MISITU NI UHAI
HIFADHI NA MATUMIZI ENDELEVU YA MISITU
Misitu ni nini?
Misitu ni ardhi yoyote yenye uoto wa mimea na wingi wa miti ya kimo
chochote ivunwayo na isiyovunwa na iliyo na uwezo wa kutoa timbao au
mazao mengine yenye kurekebisha hali ya hewa au mfumo wa vyanzo vya
maji au yenye kuhifadhi mifugo au wanyamapori
Msitu wa hifadhi
Hili ni eneo la misitu, aidha kwa uzalishaji wa mbao na mazao mengine ya
misitu, ama ni kwa ajili ya ulinzi wa maeneo muhimu yenye lindimaji chini ya
udhibiti wa sheria ya misitu baada ya kutangazwa na waziri mhusika.
Matumizi endelevu ya misitu
Maana ya matumizi endelevu ya misitu
Matumizi endelevu ya misitu ni utumiaji wa maliasili zilizopo kwenye msitu
pamoja na kuendelea kuzizalisha maliasili hizo bila kuathiri uwepo wake.
Katika matumizi endelevu kwa kawaida kiasi kinachovunwa hakizidi uwezo
wa eneo lile wa kuzalisha maliasili hizo. Kwa maana hiyo, japokuwa maliasili
hizo zinatumiwa, ni rahisi kuwepo kwa ajili ya vizazi vijavyo ikiwa matumizi
yake ni endelevu.
Namna ya kufanya matumizi endelevu ya misitu
Kuna njia mbalimbali za kuhifadhi na kutumia misitu katika njia endelevu
kama ifuatavyo:
Ushirikishwaji wa wananchi katika kusimamia na kuhifadhi misitu
Maana ya usimamizi shirikishi wa misitu
Usimamizi Shirikishi wa Misitu (USM) unahusu utaratibu wa kusimamia
misitu ambapo jamii inahusika kwa sehemu kubwa katika
utekelezaji.Usimamizi huu unaweza kuwa kwenye misitu iliyohifadhiwa
ndani ya ardhi ya kijiji au ardhi ya jumla au kwenye misitu ya hifadhi ya
serikali
Sababu za ushirikishwaji
Lengo kubwa la usimamizi shirikishi wa misitu ni kuwashirikisha wananchi
katika kuendeleza kuhifadhi na kutumia misitu kwa vizazi vilivyopo na
vijavyo. Hapo awali wakati wa sheria za misitu za kikoloni shughuli za
kuhifadhi misitu ziliendeshwa kama za kijeshi na hivyo kujenga mawazo
kuwa misitu ni mali ya serikali na wananchi hawahusiki. Kutokana na hali
hiyo wananchi hawakuipenda misitu iliyowazunguka na walijenga uadui
mkubwa baina yao na watendaji wa idara ya misitu matokeo yake
uharibifu wa misitu uliendelea kwa kiasi kikubwa. Kwa kuwa watumiaji
wakubwa wa misitu ni wananchi wanaoizunguka, serikali iliona ni vyema
ikawashirikisha wananchi wake katika swala zima la kuhifadhi ndiyo
maana siku hizi wananchi wanashiriki kwenye suala la kuhifadhi misitu
kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kutoa maamuzi. Swala la ushirikishaji
limeainishwa kwenye sera ya taifa ya misitu (Forest policy) ya mwaka
1998 na sheria ya misitu (Forest Act ya mwaka 2002)
Faida za ushirikishwaji
Faida za ushirikishwaji wananchi kwenye kuhifadhi misitu zipo nyingi
ikiwa ni pamoja na wananchi kushiriki kwenye kufanya maamuzi
kuhusu misitu yao, Kupata fursa ya kujipatia mazao ya misitu kama
kuni, madawa, matunda na mboga bila vikwazo, wananchi kupewa
fursa ya kanzisha misitu yao ya hifadhi kama vile misitu ya hifadhi ya
kijiji, ya vikundi na hata ya mwananchi mmojammoja.
Kwa upande mwingine serikali inanufaika kwa kuwa inaongezewa
nguvu na wananchi katika kuhifadhi misitu. Idadi ya misitu katika
Tanzania ni kubwa sana ukilinganisha na idadi ya watumishi wake
hivyo kwa kuwashirikisha wananchi wanasaidia katika swala zima la
kulinda misitu ili isiharibiwe na wahalifu wenye nia mbaya.
Matumizi ya mila za jadi katika kuhifadhi misitu
Matumizi ya mila za jadi kama tambiko yamechangia kwa kiasi kikubwa
kulinda misitu katika maeneo ya Usambara na sehemu nyinginezo
mbalimbali Tanzania kwa kuwa maeneo yanayotumika kwa shughuli za jadi
yamekuwa yakipewa heshima ya pekee. Kwa mfano wanavijiji na wazee wa
tambiko wamekuwa wakipanga faini kama za mifugo au pombe na hata fedha
kwa yeyote aliyejaribu kukiuka kanuni za utunzaji wa maeneo haya muhimu.