Envaya

Ubusobanuro: Kiswahili (sw): User Content: WI0006F24BB19F1000041348:content

Base (Igiswayire) Kiswahili

Tutatumia Elimisha kuokoa jamii

Makala hii imeandikwa na Joachim Nyambo, Mbeya.

MWANAHABARI yeyote ni tegemeo kubwa katika jamii inayomzunguka. Hii ni kutokana na mchango mkubwa wa kazi yake wa kufichua yanayoendelea katika eneo husika, kuelimisha na hata kuhabarisha na kuburudisha.

Kupitia kalamu yake jamii huweza kunufaika hasa kwa mwanahabari aliyeapa kuitumikia jamii. Lakini wapo wanaoona kuandika pekee hakutoshelezi kuitumikia jamii na hasa kutokana na mazingira magumu yanayomzunguka mwanahabari katika nchi zinazoendelea, ikiwamo Tanzania.

Festo Sikagonamo anayefanya shughuli za habari mkoani Mbeya ni mmoja wa wanahabari wa namna hiyo. Baada ya kuona amefanya kazi kwa muda mrefu huku akiona malengo ya kuitumikia jamii akiyafikia kwa kusuasua akaona ni lazima atafute njia mbadala.

Mwaka 2009 aliamua kuanzisha shirika lisilo la kiserikali la Elimisha. Shirika hilo lililo chini ya waandishi wa habari lililenga kufanya kazi mahali popote Tazania Bara.

Sikagonamo ndiye amekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Elimisha, anasema taasisi hiyo ilianzishwa kutokana na msukumo wa wanahabari uliosababishwa na mguso walioupata katika utendaji wao wa kazi za kila siku ambapo katika kutekeleza majukumu yao ya kutafuta na kusambaza habari, katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya vijijini wanashuhudia matatizo mengi ya kijamii.

“Ni katika hali hiyo mimi na wenzangu tukaona uwepo wa changamoto, upungufu na pengo ambalo lisingeweza kuzibwa kwa kutafuta na kuandika habari peke yake, na hivyo kuona umuhimu wa kuanzisha shirika hili,” anasema.

Miongoni mwa changamoto na upungufu uliosukuma kuanzishwa kwa Elimisha kuendelea kwa umasikini na elimu duni miongoni mwa wananchi, hasa vijijini, licha ya Serikali kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya kupunguza umasikini hali inayothibitisha kuwepo na mdororo wa uwajibikaji miongoni mwa wananchi na viongozi kutotimiza wajibu.

Huduma za mashirika na asasi nyingi zinalenga maeneo ya mijini wakati makundi makubwa ya wahitaji yapo vijijini. Kutokana na ukosefu wa utawala bora, wananchi hawa wameshindwa kushiriki kikamilifu katika mipango ya maendeleo pamoja na kuhimiza uwajibikaji wa viongozi wao ili kuharakisha maendeleo.

Maeneo mengi ya vijijini, mfumo dume umewaacha pembezoni wanawake na hivyo kuwanyima fursa za kushiriki kikamilifu katika mikutano ya maamuzi ya vijiji na hivyo hoja zao na vipaumbele vyao kukosa nafasi katika mipango ya maendeleo.

Hali kadhalika, wanawake wanaachwa nyuma kuwania nafasi za uongozi hata za kwenye kamati za miradi ya maendeleo ya vijiji vyao kama miradi ya maji, elimu na Ukimwi na kusababisha kupungua kwa nguvu kazi.

Sikagonamo anasema jitihada za Serikali kuinua uchumi vijijini bado zinakwama hivyo vijana wavulana kwa wasichana wanakata tamaa ya maisha na kukimbilia mijini kwa kukosa elimu ya darasani na ya ujasiriamali ya kuwaondoa katika umaskini kupitia rasilimali zinazowazunguka ikiwemo ardhi nzuri na fursa zingine.

Kundi kubwa la watoto ambao ndiyo mustakabali wa taifa wamekosa matumaini kutokana na baadhi yao kukosa fursa za elimu kwa wazazi kutothamini elimu huku wengine wakitumikishwa kinyume cha sheria katika mashamba makubwa, kufanya vibarua vya kubeba mizigo, kuchunga mifugo, na kazi za ndani hali ambayo inawaathiri kisaikoloji maisha yao.

