MAAJABU YA MKOMAMANGA KATIKA TBA
Dr. Clifford B. Majani
Mkomamanga (Punica granatum)ni mmea ambao asili yake ni katika nchi za Mashariki ya Kati (Middle East) na umetajwa sana katika vitabu vya kale vya historia ya eneo hilo. Kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili Sanifu iliyoandikwa na Taasisi ya Utafiti wa Kiswahili (Institute of Kiswahili Research) ya Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam-Tanzania, mkomamanga ni mti unaozaa matunda ambayo maganda yake huchemshwa na kufanywa dawa ya kufunga kuhara (TUKI, 1981). Hii inaonyesha kuwa wenyeji wa Upwa wa Afrika Mashariki wamekuwa na uzoefu wa kutosha kuhusiana na uwezo wa tiba wa mmea wa mkomamanga kwa muda mrefu hasa ikizingatiwa kuwa wamekuwa na mfungamano wa kihistoria na wageni toka Mashariki ya Kati kwa kipindi kirefu.
Mkomamanga una dawa mbalimbali kama vile Tannis (punicalin na punicalagin), Flavonoids, Alkaloids, Steroids, Triterpenes na Polyphenols. Dawa hizi hupatikana katika magome, majani, mbegu, maganda ya matunda, juisi ya matunda na katika maua ya mkomamanga. Tunda la komamanga pia lina vitamini C na E kwa wingi pamoaja na madini ya potassium na copper.
Faida za kitabibu za mmea-dawa huu
Katika majaribio ya kisayansi imethibitika kuwa juisi ya komamanga na fukuto ya mmea huu husaidia kudhibiti kasi ya kuzaliana kwa virusi vya UKIMWI namba 1 [HIV-1]. Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Neurath A. R pamoja na wenzake na kupewa kichwa kisemacho “Punica granatum juice provides an HIV-1 inhibitor and candidate tropical microbicide”. Utafiti huu ulichapishwa katika jarida la kisayansi la BMC infectious diseases (4) 41-45(2004). Matokeo yanayofanana na hayo pia yalithibitika katika utafiti mwingine uliofanywa na Kun Silprasit na wenzake mnamo mwaka wa 2011 na kupewa jina la “Anti-HIV-1 Reverse transcriptase activities of hexane extracts from Asian Medicinal Plants”. Utafiti huo ulichapishwa katika jarida la kisayansi la “Journal of Medical Plant Research Vol. 5 (17), pp. 4194-4201, 9 Sept 2011”.
Dawa zinazopatikana katika maganda na majani ya mkomamanga husaidia katika matibabu ya hali ya tumbo kujaa gesi na kudhibiti tindikali (acid) tumboni. Mkomamanga pia husaidia katika matibabu ya kuhara damu na kutibu uambukizo katika kibofu cha mkojo (Cycititis).
Lojo ya mbegu za matunda ya komamanga ikichanganywa na maziwa, husaidia katika tiba ya kuondosha mawe katika figo. Fukuto ya Mkomamaga husaidia katika tiba ya minyoo aina ya tegu (Tapeworms) lakini pia husaidia katika matibabu ya uvimbe wa wengu (Spleen). Dawa-lishe hii pia husaidia kwa kiwango kikubwa katika uponaji wa vidonda vya tumbo.
Katika jaribio moja lililofanywa kwa wanyama, dawa hii ilionyesha uwezo mkubwa sana (97.4%) wa kuponya vidonda vya tumbo. Kazi hii hutokana na uwezo wa dawa hii wa kudhibiti bakteria aina ya Helicobacter pylori ambao kwa kiasi kikubwa huchangia kutokea kwa vidonda vya tumbo (70 -80% ya vidonda vya mfuko wa chakula na 90% ya vidonda katika utumbo). Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Hu W. na wenzake mnamo mwaka 2006 na kupewa kichwa kisemacho “Study of in-vitro inhibition effect of Pomegranate rind on H.pylori”. Utafiti huu ulichapishwa katika jarida la Academic Journal of Kunming Medical College 27, 25-27.
