Envaya
Uru rupapuro ruragaragazwa mu rurimi rw'umwimerere Igiswayire. Edit translations

JAMII YA KIISLAM NA WATANZANIA INAWATAZAMA VIPI WATOTO YATIMA NA WAZEE

Sheikh Juma A. Simba (Mugumu Serengeti)
25 Kamena, 2013 at 12:39 EAT (edited 17 Ukuboza, 2020 at 20:59 EAT)

 

 

MADA

JAMII YA KIISLAM NA WATANZANIA INAWATAZAMA VIPI WATOTO YATIMA NA WAZEE

                                                          

بسم الله الرحمن الرحيم

الحمد لله رب العالمين، أرسل رسوله بالهدى ودين الحق ليظهره على الدين كله، وأشهد أن لا إله إلا الله وحده لا شريك له، وأشهد أن محمدًا عبده ورسوله، صلى الله عليه وعلى آله وصحبه، والذين اتبعوهم بإحسان، وسلم تسليمًا.

                                 

           Waislam na Watanzania katika hali halisi tumeacha mambo miongoni mwa mambo yaliyowajibu kwetu,na tumebaki kushabikia hoja za kisiasa zaidi kuwa huyu ni hodari wa kusema na huyu si hodari wa kusema, siasa ambazo mwisho wake ni kutufikisha sisi na taifa letu mahala pabaya kabisa na siku ya mwisho mbele ya Mola wetu tukafikia katika adhabu ya Moto, tuzinduke ndugu zangu.

 Pia tumekuwa tukitumia muda mwingi katika malumbano ya kisiasa na kuacha kutumia muda huo katika kutenda yaliyowajibu kwetu kwa masilahi yetu mbele ya Mola wetu na taifa letu hapo baadae. Mimi leo napenda tukumbushane jambo litakalo imarisha Imani zetu na kutuweka karibu na Mola wetu, pia litatoa migogoro isiyo ya lazima katika jamii zetu endapo tutalifanya vile alivyotuamrisha Mola wetu na Mtume wake, na hii itakuwa ni jambo jema tukitumia muda huo katika kutekeleza wajibu huu, na tutaweza kufikia lengo la kuunusuru Umma kwa jumla, kwani kwa asilimia kubwa migogoro,vurugu,uhalifu nk inatokana na kutojali au kutoshughulikia matatizo ya makundi yaliyopewa umuhimu na Mola wetu ambayo makundi hayo ni sababu ya Usalama na Amani ya Dunia hii.

Fikira za wengi wetu zinachukulia matatizo ya makundi hayo na Serikali au taasisi pekee kitu ambacho ni kinyume na maagizo ya Mola wetu, kwani tuliopewa wajibu huo ni sisi na sio Serikali au Taasisi. Na hayo yanaanzia ndani ya majumba yetu kama tutakavyoona hapa chini.

Turudi katika mada yetu,

M/Munga anasema:-

لَا تَعْبُدُونَ إلا الله وَبِالْوَالِدَيْنِ إحْسَانًا وَذِي الْقُرْبَى وَالْيَتَامَى وَالْمَسَاكِين وَقُولُوا لِلنَّاسِ حُسْنًا وَأَقِيمُوا الصَّلَاة وَآتُوا الزَّكَاة {2:83}

83. Hamtamuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu; na muwafanyie wema wazazi na jamaa na mayatima na masikini, na semeni na watu kwa wema, na shikeni Sala, na toeni Zaka

 Tukumbuke  tulichukua ahadi kwa Mola wetu kuwa hatutamuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, na kuwatendea wema wazazi na jamaa na mayatima na masikini, na tunapo zungumza na watu tutumie maneno mazuri ya kuleta masikilizano baina yetu na wala sio ya kututenganisha, na tutimize yaliyo kuwa waajibu juu yetu, nayo ni Sala, na Zaka.

Katika aya hii kuna mambo ya kujifunza kama ifuatavyo:-

  1. Kumwabudu M/Mungu {kufanya yote aliyoamrisha na kuacha yote aliyokataza},
  2. Kuwafanyia wema wazazi wawili,
  3. Kuwafanyia wema jamaa,mayatima na masikini,
  4. Kusema na watu kwa wema {maneno mazuri},
  5. Kusimamisha swala {swala tano},
  6. Kutoa zaka {katika biashara,mali,mazao na mifugo}

         Katika mambo haya sita mimi nitazungumzia kwa ufupi sana mambo 2 {yaani la pili na la tatu} ili kuleta mawazo ya Waislam na Watanzania kwa pamoja tayari kuelekea katika utekelezaji wa mambo hayo hasa katika kipindi hiki kuelekea mwezi mtukufu wa Ramadhani.

