Envaya

HOTUBA YA MGENI RASMI

MAADHIMISHO YA SIKU YA WAZEE KITAIFA MKOANI MWANZA.

  

HOTUBA YA MHESHIMIWA STEPHEN MASATU WASIRA, WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS – MAHUSIANO NA URATIBU KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA WAZEE DUNIANI UWANJA WA KIRUMBA, MWANZA, TAREHE 1 OKTOBA 2012

  

  • Mheshimiwa Dkt. Seif S. Rashid (Mb.), Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
  • Mheshimiwa Eng. Evarist Ndikilo, Mkuu wa Mkoa Mwanza,
  • Waheshimiwa Wabunge, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
  • Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya na Wakurungenzi,
  • Mheshimiwa Mkurugenzi Mkazi wa Help Age International,
  • Viongozi na Watumishi wa Serikali mliopo hapa,
  • Mwenyekiti wa Mtandao wa Mashirika ya Wazee,
  • Wazee wangu toka Mikoa Mbalimbali
  • Wanahabari na Wasanii,
  • Kamati ya Maandalizi,
  • Mabibi na Mabwana.

Kwanza kabisa naomba kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na Afya njema na kutuwezesha kuiona siku hii ya leo ambayo ni muhimu sana kwetu sote na hasa kwa wale ambao tumefikia umri wa miaka 60 na kuendelea. Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kufikia umri huo.

Aidha, nawashukuru sanawazee wangu wa Mkoa wa Mwanza kwa kuona inafaa kumwalika Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nimekuja kwa niaba yake kushiriki pamoja nanyi katika maadhimisho haya baada ya Mheshimiwa Rais kuwa na shughuli nyingi muhimu.

Naupongeza uongozi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mheshimiwa Evarist Ndikilo, WHO, TAMISEMI, HelpAge International, Kamati ya maandalizi na wazee wote kwa ujumla kwa kufanikisha maadhimisho haya.

Ninawashukuru kwa namna ya pekee wazee waliotoka mikoa mbalimbali kuja kuungana nasi,   poleni kwa safari.

Ndugu wananchi,

Napenda kuvishukurusanavyombo vya habari, ambavyo vimefanya uhamasishaji kwa siku ya leo, Naamini vyombo hivi vitaendelea kuhamasisha na kutoa elimu kwa jamii ili kuondokana na imani potofu juu ya wazee.

Aidha, sina budi kuwashukurusanawananchi wa Mkoa wa Mwanza, Taasisi mbalimbali, vikundi vya sanaa na burudani, kwa kuacha shughuli zao, ili kuja kujiunga nasi katika siku hii ya Kitaifa ya Wazee Duniani.

Ndugu Wananchi,

Baraza la Umoja wa Mataifa limeweka tarehe 1 Oktoba, ya kila mwaka kuwa ni siku ya wazee duniani, siku hii

inalenga kuhamasisha jamii, katika nchi husika kutambua haki, mahitaji na changamoto zinazowakabili wazee na kutafuta namna ya kukabiliana nazo.

Umoja wa mataifa, ulifikia uamuzi wa kutenga siku ya wazee duniani kwa sababu nyingi, moja ni kutoa nafasi kwa mataifa yote duniani kutafakari hali ya maisha ya wazee na kuangalia mapungufu yaliyopo na kuweka mipango ya kushughulikia kundi hili kwa lengo la kuboresha maisha yao na kuwafanya wazee waishi maisha ya heshima kwa kwapatia mahitaji yao muhimu. Leo Tanzania inaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku hii ya wazee.

Ndugu Wananchi,

Maadhimisho ya siku ya wazee duniani huambatana na ujumbe maalumu kila mwaka kulingana na mahitaji ndani na nje ya nchi. Ujumbe huu ni dira ya maadhimisho haya.

Nimeambiwa kwamba kauli mbiu ya mwaka huu ni “Longevity Shapes the Future” kwa tafsiri iliyofanywa na wazee wenyewe kuwa Maisha Marefu Hujenga Mustakabali wa Taifa Letu. Kauli mbiu hii, inalenga katika kuhamasisha Serikali, jamii, na wadau mbalimbali

kutambua maisha marefu ya wazee kwa kuwajengea mazingira mazuri na kuwahusisha katika shughuli mbali mbali za maendeleo ya uchumi na kijamii, wazee wana uwezo na vipaji mbalimbali, hivyo wazee ni mustakabali wa Taifa letu.

