Envaya

ELIMISHA

Amateka

Uru rupapuro ruragaragazwa mu rurimi rw'umwimerere Igiswayire. Edit translations

 

                                                www.elimishatz.org

Utangulizi

ELIMISHA ni shirika lisilo la kiserikali, lililoanzishwa na waandishi wa habari mkoani Mbeya mwaka 2009 Kwa ajili ya kufanya kazi mahali pote Tazania Bara.

ELIMISHA ilipata usajili wake rasmi Aprili mwaka 2010 kwa namba ooNGO00003744 Lengo la kuanzishwa kwa shirika hili ni kusadia jitihada za serikali katika kuwezesha jamii hasa wanawake, watoto na vijana kuwa na Afya, Elimu bora, na kuwa na kipato endelevu kupitia miradi rafiki na mazingira na kushiriki na kushirikishwa katika shughuli za maendeleo ya nchi, kufaidi matunda ya jitihada zao na kupewa fursa zaidi katika nyanja mbalimbali zikiwemo za uongozi na utawala ili kuwa na maisha bora, endelevu na yenye kutimiza ndoto zao.

 Ili kufikia ndoto yake hii, shirika la ELIMISHA kwa kutumia vyombo vya habari na mbinu nyingine, limejifunga kufanya yatuatayo;

 • Kuelimisha jamii juu ya haki, wajibu na majukumu ya raia na viongozi kwa mujibu wa katiba ya nchi kupitia midahalo, warsha na semina, sambamba na matumizi ya vyombo vya habari katika upana wake.

 • Kuibua vyanzo vinavyochangia kuongezeka kwa huduma duni, za Afya, Elimu, maji,umasikini,miundombinu na magonjwa.

 • Kufanya tafiti zinazohusu vyanzo vya umasikini, ukosefu wa maji, Elimu, ya kujitegemea, Afya, na matatizo ya wanawake, watoto na vijana kwa ajili ya maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

• Kushirikiana na jamii katika kujenga ufahamu wa sera na sheria zinazohusu wanawake, watoto, vijana na jamii kwa ujumla.

 • Kuhamasisha ushiriki wa wanawake na vijana katika kuainisha na kuchambua matatizo na mahitaji yao kupitia mikutano halali na maamuzi kwa lengo la kuandaa mikakati ya kutafutia ufumbuzi.

• Kuwajengea uwezo wanawake na vijana juu ya uandaaji, utekelezaji, ufualitiliaji na ufanyaji tathimini wa miradi yao ya kijamii na kiuchumi, na kuhudumia makundi maalum, kama watoto yatima na waishio katika mazingira hatarishi, watu wenye ulemavu na wazee.

 • Kuendesha kampeni ya kutokomeza tabia ya utegemezi, kutojiamini na ukosefu wa ari ya kutojituma kufanya kazi iliyojengeka miongoni mwa wanawake na vijana kwa njia ya elimu na stadi mbalimbali.

 • Kushirikiana na wadau mbali mbali katika kukuza na kuhimiza uadilifu na uwajibikaji wa serikali za mitaa ili ziwe na ufanisi katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi, hususan makundi maalum na walioko vijijini/pembezoni.

KUANZISHWA KWA SHIRIKA

Shirika la ELIMISHA lilianzishwa kutokana na msukumo wa wanahabari uliosababishwa na mguso walioupata katika utendaji wao wa kazi za kila siku. Katika kutekeleza majukumu yao ya kutafiti, kutafuta na kusambaza habari, waanzilishi wa shirika hili, wanapata fursa ya kuyafikia maeneo mengi yakiwemo ya pembezoni/vijijini, ambapo wanajionea na wanashuhudia matatizo mengi ya kijamii.

 Ni katika hali hiyo waliweza kuona uwepo wa changamoto, upungufu na pengo ambalo lisingeweza kuzibwa kwa kutafuta na kuandika habari peke yake, na hivyo kuona umuhimu wa kuanzisha shirika hili. Miongoni mwa changamoto na upungufu uliosukuma kuanzishwa kwa ELIMISHA ni pamoja na;

• Kuendelea kwa umaskini na Elimu duni miongoni mwa wananchi hususan wa pembezoni/vijijini licha ya serikali kutenga na kupeleka fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya kupunguza umasikini. hii imethibitika kuwepo na mdororo wa uwajibikaji miongoni mwa wananchi na viongozi kutotimiza wajibu.

• Huduma za mashirika na asasi nyingi zinalenga maeneo ya mjini wakati makundi makubwa ya wahitaji; wake kwa waume, vijana na watoto, yapo vijijini. Kutokana na ukosefu wa utawala bora, wananchi hawa wameshindwa kushiriki kikamilifu katika mipango ya maendeleo pamoja na kuhimiza uwajibikaji wa viongozi wao vijijini ili kuharakisha maendeleo.