Anasema wapo yatima ambao idadi yao inazidi kuongezeka kutokana na ugonjwa wa Ukimwi wameachwa bila msaada.

“Kwa haya tukaona kuna ulazima wa kuwa na chombo cha kusaidia kuwezesha jamii hasa wanawake, watoto na vijana kuwa na Afya na Elimu bora, kujikinga na maambukizi mapya ya VVU/UKIMWI kushiriki na kushirikishwa katika shughuli za maendeleo ya nchi, kufaidi matunda ya jitihada zao na kupewa fursa zaidi katika nyanja mbalimbali zikiwemo za uongozi na utawala ili kuwa na maisha bora, endelevu na yenye kutimiza ndoto zao.”

Lakini haya yote yanawezaje kufanikiwa kupitia taasisi hii iliyo chini ya mwanahabari. Sikagonamo anasema ili kufikia ndoto yake hii, Shirika la Elimisha kwa kutumia vyombo vya habari na mbinu nyingine, limejifunga kufanya mambo mengi kwa hisani ya wadau mbalimbali watakaoguswa.

Anayataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kuelimisha jamii juu ya haki, wajibu na majukumu ya raia na viongozi kwa mujibu wa katiba ya nchi kupitia midahalo, warsha na semina, sambamba na matumizi ya vyombo vya habari katika upana wake.

Kuibua vyanzo vinavyochangia kuongezeka kwa huduma duni, za elimu, umasikini na magonjwa, kufanya tafiti zinazohusu vyanzo vya umasikini, elimu duni, afya hafifu, athari za VVU/UKIMWI na matatizo ya wanawake, watoto na vijana kwa ajili ya maendeleo yao na taifa kwa ujumla ni jukumu pia la Elimisha.

Mkurugenzi Mtendaji huyu anasema kushirikiana na jamii katika kujenga ufahamu wa sera na sheria zinazohusu wanawake, watoto na vijana, kuhamasisha ushiriki wa wanawake na vijana katika kuainisha na kuchambua matatizo na mahitaji yao kupitia mikutano halali na maamuzi kwa lengo la kuandaa mikakati ya kutafutia ufumbuzi.

“Tumelenga pia kuwajengea uwezo wanawake na vijana juu ya uandaaji, utekelezaji, ufuatiliaji na ufanyaji tathmini wa miradi yao ya kijamii na kiuchumi, na kuhudumia makundi maalum, kama watoto yatima na waishio katika mazingira hatarishi, watu wenye ulemavu na wazee”. Anasema na kuongeza.

“Hatuishii hapo bali tunakwenba mbali zaidi na kuhakikisha tunaendesha kampeni ya kutokomeza tabia ya utegemezi, kutojiamini na ukosefu wa ari ya kutojituma kufanya kazi iliyojengeka miongoni mwa wanawake na vijana kwa njia ya elimu na stadi mbalimbali”.

Anasema shirika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inanuia kukuza na kuhimiza uadilifu na uwajibikaji wa Serikali za Mitaa ili ziwe na ufanisi katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi, hususan makundi maalumu na walioko vijijini/pembezoni.

Akizungumzia shughuli zinazofanywa na shirika tangu kupata usajili wake mwaka 2010, Sikagonamo anasema Elimisha inafanya shughuli za utafiti kuhusu chanzo cha umasikini wa wananchi hasa vijijini katika mkoa wa Mbeya kwa lengo la kuisaidia kutafuta ufumbuzi.

Hii inatokana na ukweli kwamba licha ya mkoa wa Mbeya kuwa na rasilimali nyingi na jitihada nyingi za wadau mbalimbali, bado umasikini umeonekana kuzidi kuotesha mizizi.

“Hali kadhalika Elimisha haiko nyuma katika suala la uhamasishaji katika uhifadhi na utunzaji mazingira ambao unapewa msukumo mkubwa.

Baadhi ya tafiti tulizofanya maeneo mbalimbali hasa vijijini tumebaini kuwa wakati uchumi unapoyumba watoto wanaotoka katika jamii zenye kipato cha chini wanakumbana na tishio kubwa la kutofanya vyema katika masomo yao”.

