Envaya
Parts of this page are in Swahili. Edit translations

KUKOSA USINGIZI

Na Dr. Clifford B. Majani

Utangulizi

Kukosa usingizi siyo ugonjwa ila ni dalili ya ugonjwa au dalili ya tatizo la kiafya. Mtu anaweza kukosa usingizi katika mojawapo ya mitindo ifuatayo:-

  1. Kushindwa kupata usingizi unapokwenda kulala(mwanzoni).
  2. Kutopata usingizi katikati ya usingizi- mwanzoni unalala, kisha usingizi unakatika na hupati tena usingizi. Watu wengi hupata tatizo hili. Chanzo kikuu cha tatizo hili ni maumivu
  3. Kupata usingizi lakini ukaamka mapema kuliko kawaida (Terminal or late sleeplessness).

Aina za kukosa usingizi kulingana na muda.

  1. Kipindi cha mpito cha kukosa usingizi (Transient insomnia) Siku 1 – Juma 1.
  2. Kukosa usingizi kwa kipindi kifupi (Short term insomnia) Juma 1 hadi majuma 3.
  3. Kukosa usingizi kulikokithiri (Acute insomnia) Majuma 3 – miezi sita.
  4. Kukosa usingizi sugu (Chronic insomnia) Miezi sita – hadi miaka kadhaa.

Vyanzo vya tatizo la kukosa usingizi kwa ujumla.

  • Mabadiliko ya mazingira ya sehemu ya kulala kama vile kukiwa na baridi, moshi, harufu mbaya, chawa , mbu, kunguni au viroboto.
  • Kubadili saa/muda na kulala tofauti na mtu alivyozoea.
  • Makelele, muziki wenye mdundo mzito au sauti ya juu au vurugu.
  • Msongo wa mawazo na sonona
  • Wasiwasi, woga, na hofu
  • Maumizu ya mwili, jino au kichwa.
  • Kupata hisia zisizo za kawaida miguuni – ganzi, baridi, muwasho nk.
  • Matumizi ya aina fulani ya dawa

-          Dexamphetamine

-          Clecoxib (NSAIDS)

-          Pseudoephedrine

-          Fluoruquinolone antibiotics mfano - ciprofloxacin

  • Matatizo ya kimaisha, matatizo ya kifedha, matatizo ya kifamilia
  • Kutotosheka kwa mapenzi ya mahaba au kuwaza sana juu ya mpenzi ambaye yuko mbali (hasa mpenzi mpya).
  • Magonjwa ya mishipa ya damu na moyo – ongezeko la shinikizo la damu(hypertension)
  • Kuacha pombe, sigara au dawa za kulevya ghafla (withdrawal syndrome)
  • Magonjwa mengine

-Pumu, Kikohozi kinachokereketa kinachoendelea, utendaji mbovu wa tezi la shingo(hyperthyroidism) au uvimbe wa maungio( Arthritis).

 

  • Kuvimbewa
  • Minyoo tumboni au katika ngozi.
  • Vinywaji vyenye caffeine vinapotumiwa usiku, (Chai, Kahawa, Cocoa, Red bull, Cocacola na Pepesi)
  • Matumzi ya pombe, tumbaku na uvutaji wa sigara au dawa za kulevya uliokithiri.
  • Kukosekana kwa ulinganifu wa vichocheo vya ujinsia (kupungua kwa Estrogen) hasa kwa wanawake.
  • Ndoto mbaya

-          Jinamizi

-          Kutembea wakati wa usingizi

-          Vurugu wakati wa kusinzia (Violent behavior while sleeping)

  • Ongezeko la vichocheo vya Cortisol na Adrenocorticotropic mwilini – moyo unadunda haraka.
  • Kuangalia picha au sinema zinazotisha au kusisimua mwili wakati wa usiku.
  • Magonjwa ya akili na ubongo
  • Kuwatishatisha watoto kunasababisha wasipate usingizi mzuri wakati wa usiku.

MATIBABU

  1. Matibabu kwa kutumia vyakuladawa na tiba za nyumbani(Non – pharmacological treatment)

Haya ndiyo matatibu bora kabisa kuliko dawa za usingizi.

