDA kama asasi ya kiraia inaona tunalo jukumu la kulitokomeza tatizo hili kwa kutoa elimu kwa wazazi na walezi ili kuhimiza jamii kubadilika na kuhakikisha kuwa familia ambayo ndiyo kitovu cha jamii yote inakuwa ni mahala salama penye upendo, amani na mshikamano miongoni mwa wanafamilia kwa kuwapatia watoto haki zao za msingi ikiwamo haki ya kuishi. Elimu hii itawafanya wanafamilia kuwa wavumilivu na kuchukua maamuzi yenye kuzingatia maslahi ya watoto kama Sheria ya Watoto ya mwaka 2009, uanzishwaji wa mabaraza ya watoto, na Sera ya Maendeleo ya Watoto ya mwaka 2008 vinavyoagiza pia ikiwa ni pamoja na maazimio kadhaa ya kimataifa yanayolenga kulinda haki za watoto kama vile Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (1999) na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (2003). WITO CHIDA inatoa wito kwa mashirika yajitokeze kwa kufadhili ili kunusuru hali ya uvunjifu wa haki za watoto katika vijiji vya Nyololo Njiapana, Nyololo Shuleni, Lwing’ulo katika kata ya Nyololo pamoja na ile ya Bumilayinga/Maduma ambako ndiko watoto wengi wanatoka. Utafiti wetu unaonyesha idadi kubwa ya watoto wa sehemu hizi wanaomaliza darasa la saba ndio wanaochukuliwa kwa wingi ili kufanya kazi za ndani (Housegirl) jijini Dar namara nyingi huchukuliwa kwa ridha ya wazazi hawa hawa wasiozijua haki za watoto. |