Anasema mara nyingi, jambo hilo huanza kuwadhuru watoto hao wakiwa wangali katika kiwango cha shule ya msingi, katika mfumo wa elimu Tanzania na baadhi ya nchi za afrika, watoto hao hupata tishio kubwa zaidi, ikilinganishwa na watoto wengine, ya kutopata maadaraja mazuri shuleni na hata kukosa kumaliza masomo yao ya shule.

Kuna mambo kadhaa yanayoeleza sababu za wanafunzi kuwa na mazoea ya kuacha shule anasema. Anafafanua kuwa kwa watoto walio na rasilimali kidogo, tishio linatokana na sababu kama vile viwango vya watoto waliovunja sheria, viwango vya juu vya watoto waliopata mimba, wakiwa wadogo na kutegemea kiuchumi mzazi au wazazi wenye kipato cha chini.

Mwanahabari huyu aliyeamua kuisaidia jamii kwa njia mbadala ya uana habari anasema familia na jamii zisizotilia maanani uwekezaji katika elimu na maendeleo ya watoto masikini hupata matokeo yasiyo mazuri kwani baadaye watoto hao hukosa kazi na huwa na mapato madogo, Viwango vikubwa zaidi vya kuzaa mapema na hatari zake kwa familia, afya na maisha bora kwa ujumla ndiyo mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa kwa kuwa elimu kutoka kiwango cha shule ya msingi hadi shule ya sekondari ina umuhimu mkuu maishani.

“Umasikini mara nyingi huathiri, kwa kiwango kikubwa cha kufaulu kwa watoto shuleni. Kwa hivyo, tunaweza kusema kuwa watoto wanaoishi katika hali ya umasikini au chini ya kiwango cha umasikini watakuwa na wakati mgumu zaidi kufaulu katika elimu kuliko watoto wanaoishi katika hali isiyo ya umasikini”.

“Watoto masikini hawapati huduma muhimu za afya na hii inawafanya wakose kwenda shuleni kwa siku nyingi katika kila mwaka. Pia, kuna uwezekano zaidi kwa watoto masikini kuteseka kwa njaa, uchovu, kukasirika hovyo, maumivu ya kichwa, maambukizi ya masikio, mafua na homa… Magonjwa haya yana uwezo wa kumzuia mtoto au mwanafunzi kuelewa yale anayofunzwa darasani”.

Yapo mambo mengi yanayotajwa na Sikagonamo kama matarajio ya kazi katikaa shirika la Elimika. Lakini jambo la msingi hapa ni kwa wanahabari nchini kujifunza namna ya kubadilika ili jamii izidi kunufaika zaidi na uwepo wao.

Ni vema wanahabari wakachukulia maamuzi kama haya ya Sikagonamo na wengine wengi walioonesha mabadiliko kwa kuchukua mikakati yao kama changamoto za wao kubadilika. Nayasema haya kutokana na uzoefu nilionao katika tasnia hii.

Yawezekana ni uzoefu mdogo lakini hakuna anayeweza kubisha kuwa wanahabari wengi wamebaki watu wa kuandika na kusambaza habari. Ni kutokana na kukosa ubunifu wengi maisha yao yamebaki mikononi mwa wahariri wanaoamua kazi zao zitoke ama zitupwe kapuni.

Matokeo ya kazi za wanahabari hawa kutupwa kapuni ni janga kubwa kwa vyanzo vya habari hizo hasa wale wananchi waishio katika maeneo ya pembezoni ambao sauti zao ni mara chache kusikika.

Iwapo wanahabari tukabadilika tukawa na ubunifu wa kuzisaidia jamii zaidi ya kuchukua habari zao kuziandika na kuzitangaza ni wazi jamii zitanufaika. Tuige mfano huu na wa wanahabari wengine walioona sababu ya kuzisaidia jamii kwa njia mbalimbali badala ya kuishia kuandika na kutegemea wahariri kuzipitisha habari zetu.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa email nyambojoachim@gmail.com ukumwitu@yahoo.com simu 0756 40 95 97/0713 12 83 71.

(Not translated)

Kugirango ugire icyo uhindura kubyo wasemuye, ugomba kwinjira mu rubuga Injira · Iyandikishe