KUWAFANYIA WEMA WAZAZI WETU

M/Mungu anasema:-

وَقَضَى ربك ألا تعبدوا إلا إياه وَبِالْوَالِدَيْنِ إحْسَانًا إما يَبْلُغَنَّ عندك الكبر أحدهما أو كلاهما فلا تقل لهما أف ولا تنهرهما وقل لهما قولا كريما {17:23}

23. Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima

Mola wetu amekwishahukumu kuwa tusimuabudu yeyote isipo kuwa Yeye. Na pia tuwafanyie wema kwa ukamilifu wazazi wetu wawili ikiwa wote wapo hai. Na au mmoja wao atakayekuwa yupo hai, kama wataishi au kuugulia kwako na kwa hali ya uzee au unyonge na mwisho wa umri wao, basi usiwachoke kuwasaidia na jitahidi lisikutoke tamko la kuchoka nao au kuudhika kwa yanayo kupata kutokana nao. Wala usiwahamakie na kuwakemea. Na sema nao maneno mazuri, laini, yenye kuwaonyesha ihsani na kuwahishimu.Katika hali isiyo ya kawaida utaona jinsi vijana walivyochupa mipaka ya Mola wao hata kuonesha wazi kutowajali wazazi wao na wengine hata kuwapiga au hata kuwatukana kitu ambacho ni kemeo kubwa toka kwa Mola wetu, kwani imepokewa katika hadithi za Mtume kuwa Laiti kama dunia hii isingekuwa na Wazee,Watoto na Kinamama wajawazito basi Mola wetu angeifuta kabla ya muda wake kutokana na vitendo viovu vya wanadamu.

Ni lazima sisi nasi tukubali matatizo yatakayotokana na wao kama wao walivyo yakubali wakati sisi tukiwa watoto hatujitambui,  hebu tafakari maneno haya ya Mola wetu:-

وَوَصَّيْنَا الْإِنْسَان بِوَالِدَيْه حَمَلَتْهُ أُمّه وَهْنًا عَلَى وَهْن وَفِصَاله فِي عَامَيْنِ أَنْ اُشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْك إلَيَّ الْمَصِير{31:14}

ِ14. Na tumemuusia mwanadamu kwa wazazi wake wawili {awafanyie wema}. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu{tabu} juu ya udhaifu{tabu}, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili. (Tumekuusia): Unishukuru Mimi na wazazi wako. Ni kwangu Mimi ndiyo marudio {ya kila kitu kwa ajili ya malipo}.

 

Hapa pia Mola wetu anatutaka tuwafanyie wema wazazi wetu, na mama zetu tuwape fungu kubwa zaidi na heshima. Kwani wao walitubeba katika mimba kwa tabu zinazozidi kila siku kidogo kidogo. Na tena wakatunyonyesha muda wa miaka miwili, ndipo walipo tuachisha ziwa. Na tumeusiwa:  tumshukuru Mwenyezi Mungu na wazazi wetu. Kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo kwa ajili ya hisabu na malipo

Pia kua hadithi nyingi za mtume zinazotuusia juu ya wazazi wetu mongoni mwazo ni hii;

 

عن أنس وغيره أن النبي صلى الله عليه وسلم لما صعد المنبر ثم قال " آمين آمين آمين " قيل يا رسول الله علام ما أمنت ؟ قال " أتاني جبريل فقال يا محمد رغم أنف رجل ذكرت عنده فلم يصل عليك قل آمين فقلت آمين ثم قال رغم أنف رجل دخل عليه شهر رمضان ثم خرج فلم يغفر له قل آمين فقلت آمين ثم قال رغم أنف رجل أدرك والديه أو أحدهما فلم يدخلاه الجنة قل آمين فقلت آمين ""

 Kutoka kwa Anas na wengineo kwamba Mtume {S.A.W} zama alipopanda katika Mimbari{ili kuhutubu alisikika akisema:}  “AMIN, AMIN, AMIN” tukamuuliza Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu tujulishe kwanini unasema AMIN? Akasema Mtume: kaniijia Jibrilu na kuniambia; Ewe Muhammad, amepata hasara mtu ambaye umetajwa wewe mbele yake na hakukutakia Rehema wewe, sema AMIN, basi nikasema: AMIN, kasha akasema tena; amepata hasara mtu ambaye umeingia mwezi wa Ramadhan kasha ukatoka hakusamehewa, seme; AMIN, basi nikasema AMIN, kisha akasema tena; amepata hasara mtu ambaye ameishi na wazazi wake wawili au mmoja wao halafu hakuingia peponi, sema; AMIN, basi nikasema AMIN””