Ndugu Wananchi,

Dhana ya uzee unalezea hatua ya mwisho ya makuzi ya binadamu kuanzia utoto, ujana hadi kufikia uzee. Uzee

unaonesha thamani ya maisha marefu waliyopewa zawadi na mwenyezi Mungu, ni umri uliopitia mengi, una uzoefu mkubwa na upeo mpana kuwafanya wazee wawe hazina kubwa ya ujuzi.

Wazee ni rasilimali na ni hazina kubwa ya ufahamu, busara, ushauri, maarifa na uzoefu wa vitu muhimu kwa

maendeleo.   Kwenye matatizo tunakwenda kwa wazee kupata ushauri na mara nyingi tatizo linakwisha. Kwa busara na heshima zao wazee ni dawa kwa hiyo tujue wazee ni muhimusanakatika maisha yetu na tuendelee

kuwaenzi na tuwatumie kwa kadri itavyowezekana kwa mustakabali wa Taifa letu.

Ndugu Wananchi,

Serikali inatambua umuhimu wa wazee kuwa ni rasilimali na hazina kubwa katika kukuza uchumi wa nchi yetu na kuleta mbadiliko ya kiuchumi na kwamba wazee ndio waliotujengea misingi ya Taifa tuliyonayo leo, walitukomboa kutoka kwa wakoloni, walioweka misingi ya Umoja, Utaifa na Amani tuliyonayo leo hii, walitunza maliasili tulizonazo na wameturithisha utamaduni wetu.

Natoa changamoto kwa vijana kuwa karibu na wazee ili kujifunza maadili mema toka kwao na kuwajibika kuwahudumia ipasavyo na hatimaye kufanya maandalizi ya maisha wanapoelekea uzeeni.

Ndugu wananchi,

Natambua changamoto zinazowakabili wazee wetu, changamoto hizo ni pamoja na pensheni kwa wastaafu na wazee, Huduma za Afya, Msamaha wa kodi ya majengo

kwa nyumba wanazomiliki, Ushirikishwaji, utamaduni na maadili, na mauaji ya wazee.

Serikali kwa nyakati tofauti imebuni Sera na mikakati mbalimbali inayoelekeza jinsi ya kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wazee nchini. Sera ya Taifa ya wazee ya mwaka 2003 ilikuwa waraka wa kwanza wenye mwelekeo thabiti wa kuyashughulikia masuala tete ya wazee. Sera hii ilifuatiwa na mikakati na matamko mbalimbali yanayohusu wazee. Hii inaonesha kuwa Serikali yaTanzaniainatambua umuhimu wa wazee

kamarasilimali na hazina muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu.

Ndugu Wananchi,

Kuhusu pendekezo la matibabu kwa wazee la kuwepo madirisha maalum kwa wazee katika hospitali na vituo vya Afya vya Umma kote nchini pamoja na kuwapata wataalamu wa magonjwa ya uzee, nakubaliana nanyi, naiagiza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kukamilishamchakato wa utoaji wa huduma za Afya kwa wazee mapema iwezekanavyo kote nchini.

Ndugu Wananchi,

Serikali ilipitisha Sera ya Taifa ya Wazee mwaka 2003. Utekelezaji wa Sera hii umekuwa ukikwama kwa sababu ya kutokuwepo na sheria inayosimamia utekelezaji wake. Hivyo mipango mingi inayohusu wazee imeendelea kutegemea zaidi huruma kwa wale wanaojisikia. Kwa kuzingatiahiloSerikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi

wa Jamii imekuwa inashughulikia kufanikisha kuwepo kwa Sheria ya Wazee nchini. Mchakato huo umefikia hatua ya kuandaliwa kwa rasimu na baadaye kuwasilishwa

kwenye Baraza la Mawaziri ili kupata idhini ya kutungwa kwa Sheria ya Wazee. Uanzishwaji wa sheria hii utaboresha maisha na kuondoa vikwazo vya upatikanaji

wa huduma za jamii kwa wazee. Vile vile, Sheria ya Wazee itasaidia huduma za wazee kutambulika kisheria.