Utafiti mwingine uliofanywa na H.R. Rahimi na wenzake mnamo mwaka 2011 ujulikanao kwa jina la “Punica granatum is more effective to prevent Gastric Disorders Induced by Helicobacter pylori or any other stimulator in humans” uliochapishwa katika jarida la kitabibu la Asian J. of Plant Sciences 10 (7): 380-382, 2011; pia ulithibitisha uwezo wa mkomamanga katika tiba ya vidonda vya tumbo. Lakini pia uwezo wa dawa hii wa kupunguza uzalishaji wa tindikali tumboni, huchangia katika uponaji wa haraka wa vidonda vya tumbo.
Katika mfumo wa damu, komamanda hutoa msaada mkubwa wa kuzuia na kutibu magonjwa yanayoshambulia mfumo huo nyeti. Komamanga ni dawa nzuri ya kuzuia na kutibu shinikizo la damu, magonjwa ya nyama za moyo, kiharusi (Cerebrovascular Accident) na magonjwa ya mishipa ya damu. Komamanga lina madini aina ya potassium na copper kwa wingi, pamoja na faida zingine mwilini, madini haya husaidia kusharabiwa (kufyonzwa) kwa madini ya chuma kutoka katika utumbo kwenda mwilini kwa urahisi na hii husaidia katika matibabu na kinga ya tatizo la upungufu wa damu mwilini.
Komamanga pia ni mahili katika tiba na kuzuia magonjwa ya kusendeka (magonjwa ya muda mrefu) kama vile saratani ya tezi ya prosteti ya wanaume, saratani mbalimbali, kisukari, baridi yabisi na uvimbe wa maungio ya vidole (gout). Komamanga husaidia mwili kuondosha sumu na uchafu utokanao na kemikali na mabaki ya vyakula mwilini kama vile asidi ya uriki (uric acid). Sumu hizi ni chanzo kikuu cha magonjwa mengi ya kusendeka.
Komamanga pia husaidia katika jitihada za kukabiliana na tatizo la unene wa kupindukia (Obesity). Husaidia katika matibabu ya tatizo la ini pale linapolemewa (Liver congestion). Dawa ndani ya komamanga licha ya kuwa na uwezo wa kudhibiti aina kadha wa kadha za bakteria wanaosababisha magonjwa mwilini, pia zina uwezo wa kukabiliana na virusi wa aina mbalimbali wanaosababisha magonjwa kwa binadamu.
Kwa mujibu wa wasomi na wanazuoni wenye shahada za uzamivu, Dk. Navindra Seeram na Dk. Risa Schulman, komamanga kwa hakika ni dawa asilia inayotamba katika tiba za kisasa (Modern Medicine) kwenye karne ya 21.
Kipimo
Dawa-lishe hii hutumiwa kwa kunywa fukuto inayotokana na sehemu za mmea kiasi cha gram 3 hadi 9 kwa siku inatosha kwa ajili ya tiba ya magonjwa mbalimbali. Kwa ajili ya minyoo ya tegu magome au mizizi ya mkomamanga kiasi cha gram 50 huchemshwa katika lita 1 ya maji ili kupata fukuto.
Juisi ya matunda yake pia inaweza kutumiwa kiasi cha bilauli moja kila siku ili kukinga magonjwa mbalimbali. Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali dawa hii ni salama kama itatumiwa kulingana na kipimo sahihi. Tahadhari ichukuliwe kuhusu matumizi ya dawa hii kwa wanawake wajawazito na kwa watoto chini ya umri wa miaka 12 kwani hakuna taarifa za kutosha kuhusiana na usalama katika makundi haya.
