Envaya

ATHARI   ZA MAFURIKO JIJINI DAR ES SALAAM

Kutokana na mafuriko yaliyolikumba jiji la Dar es salaam,tarehe 20/12/2011 wananchi wengi mpaka sasa hawana makazi ya kudumu na huduma za afya zimezidi kuzorota kwa kiwango kikubwa.

Takwimu zinaonesha kuwa watu wapatao 41 wamefariki dunia kutokana na mafuriko hayo,wakati wengine mamia wamepoteza makazi na mali zao.Baada ya tukio hilo kutokea serikali na wadau wengine walishirikiana kuhakikisha kuwa misaada ya hali na mali inapatikana kwa ajili ya wahanga wa tukio hilo.

Hali ya maisha kwa wahanga imekuwa ngumu zaidi kutokana na kukabiliwa na mafuriko hayo,hususani kwa wale waliokuwa wanaishi maeneo ya bondeni.Pamoja na sababu za kisayansi zilizoainisha kuchangia kutokea kwa mafuriko hayo,bado kuna kila sababu ya kuamini kuwa uchafu uliokithiri katika maeneo mengi ya jiji na miundo mbinu mibovu imechangia kuongeza ukubwa wa tatizo.

Utupaji wa taka ovyo katika mifumo ya kupitishia maji,ulipelekea mikondo ya maji kubadili uelekeo wake kutokana na kukosa uelekeo ulio sahihi.Mkazi mmoja wa kimara kilungule aliyejulikana kama baba Jesca,alieleza kuwa uchafu uliokithiri katika mitaro ya maji ndio sababu iliyochangi kwa kiasi kikubwa maji kubadili uelekeo wake na kuingia katika nyumba,baada ya kukosa uelekeo wa moja kwa moja.

Wakati mwingine kutokana na mitaro kuziba ilibidi maji yakose uelekeo na hivyo kuharibu maeneo menginie,hasa ikichukuliwa kuwa sehemu nyingi za jiji la Dar es salaam zina udongo wa kichanga,hali ambayo ni rahisi kwa maji kujipenyeza mahala popote hasa pale yanapokutana na ukinzani.

Maeneo mengi ya jiji la Dar es salaam yamejaa taka taka,hali ambayo ni hatari kwa afya za wakazi wa maeneo husika na mkoa kwa ujumla.Ukibahatika kupita maeneo ya jangwani,kimara baruti,ubungo kibangu,ubungo msewe,bonde la msimbazi na maeneo mengine ya tabata,mburahati,mbezi na hata katikati ya jiji kwa kutaja baadhi hali ya mazingira ni mbaya sana.Hali hiyo inapelekea kuwepo kwa mlipuko wa magonjwa ya mara kwa mara,kama vile kipindu pindu ,kuhara na ugonjwa matumbo.

Hali ni mbaya zaidi kwenye maeneo yaliyokumbwa na mafuriko,kutokana na maeneo hayo kuendelea kuwa na uchafu uliochanganyikana na kinyesi cha binadamu.Iwapo hatua za haraka hazitachuliwa,madhara yake yatakuwa makubwa sana,hali ambayo itaiingiza serikali katika gharama nyingine.

Nyumba nyingi bado zimejaa tope zenye vinyesi hali ambayo ni hatari kwa afya za binadamu,hususani watoto wadogo ambao hawajui madhara yoyote wanapokuwa wanacheza katika tope hizo.Miundo mbinu ya maji nayo imechafuliwa sana na mafuriko hayo,hivyo hali hiyo inaleta wasiwas zaidi ya watu kunywa maji yenye maji yenye uchafu na yasiyo salama kwa afya zao.

Jitihada za makusudi inabidi zichukuliwe kuhakikisha kuwa mazingira na maeneo yaliyoathiriwa yanakuwa safi na salama kwa watu kuishi.Elimu ya mazingira ni muhim,hasa katika kuondoa tope kwenye nyumba,kufukia madimbwi ya maji machafu,kuchimba mashimo ya taka,kusafisha mitaa yote ili kuiweka katika hali ya usafi na salama zaidi.