  • Kula chakula chenye asili ya mimea – mboga za majani, matunda, na nafaka punguza nyama sana au achana nayo kabisa katika kipindi cha kukosa uzingizi.Smamaki wabichi wa kuchemsha ni salama wakitumiwa kwa kiasi, mafuta ya samaki ni mazuri kwa afya ya ubongo.
  • Kunywa maziwa glas 1 angalau saa 2 kabla ya kulala, yana madini ya chokaa(Calcium) ambayo hutia afya mishipa ya fahamu.
  • Usile chakula kingi wakati wa usiku na wahi kula saa tatu (3) kabla ya kulala ili chakula kiyeyuke vizuri na kusharabiwa kabla ya kulala.
  • Achana na vyakula au vinywaji vyenye vichocheo vya Caffein(Chai, Kahawa, Cocacola, Pepsi, Redbull, Cocoa nk.) Usitumie tumbaku, pombe au dawa za kulevya.
  • Tumia vijiko viwili vya asali kabla ya kulala, hii husaidia kupata usingizi vizuri
  • Oga maji ya uvuguvugu kabla ya kulala , hii itasaidia kuchangamsha mishipa ya fahamu.
  • Pata muda wa kukandwakandwa mabegani (Body massage hii hupunguza ukakamavu wa misuli na kuzalisha vichocheo vya raha mwilini ambavyo ni muhimu kwa upatikanaji wa usingizi wa asili.
  • Sikiliza muziki mwololo kabl ya kulala – epuka makelele na muziki wenye midundo mizito.
  • Hakikisha chumba kina hewa safi na hali ya joto linalokubalika. Epuka baridi kali chumbani.
  • Lalia godoro lisilobonyea sana.
  • Fanya mazoezi asubuhi na jioni kila siku kwa dakika zisizopungua 30.Mazoezi ya kutembea ni bora pia. Tofautisha mazoezi na kazi.
  • Usiangalia TV au kusoma katika chumba cha kulala usiku, chumba cha kulala kiwe maalumu kwa ajili ya malazi na mambo yanayohusiana na malazi tu.
  • Usiongee maneno yanayochochea hasira au kuadhibu watoto wakati wa usiku. Epuka ugomvi na ghadhabu wakati wa usiku. Pata dozi ya maneno matamu na kicheko kabla ya kulala. Cheka hata kama ni kwa kujilazimisha inafanya kazi sawa na kicheko cha kawaida.
  • Usitumie vipodozi vyenye viambato vya dawa mfano, Medivin, Diprosone, Betacort –N nk

 

2        Matibabu kwa kutumia dawa  

  • Tumia dawa kwa muda mfupi, dawa za usingizi zikitumika kwa muda mrefu zitaongeza tatizo pale zitakapozoeleka.
  • Tumia dawa ya minyoo mara moja kwa mwezi.
  • Tibu maumivu ya mwili kwa dawa za maumizu kabla y akwenda kulala.
  • Meza vidonge vya melatonin vitaleta usingizi mzuri

Usingizi wa kutumia dawa hauna viwango vya ubora na hauna faida kubwa mwilini kama usingizi wa asili.

Athari za kukosa usingizi:

  • Hasira na ukali bila sababu za msingi
  • Uchovu wa mwili na akili
  • Maamuzi mabovu
  • Usahaurifu
  • Utendaji kazi kwa ufanisi unaathiriwa
  • Kukosa usingizi sugu kunaweza kukasababisha BP, Diabetes, Unene uliokithiri.

       Rejea(References):

  • Roddie and Wallace, The physiology of Diseases, Lloyd – Luke (Medical Books) LTD, London, 1975 Pg. 79.
  • Wikipedia, the free Encyclopedia, Insomnia.
  • Monthly Prescribing Reference (MPR) April 2009, Central Nervous system, Section 3A, Insomnia Pg. 71
  • Marcus A. Krupp and Milton J. Chatton, Current Medical Diagnosis and Treatment 1978, Pp 636-638.

 

MATIBABU YA UGONJWA WA KISUKARI KWA KUTUMIA VYAKULA-DAWA

Utangulizi

Kisukari ni ugonjwa wa muda mrefu(chronic disease) unaotokana na ongezeko la kiasi cha sukari lisilokuwa la kawaida ndani ya damu(zaidi ya 125 mg/dl) ya kipimo cha sukari katika damu wakati mtu anapopimwa kabla ya kula chakula. Vipimo hivi lazima vifanyike katika vipindi viwili tofauti.

Kiwango cha sukari ili kiwe katika kiasi cha kawaida hudhibitiwa na homoni ya insulin inayozalishwa na seli za Beta katika kongosho.Insulin isipozalishwa au kuzalishwa kidogo au ubora wake ukiwa duni au nyama za mwili zikisitisha utumiaji wa insulin, kiasi cha sukari katika damu huongezeka kuliko kawaida na kusababisha ugonjwa wa kisukari.