Madhara yanayoweza kutokea kwa kutumia dawa-lishe hii (Adverse reactions)
Matumizi ya kipimo kikubwa cha dawa hii ikiwa katika hali yake ya asili (zaidi ya gram 80) kinaweza kusababisha kizunguzungu, maumivu makali ya kichwa, kushindwa kufumbua macho, kutapika, kuzimia na wakati mwingine inaweza kusababisha kifo. Dawa hii pia inaweza kusababisha mwili kunyong’onyea, kutokuona vizuri, kushitukashituka kwa misuli na kutetemeka kwa mikono kama mlevi (tremors).
Onyo: Ni vizuri kuepuka matumizi holera ya dawa hata kama ni dawa za asili. Si kila dawa ya asili ni salama kama itatumiwa bila kufuata ushauri wa mtaalamu aliyesoma na kuelewa vizuri sayansi ya tiba asilia na lishe. Mimea ina kemikali za asili hivyo inapotumiwa ni lazima tahadhari zichukuliwe kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza.Kumbuka mimea ni dawa.
Rejea
- · Ajaikumar KB et al (2005): The inhibition of gastric mucosal injury by punica granatum L. methanolic extract. Journal of Ethnopharmacology 96; 171-176.
- · Bensky D, Gamble A (1993). Chinese herbal medicine Materia medica, revised ed. Seattle, Washington, Eastland Press.
- · Das, AK, Mandal, SC.; Banerjee, SK.; Sinha, S.; Das, J.; Saha, BP. & Pal, M. (1999). Studies on antidiarrhoeal activity of Punica granatum seed extract in rats. Journal of ethnopharmacology, Vol.68, No.1-3 (December 1999), pp. 205-208. ISSN 0378-8741
- · H.R. Rahimi, M. Arastoo and M.Shiri (2011): Punica granatum is more effective to prevent Gastric Disorders Induced by Helicobacter pylori or any other stimulator in humans. Asian J. of Plant Sciences 10 (7): 380-382, 2011.
- · Hu W, Dai W, Yang YM, Zhou ZF, Li XY, and Duan LP (2006): Study of in-vitro inhibition effect of Pomegranate rind on H.pylori. Academic Journal of Kunming Medical College 27, 25-27.
- · J.C. Kurian: Herbal Help for Organs, Autumn House Publications (Europe) Ltd, 2013.
- · Kun Silprasit et al. Anti-HIV-1 Reverse transcriptase activities of hexane extracts from Asian Medicinal Plants. Journal of Medical Plant Research Vol. 5 (17), pp. 4194-4201, 9 Sept 2011.
- · Lansky EP, Newman RA et al. (2007): Punica granatum (Pomegranate) and its potential for prevention and treatment of inflammation and cancer. Journal of Ethnopharmacology 109, 177-206.
- · Li DG, Zhang ZM and Chen XJ (2003): Study on the influence of aqueous extract of leaves of Punica granatum on the secretion of gastric acids and experimental gastric ulcer. Chinise Journal of Preventive Medicine 19, 23-24.
- · Medicinal plants in China. Manila, World Health Organization Regional Office for the Western Pacific, 1989 (WHO Regional Publications, Western Pacific Series, No. 2).
- · Neurath AR et al.,(2004): Punica granatum juice provides an HIV-1 inhibitor and candidate tropical microbicide. BMC infectious diseases, 4, 41-45.
- · Nutritional Informational Services (2008): Beneficial compounds in Pomegranate guards against major health threats. Natural Wellness Vol.8, Report #3.
- · Pharmacopoeia of the People’s Republic of China. Vol. I (English edition). Beijing, Chemical Industry Press, 2005.
- · Rufeng Wang et al. Pomegranate: Constituents, Bioactivities and Pharmacokinetics. Fruit, vegetable and cerial science and biotechnology 4 (special issue 2), 77-87, 2010 Global Science Books.
- · Seeram NP, Schulman RN, Heber D (Eds): Pomegranate: Ancient Roots to Modern Medicine. Boca Raton, FL: CRC Press & Taylor and Francis Group, 2006.