 Katika hadithi hii inatufundisha kuwa Malaika Jibrilu aliomba dua ya kupata hasara kwa watu 3 na Mtume akaitikia AMIN ambao ni;

  1.  Likitajwa jina la Mtume MUHAMMAD {S.A.W} hamtakii rehema Mtume.
  2. Umefika mwezi wa RAMADHAN wa kusamehewa dhambi,  yeye anaendelea na maovu mpaka mwezi waondoka hakuomba msamaha kwa Mola wake.
  3. Aliyeishi na wazazi wake akawa mkali na kuwakaripia wazazi au mchungu kutoa mali zake kwa sababu ya shida za wazazi wake na kutoa maneno ya kashfa kwao.

 

Aya nyingine M/Mungu anasema:-

 وَاخْفِضْ لَهُمَا جَنَاح الذُّلّ مِنْ الرَّحْمَة وقل رب ارحمهما كما ربياني صغيرا {17:24}

24. Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma. Na useme: Mola wangu Mlezi! Warehemu kama walivyo nilea utotoni.

 Yaani wafanyie upole, na wanyenyekee kwa kuwaonea huruma, na uwaombee dua kwa kusema:- Ewe Mola Mlezi! Warehemu wote wawili, kama walivyo nifanyia huruma walipo nilea utotoni.

عن أبي عبيد عن أبي أسيد وهو مالك بن ربيعة الساعدي قال : بينما أنا جالس عند رسول الله صلى الله عليه وسلم إذا جاءه رجل من الأنصار فقال يا رسول الله هل بقي علي من بر أبوي شيء بعد موتهما أبرهما به ؟ قال نعم خصال أربع : الصلاة عليهما والاستغفار لهما وإنفاذ عهدهما وإكرام صديقهما وصلة الرحم فهو الذي بقي عليك من برهما بعد موتهما " ورواه أبو داود وابن ماجه

 Kutoka kwa Abii Ubaid kutoka kwa Abii Usaid naye Maalik bun Ribiiya Saadiyu Anasema:- nilikuwa nimekaa mbele ya Mtume {S.A.W} alipokuja mtu mmoja wa Kiaansar akasema; Ewe Mjumbe wa ALLAH, je, kuna kitu chochote kimebakia kuwafanyia wema wazazi wangu baada ya kufa kwao? Mtume akasema: ndiyo kuna mambo manne:- waombee dua na uutafute msamaha kwao, uwatekeleze ahadi zao, uwakarimu jamaa zao na uunge udugu, huo ndio wema uliobaki kwako kuwafanyia wao baad aya kufa kwao.

  رَبّكُمْ أَعْلَم بِمَا فِي نُفُوسكُمْ إنْ تَكُونُوا صَالِحِينَ فإنه كان للأوابين غفورا {17:25}

25. Mola wenu anajua kabisa yaliyo nyoyoni mwenu. Ikiwa nyinyi mtakuwa wema, basi hakika Yeye ni Mwenye kuwaghufiria wanao tubia kwake.

 Enyi watu! Mola wenu Mlezi anajua kuliko nyinyi yaliyomo katika dhamiri zenu, na atakuhasibuni kwayo kwa thawabu na Adhabu. Na mkiwa mnakusudia wema na mkautenda, tena mkatokea baadhi yenu mkateleza, na kisha mkarejea kwa Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu Subhanahu atakusameheni. Kwani Yeye ni Mwenye kusamehe daima kwa wale wanao rejea kwake.

Ndugu zangu Waislam na Watanzania katika sehemu ya kwanza nitaishia hapa ili kutafakari kwa makini na kuzingatia tayari kwa kuyafanyia kazi maneno hayo kwani wazazi wetu ndio hao wazee ambao pia wapo katika majumba mbali mbali na sehemu mbalimbali wakitaabika na hawana usaidizi wowote, nao pia ni wajibu wetu kuwashughulikia.

Nakaribisha mawazo na michango yenu juu ya mada hii tushiriki katika mjadala huu.

Ahsanteni.

 

 

Wasiliana na mtoa mada kwa

Sheikh Juma A. Simba

+255 756 229093

+255 713 417921

Sheikhwaser@gmail.com

jmagohe@gmail.com

Mugumu Serengeti.


Andika ubutumwa (Hisha)

Izina ryawe:
Aho uherereye
Your email:
(optional)
Your email address will not be published.