 

 

Ndugu Wananchi,

Vitendo viovu vya ukatili yakiwemo mauaji wanayofanyiwa wazee wetu hasa wanawake ni jambo la kusikitishasana, tuendelee kulaani kila tunapopata fursa, viongozi wa Serikali, Mashirika ya Dini na Taasisi za kiraia, wasiache kulisema hili kila wanapopata nafasi na sisi viongozi wa siasa lazima tuendelee kulikemea suala hili. Serikali kwa upande wake itaendelea kuchukua hatua za kupambana na vitendo hivi ili kuvikomesha, nawaomba wananchi kuwataja watu wanaowajua kuwa wanajihusisha na mauaji ya wazee. Nawahakikishia Serikali kwa kutumia vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na kushirikisha

wananchi bado inaendelea na juhudi za kupambana na ukatili wa mauaji ya wazee.

Ndugu Wananchi,

Serikali imeanzisha mchakato wa kuitazama upya Katiba ya Nchi yetu ili hatimaye tuwe na katiba inayoendana na

Taifa letu na mahitaji ya sasa. Wakati mchakato huu wa kuandaa katiba mpya unapoendelea katika mikoa yote nchini hatuna budi kukubali na kutambua kuwa katiba yetu ya sasa tuliyoachiwa na waasisi wa Taifa letu, imeifanyia nchi yetu mambo mazuri na kuifikisha hapa tulipo. Hivyo, nawaomba wazee wangu mshiriki katika mchakato wa kutoa maoni ili masuala ya wazee yaboreshwe na kuingizwa katika Katiba Mpya.

Ndugu wananchi,

Natambua kazi zinazofanywa na taasisi zisizo za kiserikali. Taasisi hizi ni muhimu kwa kuwa zinachangia katika jitihada za Serikali za kutoa huduma kwa wazee. Hata

hivyo, suala la kutotosheleza huduma na mahitaji ya wazee inatokana na uwezo mdogo wa Serikali kifedha na majukumu yanayohusiana na huduma katika sekta mbalimbali. Hivyo, nasisitiza kiasi cha fedha kinachotolewa na Serikali kitumiwe kulingana na vipaumbele vilivyopangwa. Suala la uzee ni mtambuka. Hivyo nachukua nafasi hii kutoa wito kwa watendaji wote

kwa nafasi zao mbalimbali hususan Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Miji/Manispaa/Wilaya na Asasi mbalimbali za Serikali na za watu binafsi zinazotoa

huduma kwa wazee kuweka mipango na kuimarisha mifumo ya kinga ya jamii iliyopo ili kuboresha huduma wanazopata.

Ndugu Wananchi,

Nawashukurusanawazee wangu kwa risala nzuri mliposoma ikiwa ni salaam za wazee kwa serikaliyao.

Nakiri kuwa maombi na mapendekezo yaliyosemwa ni ya msingi, na muhimu kwa mustakabali wa maisha ya wazee. Baadhi nimejaribu kuyajibu katika hotuba yangu, na mengine utekelezaji wake utachukuwa muda mrefu kulingana na hali halisi ya Serikali. Mengi ya mapendekezo yaliyoelezwa yatakamilika baada ya Sheria ya wazee kutungwa. Naahidi yote yatafanyiwa kazi na serikali yenu.

Baada ya kusema hayo napenda niwashukuru tena kwa kumwalika Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano

waTanzaniaMhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Mgeni Rasmi. Ni watakie safari njema mtakapokuwa mnarudi, na ninawashukurusanakwa kujitokeza kuhudhuria maadhimisho haya ya Kitaifa.

Nawatakia maadhimisho mema.

Ahsanteni kwa kunisikiliza!

 

VIBWAGIZO SIKU YA WAZEE DUNIANI

(1)                  HUDUMA BORA KWA WAZEE

(2)                  MATUNZO KWA WAZEE

(3)                  PENSHENI KWA WAZEE

(4)                  WAZEE WASHIRIKISHWE KATIKA NYANJA ZOTE

(5)                  MABARAZA YA WAZEE YAUNDWE

(6)                  MATIBABU BURE KWA WAZEE

 

 

2 Novemba, 2012
« Iliyotangulia Ifuatayo »

Ongeza maoni

Jina lako:
Mahali ulipo:
Email yako:
(sio lazima)
Anwani yako ya email haitachapishwa.