- · Seeram NP: Impact of Pomegranate juice on human health and diseases. Worldnutra 2006, Nutritional Outlook, 10 (6): 235-7, July/August 2007.
- · Shalini H Kumar and Pushpa A: Pomegranate – an Insight into its Antioxidative, Thrombolytic and Membrane Stabilizing Property, Journal of Natural Sciences Research ISSN 2224-3186 (Paper) ISSN 2225-0921 (Online) Vol.2, No.10, 2012.
- · TUKI: Mkomamanga. Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Oxford University Press, Dar-es-Salaam (1981) uk. 174.
MAARIFA YA WENYEJI NA TEKNOLOJIA YA WAAFRIKA INAVYOWEZA KULETA MAGEUZI YA KIUCHUMI NA MAENDELEO.
Bidhaa pekee katika soko huria iliyo na ushindani wa kweli ni ile inayotokana na ubunifu. Wenyeji wa Afrika wanaweza kupambana na umaskini wao wenyewe bila kutegemea misaada toka nje ya bara hili. Bara la Afrika lina malighafi nyingi, elimu, ujuzi, sayansi na teknolojia ambazo zikitumiwa kwa ufanisi, zinaweza kabisa kuleta mageuzi ya kiuchumi, kiafya na kibiashara.
Ras Mongo wa Jijini Mbeya ambaye ni mjuzi na mwenye elimu kubwa katika teknolojia na sayansi za asili ya Afrika, anathibitisha kuwa waafrika wanaweza kujikomboa kutokana na ubunifu.Ras Mongo anatengeneza na kuuza bidhaa rafiki kwa mazingira na afya ya watumiaji. Anatengeneza viatu, mapambo, viti vya kifahari na vyombo imara vya nyumbani vitokanavyo na malighafi za asili zinazopatikana kwa urahisi barani Afrika.
Vyombo vingi vya plastiki na mabati ya aluminiamu vimekuwa vikilaumiwa na wataalamu wa afya ya jamii kuwa vinaweza kusababisha kansa na magonjwa ya ini. Kutumia vyombo vya asili vitokanavyo na miti pamoja na udongo ni salama kwa afya na ni rafiki kwa mazingira, vinadumu na pia ni rafiki wa uchumi na mfuko wako. 'Africans stop being poor' anasema Ras Mongo anayepatikana eneo la Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya au kwa kumpigia simu namba 0767 589 665. Hapa chini ni baadhi ya kazi za Ras Mongo, msomi mwenye elimu, ujuzi na teknolojia za asili ya Afrika.
ZABIBU (Vitis vinifera L.)NA FAIDA ZA TIBA
Zabibu ni matunda yenye madini (kalishiamu, potashiamu na magnesiumu), sukari, vitamin na dawa-lishe kwa wingi.
Divai au Mvinyo Usiochacha
Maji ya matunda ya zabibu (juisi ya zabibu) hujulikana kama divai au mvinyo. Maneno haya ya Kiswahili yanatokana na tafsiri ya neno la Kiingereza ‘Wine’ lakini pia neno hili la Kiingereza limetoholewa kutoka katika maneno ya Kiebrania ‘Yayin’ au ‘Tirosh’ na maneno ya Kigriki ‘Oinos’au ‘Gleukos’. Maneno haya ya lugha za kale yalitumika kumaanisha maji ya matunda ya zabibu yasiyochacha, yaani divai au mvinyo mpya upatikanao katika vichala (new wine) na divai ya namna hii hapo zamani, ilitambuliwa kama kinywaji kitamu chenye baraka (Isaya 65:8; Mika 6:15) na ilitumiwa kwa kiasi kama dawa nzuri ya matatizo ya tumbo (1 Timotheo 5:23).