Suala la kuyaweka mazingira katika hali ya usafi ni la wadau wote.Jeanmedia ikitambua umuhimu wa afya kwa binadamu imelenga kutoa elimu ya mazingira kwa wakazi wa jiji la Dar es salaam,kwa lengo la kulifanya jiji hili kuvutia kimadhari.

Kwa kuwa jeanmedia imeonesha njia kwenye suala hili,ni vema ikaungwa mkono na wadau wengine ili kufikia lengo la kuyahifadhi mazingira yetu.Wakazi walioathirika kwa mafuriko wanahitaji kupewa elimu ya mazingira kwa kuyaweka katika hali ya usafi,kuchemsha maji ya kunywa,dawa za kutibu maji na dawa na kuulia wadudu.

Wapo wakazi walio hamishiwa eneo la mabwepande,kama sehemu ya makazi yao mapya,kuna kila sababu ya wakazi hawa kupewa elimu ya kuhifadhi mazingira kutokana na huduma nyingi za kijamii kutopatikana.Huduma za maji,vyoo,dawa na vifaa vya kufanyia usafi nai moja kati ya vitu muhimu vinavyohitajika kwa wahanga hawa katika kipindi hiki wanachoanza maisha upya.

Jeanmedia inaamini kuwa ustawi bora wa maisha ya mwanadamu hutegemea ubora wa mazingira anayoishi,na kinga ni bora kuliko tiba,hivyo elimu inayotegemewa kutolewa na jeanmedia ni kinga kwa maradhi ya mlipuko.

Kusubiri tatizo litokee ndio tuanze kutumia gharama katika kuliondoa au kulidhibiti,tunazalisha matatizo zaidi,maana tatizo linapotokea tayari linakuwa limeisha acha madhara ya kifo au uharibifu wa mali na makazi ya watu.

Kutoa elimu ya mazingira itasaidia kupunguza gharama zisizokuwa na sababu kwa mwananchi.Mfano badala ya kusubiri mwananchi augue kipindu pindu ndio apatiwe matibabu ni vema akapewa elimu ya kujikinga na maradhi hayo,ili gharama ambazo zingetumika kwenye matibabu zitumike kwenye huduma nyingine za kimaendeleo.

Ikumbukwe kuwa hata mabadiliko ya tabia nchi yamechangiwa kwa kiwango kikubwa na shughuli za kibinadamu na harakati zake kuyatawala mazingira.Kutokana na ukweli huo,elimu pekee ndio njia mbadala ya kuhifadhi mazingira na kuyafanya kuwa endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Taarifa zilizokuwa zinatolewa na idara ya hali ya hewa kama zingezingatiwa na kutiliwa kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kupunguza ukubwa wa tatizo au kulidhibiti kabisa.Mali pamoja na maisha ya watu yangeokolewa iwapo serikali na wadau wengine wangechukua jukumu la kuwaondoa la kuwaondoa wakazi wa bondeni kama ilivyofanyika hivi sasa.

Vile vile jeanmedia inaamini kuwa huu ni wakati mwafaka wa kutoa elimu ya mazingira ili kupunguza baadhi ya matatizo yasiyo ya lazima kutokea.Suala la mazingira ni la mtambuko,linahitaji uhamasishaji kwa kila mdau kutambua umuhimu wa kuyatunza mazingira kwa kupanda miti kwa wingi,kuepuka kutupa taka katika vyanzo vya maji,kuepuka kuchoma misitu,ujenzi holela usiofuata taratibu bora za ujenzi kama ilivyo miji mingi nchini,kuepuka kuchoma takataka zenye kimekali katika maeneo yenye makazi ya watu.

Ikiwa wewe ni mtu binafsi,shirika,taasisi,kikundi cha watu iunge mkono jeanmedia katika kuhakikisha kuwa inafanikisha lengo lake la kutoa elimu hii kwa jamii.Waafrika tunao msemo methali isemayo,ngoja ngoja yaumiza tumbo,hivyo linalowezekana leo lisingoje kesho.

 

 

ANTON MWITA KITERERI

 

January 5, 2012
« Previous Next »

Add a comment

Your name:
Your location:
Your email:
(optional)
Your email address will not be published.