Envaya
Parts of this page are in Swahili. Edit translations

CHAVITA YALIA NA KUSAHAULIWA NA SERIKALI.             Na. Barakaelly Mosi

Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) kimesikitishwa na kitendo cha Serikali kuwasahau katika mipango yake na kuwafanya walemavu kuwa omba-omba kutokana na kusahauliwa huko. Hayo yalielezwa na washiriki wa mjadala wa kuangalia changamoto za walemavu wasiosikia (Viziwi) lililoandaliwa na CHAVITA kwa ufadhili wa Jumuia ya Kiraia ya The Foundation for Civil Society.

Washiriki wa mjadala huo walisikitishwa na kitendo cha serikali kushindwa kuajiri wataalam wa lugha ya alama katika taasisi zake muhimu kama Polisi, Mahakamani, Bungeni, Hosipitali, ofisi za Halmashauri na Televisheni ya Taifa ili kurahisisha uwasilishaji wa taarifa kwa walemavu hao bila sababu zozote za msingi. 

Washiriki hao walisema kuwa serikali haina nia ya dhati ya kuwapatia wenye ulemavu wa kusikia haki yao ya msingi ya kuwapatia taarifa kutokana na kuwa wataalam wa lugha ya alama wapo; taasisi zake zinazo fedha za kuweza kuwaajiri lakini hawafanyi hivyo, tatizo ni nini? walihoji.

Aidha walieleza kuwa chama chao kiko tayari kutoa mafunzo kwa watu mbalimbali wenye nia ya kujifunza lugha ya alama ili waweze kurahisisha mawasiliano baina yao miongoni mwa jamii. walitoa rai kwa mashirika, taasisi na vyama mbalimbali vya kiraia kuwa na utaratibu wa kujifunza luhga ya alama ambayo walidai ni rahisi kujifunza na kueleweka kwa urahisi.

******************************************

MARAFIKI WA ELIMU WAJADILI MSWADA WA SHERIA YA UZAZI SALAMA

Na. Davis. Makundi

Wanaharakati wa Elimu kupitia asasi ya Marafiki wa Elimu Dodoma wamepata fursa ya kuijadili rasimu ya Mswada wa sheria ya uzazi salama 2012; na kutoa maoni yao juu ya namna ya kuuboresha mswada huo ambao baadaye utakuwa sheria kamili baada ya kupitishwa na Bunge na kusainiwa na Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wawakilishi wa Club za marafiki wa Elimu kutoka katika shule za Sekondari za Kikuyu ambayo ni ya serikali na shule binafsi ya Jamhuri zote kutoka Manispaa ya Dodoma; walionesha ushiriki wa hali ya juu katika kuchangia mawazo juu ya mswada huo uliofanyika katika ukumbi wa CCT mjini Dodoma.

Mjadala huo ulioandaliwa kwa ushirikiano baina ya mashirika ya CARE International, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) na Shirika la Utepe Mweupe ambapo Mkoani Dodoma mwenyeji wa mashirika hayo ilikuwa asasi ya Marafiki wa Elimu Dodoma (MED).

Washiriki hao walipendekeza kuwa katika mtaala wa elimu liwepo somo la Afya ya Uzazi kwa wanafunzi wa kuanzia angalau darasa la tano na kuendelea hadi katika vyuo ili kuifanya jamii ipate uelewa wa kutosha kuhusiana na suala la uzazi wa mpango na manufaa yake katika jamii na taifa.

Ili kuepuka suala la ndoa za utotoni ambalo licha ya kuwa sasa linapigwa vita na watu mbalimbali huku sheria ikitoa mwanya wa uwepo wa ndoa hizo; washiriki hao walipendekeza muda wa kufunga ndoa uwe angalau miaka 21 muda mambao kwa mtoto wa kike atakuwa angalau amehitimu elimu ya sekondari. 

Majadiliano hayo pia yaliambatana na maswali na majibu kutoka pande zote zilizoshiriki (Wawezeshaji na wanafunzi) ambapo kila upande ulionesha umahiri mkubwa katika kuuliza na kujibu maswali hayo. Katika mjadala huo maswali kuhusiana na sheria ya makosa ya kujamiiana 1999 na maswali yahusianayo na Afya ya uzazi yaliulizwa kwa wingi hali iliyoufanya mjadala huo kutoa nafasi kwa idadi kubwa ya washiriki kuchangia.

Washiriki waliomba serikali, taasisi mbalimbali na asasi zisizo za kiserikali kuwezesha kufanyika kwa mijadala ya aina hiyo mara kwa mara ili kukuza uelewa wa wanafunzi na Club za marafiki wa Elimu ili elimu hiyo iyafikie makundi mbalimbali ya jamii kwa haraka.

Akifunga mjadala huo Meneja wa Miradi kutoka sherika la CARE International Bw. David Lyimo aliwataka washiriki kuimarisha Club zao na kuongea bidii katika masomo ili kuwa mfano katika jamii ndani na nje ya shule kwa kufanya vyema kila wakati katika masomo yao pamoja na tabia zao kwa ujumla.

February 23, 2012
« Previous Next »

Comments (1)

asiago.k (library) said:
sasa ni muda kwa watanzania kuwa makini mara mbili na zaidi ya tulivyokuwa mwanzo, hasa hasa katika kujadili mswada huu maana jambo la msingi la kufahamu ni kwamba muswada ukikubalika na wananchi kisha kupitishwa na Bunge la Jamuuri ya Muungano ya Tanzania na kusainiwa na rais wa nchi, basi uwa SHERIA kamili itumikayo ndani ya eneo au nchi husika katika jambo husika, na linapofanikiwa ilo basi SHERIA haijadiliwi tena bali inafuatwa.
June 4, 2012

Add a comment

Your name:
Your location:
Your email:
(optional)
Your email address will not be published.