Aina za kisukari

Kuna aina mbili kuu

  1. Kisukari cha utotoni-hakuna insulin inayozalishwa kabisa. Hiki ni kisukari tegemezi kwa insulin toka nje ya mwili. Kisukari hiki husababisha mwili kukonda.
  2. Kisukari cha ukubwani- insulin huzalishwa kidogo au utendaji wake ni dhaifu. Kisukari hiki si tegemezi kwa insulin ya nje ya mwili. Huambatana na unene.

Sababu/vyanzo vya ugonjwa

  1. Urithi wa vinasaba(genetic factors)vyenye mwelekeo wa ugonjwa
  2. Lishe:

Watoto wadogo wanaonyonya wakinyweshwa maziwa ya ng`ombe, wengine hupata mzio(immunological reaction)kutokana na insulin na protein vilivyomo ndani ya maziwa(Bovin Serum Albumin) na hii huharibu kongosho.

Kula sana na kunenepeana vikiambatana na kutokufanya mazoezi husababisha 55% ya wagonjwa wa kisukari cha ukubwani.

  1. Ujauzito : 4% ya wajawazito hupata kisukari(Gestetional Diabetes)
  2. Uzee: 20% ya wazee katika Amerika ya kaskazini wana kisukari, yaelekea ni kutokana na kutokufanya mazoezi au kuzeeka kwa kongosho.
  3. Matumizi ya tumbaku na pombe pia huchangia kupata kisukari.

Dalili

  • Kukojoa sana
  • Kiu na kunywa maji mara kwa mara
  • Kupata njaa mara kwa mara na kula sana
  • Kutokwa jasho jingi
  • Kuchoka choka sana
  • Kupungua uzito
  • Ganzi na hisia ya kuungua miguuni na mikononi
  • Kuwashwa sehemu za siri hasa kwa wanawake
  • 25-50% ya wagonjwa hawaonyeshi dalili, hugunduliwa kwa bahati kupitia vipimo vya maabara

Athari za ugonjwa huu

Usipodhibitiwa ugonjwa huu husababisha

  • Upofu
  • Upungufu wa nguvu za tendo la ndoa
  • Figo kushindwa kufanya kazi zake vizuri
  • Ugonjwa wa moyo
  • Shinikizo la damu(hypertension)
  • Vidonda visivyopona
  • Matatizo ya mishipa ya fahamu na hisia.

Tiba kwa kutumia vyakula- dawa

Kila unapofikiria tiba hii, kumbuka rangi za taa za barabarani zina rangi tatu, nyekundu, njano na kijani.

Nyekundu(usile kabisa), njano(kula kwa kiasi/uangalifu) na kijani(kula kwa wingi hakuna hatari).

Vyakula hivi usile kabisa(taa nyekundu)

  • Sukari,soda tamu,pipi,chocolate,na biskuti
  • Nyama hasa nyama ya nguruwe, sausage,mayai na maziwa- vyakula hivi vinaongeza rehamu(cholesterol mbaya) na mafuta mwilini, havina nyuzinyuzi(fibers) zinazosaidia tumbo kusaga chakula taratibu na kupunguza mahitaji ya insulin.
  • Vyakula vilivyokobolewa- vinaongeza sukari, vinapungukiwa nyuzinyuzi na vitamin
  • Kahawa , tumbaku na pombe- husababisha seli za mwili ziwe na mwitikio duni kwa insulin kidogo inayozalishwa na pia huharibu mishipa ya fahamu(peripheral nerves)

Vyakula hivi kula kwa kiasi(taa ya njano)

  • Samaki na mafuta ya mimea, usikaange vyakula. Mafuta ya samaki yanaleta afya bora ya mishipa ya fahamu na ubongo
  • Mikate, ugali wa unga usiokobolewa, ndizi za kupika, wali na viazi mviringo vya kuchemsha- vina wanga ambayo hugeuzwa taratibu sana kuwa sukari katika kipindi cha masaa 3-4 ya uyeyushaji chakula tumboni. Vina nyuzinyuzi nyingi,vitamin B1 na E na vinaondosha acid katika damu.
  • Karanga, njugu,njegere,korosho na maharage- huleta nguvu mwilini, hupunguza kiwango cha sukari mwilini na huongeza vitamin na madini mwilini.
  • Matunda:

¨      Matufaa(Apples)- sukari yake ni fructose haihitaji insulin nyingi, hupunguza cholesterol, huimarisha afya ya mishipa ya damu.Tufaa lina “Pectin” ya kutosha ambayo husaidia kurekebisha kiasi cha sukari katika damu taratibu na kwa mpangilio mzuri.

