Na Godwin Msalichuma,
Newala, Mtwara
Septemba 29, 2011
JAMII katika Wilaya ya Newala wametakiwa kuanzisha madarasa ya elimu ya watu wazima ili kuondokana na tatizo la ujinga na umaskini uliokothiri haswa kipindi hiki Tanzania inavyoadhimisha miaka hamsini ya uhuru.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Bw. Chitwanga Ndembo katika maadhimisho ya juma la elimu ya watu wazima yaliyofanyika kiwilaya katika kijiji cha Mkunya ambayo yaliandaliwa na asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Umoja wa maendeleo ya elimu Newala (NEDA).
“ Wananchi mliyekuja hapa ni mabalozi wa wengine ambao hawakuja ninaagiza kuwa anzisheni madarasa ya elimu ya watu wazima katika maeneo yenu mnayoishi na hiyo ndiyo ujumbe wetu katika kipindi hiki cha maadhimisho ya miaka hamsini ya uhuru wa taifa letu…….anzisheni na hamasisheni watu wajiunge na kunufaika na madarasa hayo” alisema Bw. Ndembo.
Alisema kuwa jamii inapaswa kuelimika zaidi kipindi hiki kwani hata Halmashauri yake imeshajipanga kuanzisha Benki ya maendeleo ya watu wa Newala hivyo basi kunahitajika wananchi angalau walioelimika ili wafungue ankaunti pamoja na kuwa na hisa katika taasisi hiyo ya fedha itakayofunguliwa.
Aidha aliwaomba jamii hiyo kuchangamkia masuala ya elimu ya watu wazima kwani kutawafanya wajue umuhimu wa elimu na kuhamasika kuchangia maendeleo ya elimu ya watoto wao kama vile nyumba za walimu, madarasa na madawati.
“ Mzazi unapoelimika inakusaidia hata wewe mwenyewe kuwa makini katika kuchangia elimu ya watoto ulionao……isitoshe hata masuala ya ukulima wa kisasa wa zao letu kuu la korosho litazingatiwa hivyo kupata mazao bora na kipato cha kutosha kuendeleza afya na elimu ya familia yako” alisema Mwenyekiti huyo.
Comments (1)