Maji ya matunda ya zabibu yaliyochacha na kuzalisha alkoholi (mvinyo uliochacha), maji ya matunda mengine yaliyochacha na vinywaji vingine vyenye alikoholi (ethyl alcohol) vilivyotengenezwa baada ya kuchachusha nafaka, vilijulikana kama ‘Shekar’ katika lugha ya Kiebrania. Ingawa wakati mwingine watu walimaanisha mvinyo au divai kama kinywaji kilichochacha kwa kutumia maneno ya Yayin na Tirosh (Hosea 4:11; Mwanzo 9:20-21), vinywaji vilivyochacha vilitambuliwa kama vinywaji vyenye madhara kwa afya na vilifananishwa na sumu ya nyoka (Mithali 23:31-35). Hii ni kutokana na ukweli wa kisayansi kuwa ethyl alcohol ina uwezo wa kudhuru seli za mwili na kuharibu afya ya ini, moyo, akili na mwili kwa ujumla. Pamoja na ukweli huu kuhusu madhara ya kiafya yaliyotokana na kunywa vinywaji vyenye alkoholi, mvinyo uliochacha hapo zamani ulitumika kama dawa ya kusafishia au kutibu vidonda na majeraha (Luka 10: 30-34). Hii ilitokana na uwezo wa alkoholi (pombe) wa kuuwa bakteria hatari wanaoshambulia vidonda na kusababisha usaha.
Maji ya matunda ya zabubu ambayo hayajachacha (divai au mvinyo mpya) hasa yale yanayotokana na matunda ya zabibu nyekundu, licha ya kuwa kinywaji kizuri kwa ajili ya kuimarisha afya pia ni dawa nzuri. Divai hii ina sukari ya asili inayotia nguvu katika nyama za mwili, lakini pia ina vitamin B za aina mbalimbali ambazo huimarisha afya ya neva. Divai pia ina dawa-lishe aina ya quercetin (Flavonoid), resveratrol na dawa-lishe za aina nyingine nyingi ambazo hufanya kazi za kutibu mwili.
Mvinyo uliochacha
Mvinyo uliochacha (fermented wine) ambao unatokana na zabibu nyekundu pia haupotezi dawa-lishe zinazosaidia kuleta afya ya tumbo na mishipa ya damu kwenye moyo kwa wazee wenye umri wa kuanzia miaka 50 na kuendelea. Tafiti mbalimbali huonyesha kuwa wazee wanapokunywa kiasi cha mililita 100 hadi 200 za mvinyo mwekundu kwa siku, hupunguza uwezekano wa kupata shambulio la moyo (myocardial infarction risk) kwa takribani asilimia 30 hadi 50. Dawa lishe katika mvinyo huu, hutokana na maganda ya zabibu wakati wa kukamua zabibu kabla haijachachushwa. Lakini ethyl alcohol iliyomo ndani ya mvinyo uliochacha (pombe) inadhuru seli za mwili na kusababisha matatizo ya kiafya na haina faida yoyote mwilini.
Faida za kiafya
· Zabibu huupatia mwili nguvu na kuimarisha afya ya mishipa ya damu hasa ile inayosambaza damu kwenye nyama za moyo. Zabibu ni dawa nzuri kwa magonjwa mbalimbali ya moyo. Huimarisha afya ya mishipa ya damu na kuzuia ugonjwa wa kukakamaa kwa mishipa hiyo.
· Husaidia damu kuwa nyepesi na kuzuia isigande ndani ya mishipa ya damu na kwa sababu hii zabibu hupunguza hatari ya kupata ugonjwa wa kiharusi (Cerebrovascular accident) au stroke.
· Zabibu pia inasaidia kuzuia na kutibu tatizo la upungufu wa damu mwilini.
· Kutumia zabibu mara kwa mara huzuia na kutibu ugonjwa wa bawasili (haemorrhoeids)
· Husaidia katika tiba na kinga ya magonjwa ya ini kwa vile huongeza uwezo wa ini wa kuondosha sumu mwilini na kuzalisha nyongo kwa wingi.
· Huimarisha afya ya figo na uwezo wake wa kuondosha sumu ndani ya damu.