¨      Parachichi(Avocardo)- hurekebisha kiwango cha sukari, husawazisha kiwango cha mafuta ndani ya damu na cholesterol

¨      Tikitimaji(watermelon)-lina sukari kidogo sana, lina homoni inayoshusha sukari(glucokinin), huleta hali ya kushiba haraka na kupunguza unene.

¨      Matango- yana wanga kidogo sana,yana homoni ya mimea inayosaidia kupunguza sukari

¨      Embe-hupunguza sukari katika ugonjwa wa kisukari cha ukubwani, huleta afya ya mishipa na kudhibiti athari za kisukari kwenye mishipa ya damu.

¨      Ndizi –sukari yake inaingia ndani ya damu taratibu sana, ni vizuri kuzitumia pamoja na mazoezi ya mwili, ndizi zina madini ya potassium kwa wingi hivyo hudhibiti shinikizo la damu( hypertension)

  • Chumvi- punuza sana chumvi katika chakula ili kudhibiti shinikizo la damu.

 

 Vyakula kula kwa wingi( taa ya kijani)

  • Mboga mboga zina wanga kidogo, huzuia na kupunguza unene.
  • Vitunguu maji na majani yake- hupunguza sukari kwa sababu vina insulin ya mimea(Glycoquine)
  • Majani ya maharage- hupunguza sukari mwilini kwa wagonjwa wa kisukari.
  • Kabeji- ina homoni inayofanya kazi kama insulin, ina wanga kidogo,inaleta hali ya kushiba haraka na inaimarisha afya ya mishipa ya damu na kupunguza hatari ya kupata ugonjwa wa moyo na shinikizo la damu.
  • Spinach- hupunguza sukari, ina madini na vitamin.
  • Karoti-husaidia sukari kuingia katika misuli na kutumika katika seli zenye mafuta (Adipocytes)
  • Uyoga- hurekebisha kiwango cha sukari na kupunguza hitaji la insulin.
  • Bamia- hurekebisha kiwango cha sukari na kupunguza hitaji la insulin

Kumbuka

  • Mboga ziliwazo bila kuchemshwa sana na matunda vina faida zaidi.
  • Usile chakula kilichokufa( kuoza , kuungua au kuchemshwa sana)
  • Kumbuka kunywa maji mengi
  • Kula milo midogomidogo mara 5 au 6 kwa siku badala ya milo mitatu mikubwa.

References

  • Diabetes, Natural Life Health series, Character Building Books, London- taken from “Proof positive” by Dr. Neil Nedly, M.D.
  •  Diabetes, Wikipedia, The free Encyclopedia, accessed on 31st july, 2009.
  • Encyclopedia of Food and their Healing Power, George D. Pamplona-Roger, M.D., June 2008, 8th Print.
  •  Guide to Natural Remedies for Health and Well-being, Enrique Garza., B.Sc., C.Ht
  • Plant insulin or glucokinin: A conflicting issue, Brazilian Journal of plant physiology print version ISSN 1677-0420, Vol.15, no. 2, Londrina, May/Aug, 2003., (www.scielo.br/scielo.php) accessed on 1st Aug 2009.
  • Smoking and Diabetes,yourtotalhealth.ivillage.com/smoking…,accessed on 31st July, 2009.
  • World Conference on Orisa Tradition and Culture, Experts find Kidney Beans effective in lowering blood sugar level, renal insufficiency, Guardian Newspapers, Lagos, Nigeria, 17th Sept 2004. (www.yerubareligion.org/news/...) accessed on 31st July 2009.
January 16, 2013
Next »

Comments (4)

kitwanamhewa22@gmail.com (dodoma) said:
Safi sana nijuze mambo
March 26, 2014
(Anonymous) said:
duuh,safi sana
March 26, 2014
i. k. bavu (kimara, dsm) said:
Ni MS Ada muhimu kwa jamii. Hongera.
March 27, 2014
Thomas Alfredy (Iringa) said:
Mm jamani Nina tatizo hlo sasa takribani siku tatu sijalala naombeni msaada wenu nahangaika sana.Mungu Adam indie
July 27, 2017

Add a comment

Your name:
Your location:
Your email:
(optional)
Your email address will not be published.