Envaya

MED YAANZISHA MFUKO WA ELIMU YA SEKONDARI CHIDACHI  

Na. Barakaely Christopher

Shirika la Marafiki wa Elimu Dodoma (MED) kwa kushirikina na wananchi wa kata za Kikuyu Kusini na Mkonze Manispaa ya Dodoma wameanzisha mfuko wa kuwalipia ada na michango mingine wanafunzi wote watakaofaulu mtihani wa darasa la saba na kujiunga na elimu ya sekondari kutoka shule ya msingi Chidachi.

Lengo la mfuko huo ni kuwahamasisha wanafunzi wa shule ya msingi chidachi kuongeza juhudi kwenye masomo yao na kuwa na uhakika wa kuendelea na elimu ya sekondari.

Muasisi wa mfuko huo Bw. Davis Makundi ambaye pia ni Mlezi wa shule ya Msingi Chidachi na Mratibu wa Shirika la Marafiki wa Elimu Dodoma (MED) alianza kampeni ya kuanzisha mfuko huo Septemba mwaka jana katika mahafali ya nne ya darasala la saba ambapo mgeni rasmi alikuwa Meneja wa Benk ya Posta Tanzania Bw. Emmanueli Gyumi aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Posta Tanzania.

Katika mkutano huo wazazi wa wanafunzi wa shule ya msingi Chidachi uliofanyika shuleni hapo wameomba mfuko huo uanze haraka na kuazimia kuwa wazazi wote wenye watoto katika shule hiyo wahusike kuchangia uendelevu wake ili kupunguza mzigo wa kusomesha watoto pasi na uhakika kutokana na kipato duni walichonacho. Akaunt ya Mfuko huo itafunguliwa katika Benki ya Posta Tanzania Tawi la Dodoma.

Katika mkutano huo wazazi walipokea jumla ya madawati 15 na seti moja ya bendi ya shule vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya sh. 1,200,000 fedha ambazo zimetokana na michango ya wadau wa elimu, wazazi na wanafunzi kupitia kazi za mikono kwenye somo la Elimu ya Kujitegemea (EK).

Mwalimu Mkuu wa Shule ya hiyo Bi. Ashura Mhoji alieleza kuwa shule yake imekuwa ikifanya vizuri kwa kufaulisha wanafunzi kwa kati ya 80% hadi 100% kutokana na mwamko na ushirikiano uliopo baina ya walimu, wazazi, wanafunzi na wadau mbalimbali wa Elimu. Aidha alilishukuru shirika la MED kwa mchango wake mkubwa ambao limekuwa likitoa mara kwa mara katika shule hiyo. MED katika mkutano huo imechangia kiasi cha sh. 150,000 kwa ajili ya madawati na mfuko wa Elimu.

 

13 Februari, 2013
« Iliyotangulia Ifuatayo »

Ongeza maoni

Jina lako:
Mahali ulipo:
Email yako:
(sio lazima)
Anwani yako ya email haitachapishwa.