· Husaidia katika matibabu ya ugonjwa unaosababisha uvimbejoto wa maungio (Arthritis) na baridi yabisi.
· Kutokana na sukari yake ya asili, zabibu hupunguza uchovu wa mwili na kutibu maumivu yasiyokuwa na sababu bayana (Psychosomatic disorders).
· Husaidia katika matibabu ya shinikizo la damu (hypertension).
· Juisi ya zabibu (Divai) husaidia tumbo na utumbo kufanya kazi vizuri na kuzuia ukavu wa kinyesi (chronic constipation). Lakini pia divai huimarisha afya ya mishipa ya damu katika mfumo wa kumeng’enya, kusaga na kusharabu chakula na viinilishe. Huondosha sumu ndani ya ini na kuongeza uzalishaji wa nyongo inayosaidia kuyeyusha chakula chenye mafuta mengi kinachoingia tumboni. Divai pia husaidia bakteria rafiki kwa binadamu wanaoishi ndani ya tumbo (normal flora) kustawi vizuri na kusaidia umeng’enyaji wa chakula katika utumbo kuwa rahisi. Madini yaliyomo ndani ya zabibu, pia huifanya divai kuwa dawa nzuri inayopunguza maumivu ya tumbo yanayotokana na kujiminyaminya kwa misuli ya kuta za matumbo (antispasmodic effect).
Matumizi
· Tumia (kula) kila siku vidonge (punje) vya zabibu visivyopungua vitano kwa ajili ya afya ya mfumo wa damu na nyama za moyo.
· Kunya juisi ya zabibu (mvinyo usiochach au divai mpya) kila siku bilauli mbili, moja asubuhi moja jioni. Hakuna sababu ya kunywa mvinyo uliochacha pale unapopata faida za kiafya kutoka katika mvunyo usiochacha.
Rejea
- American Heart Association,Inc : Alcohol, wine and cardiovascular diseases(2010) retrieved 3.5.2010 at www.americanheart.org/presenter.jhtml
- Constant, J: Alcohol, ischaemic heart disease and the French Paradox. Clin. Cardiol., 20:420-424 (1997).
- George D. Pamplona-Roger: Encyclopedia of Foods and Their Healing Power Vol. 1, Editorial Safeliz, Madrid, (2008). Pp 362 -381.
- Kaye Middleton Fillmore, et al: Moderate alcohol use and reduced mortality risk: Systematic error in prospective studies. Addiction Research and Theory, vol.14 (2):101-132, April 2006.
- Peatfield R.C: Relationship between foods, wine and beer-precipitated migrainous headache. Headache 35: 355-357(1995).
- William Patton: Bible Wines; Kessinger Publishing, LLC (2003).
ZIJUE FAIDA ZA MTOPETOPE
i. Miti huu huweza kupandwa na kustawi sehemu kubwa ya nchi yetu
ii. Uvunaji na matumizi ya majani ni wa gharama nafuu, rahisi na pia ni rafiki wa mazingira
iii. Ina uwezo wa kuua viluilui vya mbu wasambazao ugonjwa wa malaria, matende, mabusha na homa ya manjano kwa wingi na kwa muda mfupi
LISHE DUNI, AFYA DHAIFU NA UMASKINI
Ingawa Tanzania imepiga hatua katika nyanja mbalimbali za afya, bado hali ya lishe si nzuri. 42% ya watoto wa Tanzania walio chini ya umri wa miaka mitano wanakabiliwa na udumavu, hii ni hali mbaya kwa mjibu wa Shirika la Afya Dunian (WHO) ambalo linautazama udumavu katika nchi kuwa ni wakutisha pale unapozidi 40%.1/3 ya watoto wenye umri kati ya miezi 6 na 59 wana upungufu wa madini chuma na vitamini A. Takribani 1/3 ya wasichana na wanawake wenye umri kati ya miaka 15 na 49 wana upungufu wa madini ya chuma, madini joto na vitamini A na 2/5 wana upungufu wa damu na 1/10 ya wanawake wana lishe duni kwa ujumla.
