Asili (Kiswahili) | Kiswahili |
---|---|
Na Neema Nkumbi – Iramba, Singida Wachimbaji wadogo wa madini mkoani Singida wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa hatua madhubuti za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha sekta ya madini, zikiwemo ugawaji wa leseni mpya na kuondoa vikwazo vilivyokwamisha maendeleo ya wachimbaji wadogo. Pongezi hizo zimetolewa Agosti 23, 2025, katika Kongamano la Wachimbaji Wadogo wa Madini wa Kanda ya Kati lililofanyika Sekenke One, Shelui Wilaya ya Iramba, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde. Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema Serikali imejipanga kuongeza kiwango cha utafiti wa kina wa madini kutoka asilimia 16 hadi kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030, kupitia mkakati wa Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri. Kwa ajili ya utekelezaji wa mkakati huo, Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 115, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa helikopta maalum kwa ajili ya upigaji picha za anga na ujenzi wa maabara za kisasa zitakazosaidia wachimbaji wadogo kufanya uchambuzi wa madini kwa ufanisi. "Hatutaki tena kuuza mawe ghafi. Tunalenga kutoka kusafirisha mawe kwenda kuuza bidhaa za madini zilizoongezewa thamani, Hii ni kwa faida ya wachimbaji wadogo, vijana, wanawake na taifa kwa ujumla,” amesema Mavunde. Waziri Mavunde ameongeza kuwa kampuni kubwa za madini zimeonesha nia ya kuwekeza katika mgodi mkubwa wa dhahabu utakaokuwa katika mikoa ya Singida na Dodoma, hatua ambayo inatarajiwa kuongeza ajira, mapato ya Serikali na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kitaifa kupitia sekta ya madini. Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego amesema kuwa sekta ya madini ndiyo inayoongoza kwa kasi ya ukuaji wa uchumi mkoani humo, ambapo kwa mwaka wa fedha 2024/25, Singida imekusanya zaidi ya shilingi bilioni 26, ikizidi lengo la awali la bilioni 24. “Zaidi ya tani 2.7 za dhahabu huzalishwa kila mwaka, ambapo tani 1.5 zinatoka kwa wachimbaji wadogo. Huu ni ushahidi kuwa sekta hii imekuwa mkombozi wa wananchi wetu,” amesema Dendego. Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, Mhandisi Sabai Nyansiri, amesema mafanikio hayo yamechangiwa na mazingira rafiki yaliyowekwa kwa wachimbaji wadogo pamoja na usimamizi madhubuti wa shughuli za uchimbaji. Nyansiri amebainisha kuwa uzalishaji wa madini mkoani Singida umeongezeka mwaka hadi mwaka na kwa sasa sekta hiyo inachangia zaidi ya shilingi bilioni 6 kwa mapato ya Serikali kwa mwaka. Kwa mujibu wa wachimbaji hao, hatua ya Serikali kufuta leseni 2,648 ambazo zilikuwa hazitumiki na kuzigawa upya kwa wachimbaji wadogo kumesaidia kupunguza migogoro ya maeneo na uchimbaji holela, hivyo kufungua ukurasa mpya wa tija na uwajibikaji katika sekta hiyo muhimu. Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), Bw. John Bina, amesema zaidi ya wachimbaji wadogo milioni 6 wanashiriki kikamilifu katika shughuli za madini nchini na kuchangia takriban asilimia 40 ya mapato ya sekta hiyo. “Tunatambua dhamira ya dhati ya Rais Samia katika kuwatambua na kuwawezesha wachimbaji wadogo, Hii ni heshima kubwa kwetu, na ndiyo maana leo tunasherehekea mafanikio haya,” amesema Bina. Bw. Bina, ametoa rai kwa serikali kutumia fursa ya amani na utulivu nchini kujenga soko kubwa la madini ndani ya Tanzania. “Tunaamini tunaweza kupata Dubai yetu hapa nyumbani Tukijenga soko hapa, wachimbaji watanufaika zaidi na kodi zitabaki nyumbani,” amesema Bina. |
(Bila tafsiri) |
Ili kuhariri tafsiri, lazima ufungue. Fungua · Jiandikishe