HAKIELIMU YAPONGEZWA Na. Davis Makundi
Shirika la HakiElimu limepongezwa kwa kazi nzuri wanayoifanya nchini hasa katika kuboresha Elimu na Demokrasia nchini. Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Asasi ya Marafiki wa Elimu Dodoma (MED) Dk. Sinda Hussein Sinda ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma UDOM wakati akifungua mkutano wa wajumbe wa Bodi hiyo ambayo ni ya kwanza tangu MED kupata usajili rasmi.
Dk. Sinda pichani alisema mara nyingi mashirika yanayofanya kazi na wadau wake hupenda kuwatumia wadau hao kama chambo cha kuwapatia umaarufu kwa ajili ya kujikuza wao lakini kwa HakiElimu imekuwa tofauti kwani hadi hatua za mwisho wa usajili waliendelea kutoa ushirikiano kwa MED hadi usajili ukapatikana. "Ndugu wajumbe, tuna kila sababu ya kuwashukuru HakiElimu kwa jambo hili ambalo sote tunaamini bila wao leo hii MED isingekuwepo" alisema Dk. Sinda.
Naye Mratibu wa MED Bw. Davis Makundi aliwaeleza wajumbe kuwa ushirikiano huo umezidi kuimarika kwani HakiElimu licha ya kukubali jina la "Harakati za Marafiki wa Elimu" litoholewe na MED na kutumika; mwishoni mwa mwezi Aprili, 2012 walituma mkataba wa sh. 1,370,000/= kwake kwa ajili ya kuendesha vipindi 10 vya radio Mkoani Dodoma vitakavyohusiana na Elimu, Demokrasia na masuala ya utawala Bora.
Bodi ya MED inaandaa utaratibu wa kufanya mawasiliano na HakiElimu kwa ajili ya kuwaomba wakubali kuwa wanachama wa heshma katika shirika la MED kwa mujibu wa katiba.
Wakati huo huo wananchi wa kijiji cha Chidachi kilichoko Kata ya Mkonze Manispaa ya Dodoma wamesema wanatamani sana HakiELimu ikubali kuwa Mlezi wa Shule ya Msingi Chidachi ambayo licha ya kuwa ni shule changa, imekuwa na mafankio makubwa kitaaluma siku hadi siku.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Bi. Zuhura Muhoji pichani kulia; alitoa ombi hilo kwa asasi ya MED na kuiomba iwasiliane na HakiElimu katika kufuatilia suala hilo. Wazazi na wanajamii wa Mkonze walieleza kuwa HakiElimu limekuwa ni shirika lisilo la kiserikali lenye mfano wa kuigwa kutokana na shughuli zake kuigusa jamii moja kwa moja tofauti na mashirika mengine ambayo yamekuwa yakifanya kazi kwa hisia za mahitaji ya jamii badala ya kuangalia hali halisi ya matatizo ya jamii husika. Shule ya Chidachi ilianzishwa katika Mpango wa MMEM na kuanza kupokea wanafunzi mwaka 2004. Mahafali ya kwanza ya shule hityo yalifanyika 2006 ambapo ufaulu ulikuwa 100%. Mahafali zilizofuata matokeo yake ni kama yanavyoonekana kwenye mabano; 2007 (91%) 2008 (88.8%) 2009 (86.9%) 2010 (87.5%) na 2011 (100%). Pamoja na mafanikio hayo kwa shule ya Chidachi, shule ina upungufu mkubwa wa madawati, nyumba za Walimu, vitabu vya kiada na ziada pamoja na changamoto ya Maktaba.