Hali duni ya lishe katika Tanzania, huchangia kutokea kwa vifo 130 vya watoto kila siku. Chanzo cha vifo ni upungufu wa kinga ya mwili ya kujikinga na magonjwa mbalimbali kwa sababu ya lishe duni. Watoto wanaonusurika kifo, hukabiliwa na uduni wa akili na kushindwa kumudu masomo shuleni. Uwezo wa kiakili hushuka kwa kiwango cha 13.5 IQ na watu wazima wenye lishe duni hushindwa kufikiri sawasawa na hawawezi kufanya kazi kwa ufanisi. Hali hii huongeza tatizo la umaskini nchini.
Ingawa tatizo linaweza kuwa upatikanaji wa chakula cha kutosha, bado mikoa yenye chakula cha kutosha kama Iringa, Mbeya na Rukwa inakabiliwa na tatizo la lishe duni miongoni mwa jamii. Hii inaonyesha kuwa kuna tatizo la kutokuelewa jinsi ya kutumia vyakula kwa manufaa au kutokujua vipaumbele vya maisha.Wakati hayo yote yakitokea, wanawake wengi hununua nywele bandia na vipodozi vya gharama vinavyo dhuru afya na akina baba hutumia pesa katika ulevi, anasa na kununua vyakula visivyokuwa na lishe kama vile vinywaji baridi vya viwandani.
Lishe duni ni tatizo linalozuilika na kwa kutambua hivyo sisi (MANSHEP) tumeamua kuunga mkono jitihada za serikali za kupambana na tatizo hili. Pia tunaunga mkono jitihada za wadau wengine kama vile Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN), www.gainhealth.org na Flour Fortification Initiative(FFI), www.ffinetwork.org katika kuboresha lishe ya jamii.
Tunatoa mafunzo ya kuandaa unga wa lishe na huduma ya kusambaza unga wa lishe kwa ajili ya lishe ya jamii. Tushirikiane, Tanzania bila lishe duni inawezekana
Chanzo: UNICEF-Nutrition Overview(www.unicef.org/10787_11047. htm).
Relaxer na Afya ya Msichana/Mwanamke.
Relaxer ni dawa ya nywele inayofanya nywele za mtu mwenye ngozi nyeusi wa asili ya Afrika zilainike na kunyooka kama nywele za wazungu. Watu wengi hasa wanawake wanapenda kutumia relaxer ili nywele zao ziwe na mwonekano tofauti. Kihistoria matumizi ya relaxer yalianza kama matokeo ya watu weusi kubaguliwa. Watu weusi walipoona hivyo waliamua kuiga maisha ya kizungu ili kufanana fanana na wazungu kwa rangi ya ngozi na nywele ili wathaminiwe na kupewa upendeleo wa kupata fursa za mafanikio na watawala wetu enzi za ukoloni. Wakoloni waliwapendelea watu walioipokea kasumba hii kwa mikono miwili.
Siyo lengo langu kuingia kwa undani katika historia, ila ninajaribu kukupa picha ya chimbuko la matumizi ya kitumwa ya dawa zinazodhuru afya ya watu weusi kwa kiwango kikubwa. Pia kupitia mada hii najaribu kukupa uelewa ili unapofanya uchaguzi wa kutumia au kuacha, uchaguzi wako ujengwe katika uelewa sahihi na siyo katika mkumbo au msukumo wa kijamii unaowaona watu wasiotumia dawa hizi kama washamba.
