Wamiliki wa viwanda Tanzania waokoeni wakulima.
WAKATI wa uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Tanzania ilikuwa nchi ya Wakulima na Wafanyakazi. Katika kipindi hicho, wafanyakazi walikuwa ngangari hali kadhalika wakulima walikuwa wanaringa kutokana na kufaidi jasho lao.
Kipindi cha mwalimu, mambo yote yalikuwa hadharani, kwani wakulima kutoka kila mkoa, wilaya, tarafa, kata na vijijini walitekeleza wajibu wao kwa uhakika.
Ama kwa hakika wakazi wa Kilimanjaro, Mbeya na Kagera walikuwa wakulima wa ukweli wa kahawa, wakati wale wa Mtwara, Pwani na Lindi walijikita kwenye korosho. Kwa ujumla kila mahali wakulima walitekeleza wajibu wao.
Sintawasahau wakulima wa mahindi wa Ismani huko Iringa wakishindana na wale wa Ruvuma na Rukwa wakati mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Mara wakulima wakijikita katika kilimo cha pamba huku Arusha hususan Mbulu ikiwa na ngano ama shayiri..
Kila mkoa kulikuwa na wakulima hodari i na Wafanyakazi walikuwa wakitekeleza majukumu yao kwenye ofisi, viwanda na mashirika mbalimbali ya umma bila uvivu.
Enzi za Mwalimu wafanyakazi walikuwa wa ukweli, kwani walitekeleza majukumu yao barabara chini ya mwamvuli wa Chama cha Wafanyakazi cha Nuta baadaye Ottu.
Tanzania ya enzi za Nyerere ilikuwa nchi yenye mipango iliyopangwa na kupangika, ingawa huruma ya sera ya ujamaa ambayo haikuweka sheria ya kumdhibiti kikamilifu anayeharibu mali ya umma. Udhaifu wa kutokuwapo kwa sheria ulisababisha viwanda, mashirika ya umma kutafunwa na wajamaa na kufa ‘kifo cha mende’.
Pamoja na wafanyakazi kuendelea kuwapo, wakiwa katika vipande vipande chini ya Shirikisho la vyama vya wafanyakazi (Tucta),
Baada ya Nyerere kufariki dunia, mambo mengi yameharibiika, mfumo wa kilimo nchini.
Wakulima wa Tanzania ya sasa hawana baba wala mama. Ni wakulima wanaohangaika. Wengi wanalima wakidhani mfumo wa mwalimu wa Serikali kununua mazao bado upo, lakini wengine wameacha kulima baada ya kuelewa kwamba Serikali hainunui mazao.
Wakulima wengine wanalima kwa imani ile ile ya kwamba wao ni wakulima , hivyo watauza watakapowaona wanunuzi, wasipoonekana wataendelea kubaki na chakula chao.
Wanunuzi wa mazao ya chakula hasa mahindi na mchele wanaonekana kwa vipindi wakitokea nchi za jirani, wakati wa mazao ya pamba, tumbaku, katani, na kahawa.
Kwa hali hiyo Tanzania ya sasa haina zao lolote la kujivunia kwa uhakika kwamba linalimwa vizuri na wakulima wake wakafaidika.
Kutokana na ukweli huu, ni nani atakayewakomboa wakulima ili waanze kulima kwa malengo. Ni nani atawarudisha wakulima kwenye mstari wa kupenda kilimo cha pamba, korosho, karanga, mtama, uwele na michikichi?
Bila shaka Wazalendo wacha Mungu wenye viwanda vya kusaga unga wa mahindi ama ngano, kubangua korosho, viwanda vya kuchambua pamba na kusindika mafuta ya kula wana nafasi ya kusaidia kuboresha sekta ya kilimo.
Wenye viwanda hivyo wanaweza kuwasaidia wakulima kama wataamua kununua mazao ya Watanzania badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi.
Wamiliki wa viwanda hivyo wamekuwa wakinunua ngano, mahindi, shayiri, na mafuta ghafi ya kula kutoka nchi za nje zikiwamo Japani, Korea na China.
Ni fedheha kwa wenye viwanda kuagiza mahindi nje ya nchi, wakati wanaweza kuwahamasisha na kuwahakikishia Watanzania walime mahindi mengi ili wayanunue.