• Maeneo mengi ya vijijini, mfumo dume umewaacha pembezoni wanawake na hivyo kuwanyima fursa za kushiriki kikamilifu katika mikutano ya maamuzi ya vijiji na hivyo hoja zao na vipaumbele vyao kukosa nafasi katika mipango ya maendeleo. Halikadhalika, wanawake wanaachwa nyuma kuwania nafasi za uongozi hata za kwenye kamati za miradi ya maenendeleo ya vijiji vyao ikiwemo miradi ya Maji, Elimu, Afya,ujenzi na Ukimwi, ambao unachangia kupunguza nguvu kazi.

 • Vijana wavulana kwa wasichana wanakata tamaa ya maisha na kukimbilia mjini kwa kukosa elimu ya darasani na ya ujasiria mali ya kuwaondoka katika umaskini kupitia rasilimali zinazowazunguka ikiwemo ardhi nzuri na fursa zingine.

 • Kundi kubwa la watoto ambao ndiyo mustakabali wa taifa wamekosa matumaini, Baadhi yao wanakosa fursa za elimu kutokana na wazazi kutothamini elimu; wengine wanatumikishwa katika ajira mbaya kinyume cha sheria katika mashamba makubwa, kufanya vibarua vya kubeba mizigo, kuchunga mifugo, na kazi za ndani hali ambayo inawaathiri kisaikoloji maisha yao. Aidha yatima, ambao idadi yao inazidi kuongezeka kutokana na ugonjwa wa UKIMWI, wameachwa bila msaada.

MWELEKEO WA SHIRIKA

Shirika la ELIMISHA, linajifunga katika kuwa chachu na kichocheo cha jamii na wadau mbali mbali katika kuzikabili changamoto hizi ambapo inalenga kufanya yafuatayo:

 • Kujenga hali ya ushirikiano na wadau mbali mbali katika eneo la shughuli zetu kama vile asasi za kidini, asasi zisizo za serikali na serikali za mitaa; halmashauri za wilaya, kata, vijiji na vitongoji kwa lengo la kufikisha huduma za shirika kwa urahisi kwa manufaa ya jamii.

• Kuhamasisha wanawake na vijana kuchukua hatua za kushiriki katika kupanga mipango ya maendeleo na matumizi ya rasilimali zao kupitia mikutano halali ya maamuzi.

• Kufafanua, kutafsiri na kurahisisha sera mbalimba na sheria zinazowahusu wanawake, watoto, vijana na jamii kwa ujumla ili ziweze kueleweka , kutumika na kutekelezwa na wananchi.

• Kuandaa mafunzo, semina, warsha ili kuwajengea wanawake na vijana fikra za kimaendeleo na utamaduni wa kujitegemea, pamoja na kutoa elimu ya afya, na uzazi wa mpango.

•Kutumia wanahabari na watalaam wengine kufanya kazi ya kutafiti na kutambua matatizo ya wanawake, watoto na vijana, kutoa msaada na namna ya kutatua, kutoa elimu kwa jamii kupitia njia mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari kama tv, magazeti, radio, majarida, mtandao,blogs na vipeperushi.

• Kuandaa mafunzo, mijadala na midahalo mbali mbali ili kukuza na kuhimiza uadilifu na uwajibikaji wa serikali za mitaa katika uboreshaji wa huduma zake kwa jamii.

KAZI ZA SHIRIKA

• 1. Tangu kuanzishwa kwake ELIMISHA inafanya shughuli za utafiti kuhusu chanzo cha umaskini wa wananchi hasa vijijini katika mkoa wa Mbeya kwa lengo kuisaidia kutafuta ufumbuzi. Hii inatokana na ukweli kwamba licha ya mkoa wa Mbeya kuwa na rasilimali nyingi na jitihada nyingi za wadau mbalimbali, bado umasikini umeonekana kuzidi kuotesha mizizi.

• 2. Kuanzia Jun 2010 ELIMISHA inaendesha mradi mdogo wa kusaidia watoto wa shule ambao ni yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi katika kijiji cha Nsonyanga wilaya ya mbarali. Pia mradi huu unahusisha uhamasishaji wa wananchi na uongozi wa vijiji kuona uwezekano wa kuanzisha miradi endelevu ili kupunguza umasikini ambao kwa sehemu kubwa unachangiwa na uwajibikaji duni wa viongozi wa serikali za mitaa, pia kuanzisha mfuko wa maendeleo wa vijiji ili kuwasaidia watoto yatima. 

UTENDAJI. Shughuli zote kwa sasa zinagharamiwa na ELIMISHA yenyewe kutokana na michango binafsi ya wanachama ikiwemo kujitolea muda na rasilimali nyingine.

********************  www.elimishatz.org  **********************