Sayansi inaonyesha kuwa matumizi ya relaxer za nywele yanaweza kusababisha au kuongeza hatari ya kupata magonjwa ya moyo, kupungua kwa uwezo wa kiakili katika kufikiri na kupambanua mambo, kuungua kwa ngozi ya kichwa na muwasho wa ngozi. Matatizo mengine ni saratani ya matiti, mabonge katika mji wa mimba (Leiomyomata), upungufu wa kinga ya mwili na kubalehe mapema kwa wasichana. Katika utafiti uliofanywa na wanasayansi Lauren A. Wise na wenzake (Wise et al, 2012) na kuchapishwa katika jarida la American Journal of Epidemiology ilibainika kuwa matumizi ya relaxer yanaongeza hatari ya kupata mabonge katika mfuko wa kizazi.
Mabonge yanaweza kusababisha ugumba hasa pale yanapokuwa makubwa na kulazimisha tiba ya upasuaji ya kuondoa kizazi (hysterectomy). Katika jamii za wanawake wanaotumia relaxer kwa kiwango kikubwa, chanzo kikubwa cha upasuaji wa kuondoa mfuko wa uzazi ni mabonge. Inasemekana kuwa katika nchi ya Marekani wanawake weusi wanakabiliwa na tatizo la mabonge mara mbili hadi mara tatu zaidi ya wanawake wengine. Hii inaweza kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na matumizi makubwa ya vipodozi kama relaxer.
Hapa Tanzania utafiti unaonyesha kuwa takribani asilimia 10 ya wasichana na wanawake waliokatika umri wa kuzaa wanakabiliwa na tatizo la Mabonge katika mji wa mimba (Kabala, 2011). Hali ya namna hii pia imeonekana katika utafiti uliofanyika nchini Naigeria, nchi yenye watumiaji wengi wa relaxer katika Afrika (Obiechina et al, 2009)
Viambato vilivyomo ndani ya dawa hii hupenya na kuingia katika mfumo wa damu na kwenda kuvuruga mfumo wa vichocheo vya ujinsia hasa homoni za kike. Relaxer nyingi za nywele zina kiwango kikubwa cha kemikali kama vile lye (Sodium hydroxide au Caustic soda), calcium hydroxide, guanidine carbonate, thioglycolic acid salts na monobutyl phthalate.
Rejea
- Majani, C.B (2013): Afya na Urembo wa Msichana;Lulu publishers.
- Kabala, R.B (2011): Imaging Finding in Infertile Patients who underwent Hysterosalpingoraphy Investigation at Muhimbili National Hospital, Master’s Thesis (MUHAS). Accessed at http://ihi.eprint.org/id/eprint/935
- Obiechina et al (2009):Clinical Pattern and Management Outcome of Uterine Fidroids seen in a Private Specialist Hospital in Southeast Nigeria. Tropical J. of Medical Research, vol 13(1),2009.
- Wise et al (2012): Hair Relaxer Use and Risk of Uterine Leiomyomata in African-American Women, American Journal of Epidemiology (2012) vol. 175(5):432-440.
Kwa habari zaidi bofya na usome hapa: Dawa za nywele zinazosababisha uvimbe wa kizazi kwa wanawake
Elimu ya ujasiriamali ina mchango mkubwa katika uboreshaji wa maisha na afya ya jamii. MANSHEP ikishirikiana na wadau mbalimbali katika mafunzo ya utengenezaji wa Sabuni za usafi wa mikono kwa ajili ya kunawa kabla na baada ya kula au kunawa baada ya kupata huduma za choo. Katika mafunzo haya yaliyofanyika Isanga katika kanisa la S.D.A, Mbeya washiriki walijifunza utengenezaji wa vitu mbalimbali. ELIMU NI UFUNGUO WA MAISHA.
Vipodozi vinavyochubua ngozi na kuleta weupe bandia vinawaweka watumiaji wake katika hatari kubwa ya kupata kansa ya ngozi, ugumba na magonjwa ya figo.
Environmental care is essential for Global Health, think Globally.
Utunzaji wa mazingira yetu ni muhimu kwa afya ya jamii ya watu wanaoishi ulimwenguni. Unapofikiria maisha fikiri kwa mtazamo mpana unaoiangalia dunia nzima kama eneo lako la mafanikio.